Umoja wa Ulaya (EU) umeongeza kampuni kadhaa za China katika orodha yake ya vikwazo dhidi ya Urusi, zikiwemo viwanda viwili vikubwa vya kusafisha mafuta—Liaoyang Petrochemical na Shandong Yulong Petrochemical—pamoja na kampuni ya biashara ya Chinaoil Hong Kong, tawi la PetroChina. Hatua hii imetangazwa kupitia Jarida Rasmi la EU, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuzuia mapato ya mafuta yanayoiwezesha Russia kufadhili vita yake nchini Ukraine.
Viwanda hivyo viwili vya China vina uwezo wa kusafisha mafuta takribani mapipa 600,000 kwa siku, sawa na asilimia 3 ya uwezo wote wa China wa kusafisha mafuta. Uamuzi wa EU unadhihirisha wasiwasi unaoongezeka kwamba baadhi ya kampuni za nishati za China zinaisaidia Russia kuepuka athari za vikwazo vya Magharibi.
Hatua hii imekuja sambamba na msimamo wa nchi wanachama wa Kundi la G7, ambao wamekuwa wakifanya kazi kwa pamoja kuhakikishaUrusi inapungukiwa na mapato kutoka kwenye mauzo ya mafuta na gesi. Lengo kuu ni kuikatia Moscow njia za kujipatia fedha za kufadhili shughuli za kijeshi nchini Ukraine.
Mbali na viwanda hivyo viwili, EU pia imeiweka kwenye orodha ya vikwazo kampuni ya Tianjin Xishanfusheng International Trading Co ya China. EU imesema kampuni hiyo imekuwa ikiisaidia Urusi kukwepa vikwazo kwa kusafirisha bidhaa zenye asili ya Umoja wa Ulaya kupitia njia za mlango wa nyuma.
China yapinga vikali, yaapa kulinda maslahi yake
Serikali ya China imelaani hatua hiyo, ikieleza “kutoridhishwa na upinzani mkali” dhidi ya uamuzi huo wa EU. Msemaji wa Wizara ya Biashara ya China alisema kuwa Beijing itachukua hatua kulinda haki na maslahi halali ya kampuni zake.
“China inaitaka EU kuacha mara moja kuorodhesha kampuni zake na kutozidi kuendelea na njia isiyo sahihi,” alisema msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya China katika taarifa rasmi.
Kwa mujibu wa EU, kampuni za Yulong, Liaoyang na Chinaoil ni wanunuzi wakubwa wa mafuta ghafi kutoka Urusi na hivyo kutoa chanzo kikubwa cha mapato kwa serikali ya Moscow.
Yulong, ambayo ni kiwanda kipya zaidi cha kusafisha mafuta nchini China chenye uwezo wa mapipa 400,000 kwa siku, imetajwa kuwa miongoni mwa wateja wakubwa wa mafuta ya Urals na ESPO kutoka Urusi.
Kiwanda cha Liaoyang Petrochemical, kilichoko kaskazini mashariki mwa China, kina uwezo wa mapipa 200,000 kwa siku na kinafanya kazi kama kampuni ya kusafisha mafuta na kemikali.
Hadi sasa, kampuni hizo zote hazijatoa maoni kuhusu hatua ya Umoja wa Ulaya, huku mvutano wa kidiplomasia kati ya Beijing na Brussels ukiendelea kuongezeka.