Wafanyakazi wa sekta ya umma na binafsi, wametakiwa kuwa mstari wa mbele katika kujitokeza kupiga kura katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 29, mwaka huu. Kwa mujibu wa Shirikisho la Vyama vya VWafanyakazi Tanzania (TUCTA), ni muhimu wafanyakazi kutimiza haki yao ya kupiga kura, kwa kuwa ndio msingi wa kupatikana viongozi watakaosimamia maslahi yao.
Wito huo, umetolewa leo, Alhamisi na Rais wa TUCTA, Tumaini Nyamhokya alipozungumza na waandishi wa habari jijini Arusha.
Amesema nchi iko salama hivyo, wafanyakazi wanapaswa kujitokeza kwenda kupiga kura, kuwachagua viongozi watakaosikiliza na kujali maslahi yao.
“Nitumie fursa hii kuwasisitiza kuendelea kuwashawishi wafanyakazi wa Arusha na Tanzania nzima tujitokeze kwa wingi Oktoba 29, kwenda kupiga kura ili tuweze kuwachagua viongozi wetu wanaojali maslahi yetu,” amesema.
Amesema kupiga kura ni haki ya mwananchi na kwa kuwa siku hiyo itakuwa ya mapumziko, wafanyakazi wahakikishe wanakwenda kupiga kura na kuendelea na shughuli zao nyingine.
“Kapigeni kura Oktoba 29, tuwachague viongozi ambao tuna ubakika ukienda kuzungumza jambo linatekelezwa. Viongozi ambao sauti ambayo sisi tunatoa kwa niaba yenu zitasikilizwa,” amesema Nyamhokya.
#StarTvUpdate