VITUKO haviishi kwenye Ligi Kuu Soka Zanzibar (ZPL), safari hii, Mwanaspoti imeshuhudia kubwa zaidi wakati wa mechi za ligi hiyo zikiendelea kwenye Viwanja vya Mao, Unguja.

Achana na vurugu zilizokuwa zikiibuka kwa kasi msimu uliopita kwa waamuzi kushambuliwa na mashabiki wakati mwingine hata viongozi ambapo baadaye Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF) likaipiga faini klabu ya KVZ kiasi cha Sh3 milioni, kufuatia vurugu zilizotokea katika mechi ya nusu fainali ya Kombe la Shirikisho (ZFF Cup) dhidi ya Uhamiaji.

Wakati mzunguko wa tano wa Ligi Kuu Zanzibar (ZPL) msimu huu ukiendelea, kumejitokeza tabia kwa baadhi ya viongozi wa mabenchi ya ufundi na hata mashabiki kutokuwa na utulivu wakifanya vitendo vinavyoashiria kuingilia mchezo.

MA 01

Wakati mechi kati ya Mwembe Makumbi na Chipukizi iliyochezwa Oktoba 20, 2025 kwenye Uwanja wa Mao A ikiendelea, Mwanaspoti ilishuhudia baadhi ya vongozi wa benchi la ufundi wa Mwembe Makumbi wakitoka eneo lao na kwenda kwa mashabiki kuwanunulia maji ya kunywa. Tukio kama hilo limejirudia katika mechi ya Malindi na JKU iliyochezwa Oktoba 21, 2025 uwanjani hapo.

Mbali na hilo, wakati Mwembe Makumbi ikifanya mabadiliko ya mchezaji, shabiki mmoja alitoka jukwaani na kuingia uwanjani kumsindikiza hadi kwenye benchi, kitendo ambacho hakiruhusu.

Akitoa ufafanuzi wa hilo, Mtendaji Mkuu wa Bodi ya Ligi Zanzibar (ZBL), Issa Kassim, amesema hayo yote kisheria hayatakiwi, pia timu zenyewe zinashindwa kudhibiti mashabiki wao huku akikiri changamoto hiyo inachangiwa na kukosekana kwa uzio uwanjani hapo.

Kuhusu biashara zinazoendelea katika mabenchi ya ufundi wakati mechi zikichezwa, amesema kila benchi lina meneja ambaye anahusika kuthibiti hilo na bodi hiyo inapinga vikali klabu kufanya matukio yasiyofaa michezoni.

“Licha ya kuwa uwanja wetu hauna uzio, isiwe sababu ya kufanya vitendo ambavyo vipo nje ya sheria za mpira na ikitokea klabu itakiuka itapewa adhabu kwa mujibu wa kanuni ya mashindano,” amesema Issa.

MA 02

Msimu uliopita, Viwanja vya Mao hakukuwa na uzio wowote hali iliyokuwa ikichangia zaidi matukio ya mashabiki kuingia sehemu ya kuchezea kirahisi na kufanya vurugu, lakini msimu huu, baadhi ya maeneo kuna uzio, ingawa upande wa Jukwaa Kuu haujawekwa na ndipo panapofanyika matukio hayo kwa wingi hivi sasa licha ya kwamba kuna walinzi wa uwanjani (Steward) lakini wanashindwa kuwadhibiti kutokana na mazingira yalivyo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *