
Wanamgambo wa Kikosi cha Msaada wa Haraka (RSF) leo wamefanya wimbi la mashambulizi ya ndege zisizo na rubani (droni) katika Uwanja wa Ndege wa Khartoum kwa siku ya tatu mtawalia.
Gazeti la Sudan News, limewanuku mashahidi na kuripoti kuwa ndege saba zisizo na rubani zililenga Uwanja wa Ndege wa Khartoum na maeneo ya karibu kusini mwa mji mkuu, na kusababisha hofu kubwa miongoni mwa raia.
Sauti za miripuko zimesikika leo katika Uwanja wa Ndege wa Khartoum. Wanamgmbao wa RSF walianza kushambulia uwanja huo wa ndege pamoja na meneo mengine nyeti katika jimbo la Khartoum Jumanne wiki hii, siku moja kabla ya uwanja huo kufunguliwa tena baada ya kufungwa kwa zaidi ya miaka miwili.
Jana Jumatano Uwanja wa Ndege wa Khartoum ulipokea ndege yake ya kwanza ya abiria. Duru za usalama zimesema kuwa hakuna madhara yaliyotokea kwenye uwanja huo baada ya mashambulizi ya RSF.
Gazeti la Rakoba limeripoti kuwa, mashambulizi ya karibuni dhidi ya maeneo muhimu na nyeti ya Sudan yanaashiria mabadiliko katika asili ya mzozo kati ya wanangambo wa RSF na jeshi la Sudan kuanzia katika makabilianao ya nchi kavu hadi kutumia droni kama wenzo wa kijeshi na mashinikizo ya kisiasa.
Hadi sasa wanamgambo wa RSF hawajatoa taarifa yoyote kuhusu kuhusika na mashambulizi hayo.
Jeshi la Sudan na waasi wa RSF wamekuwa wakipigana tangu mwezi Aprili mwaka 2023; vita ambavyo hadi sasa vimeuwa watu zaidi ya 20,000 na kusababisha wengine milioni 14 kuwa wakimbizi.