Unguja. Zikiwa zimebaki siku sita kabla ya kufanyika uchaguzi mkuu, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imetoa mafunzo maalumu ya matumizi ya karatasi za kupigia kura kwa mfumo wa kugusa na kutambua kwa vidole, maarufu kama nukta nundu (Tactile), kwa ajili ya watu wasioona ili kuhakikisha kila mtu anapata fursa ya kupiga kura.
Akizungumza leo Oktoba 23, 2025 wakati wa ufunguzi wa mafunzo hayo, Kamishna wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar, Idrissa Haji Jecha amesema hatua hiyo inalenga kuhakikisha watu wenye ulemavu wa kuona wanatumia haki yao ya kikatiba kwa uhuru na bila utegemezi kwa wengine.
“Changamoto inayowakabili ndugu zetu hawa imekuwa ni utegemezi kwa watu wengine kuwasaidia kupiga kura, jambo ambalo linapunguza faragha na uhuru wao wa kuchagua viongozi wanaowataka,” amesema.
ZEC tayari imetengeneza kifaa maalumu kwa ajili ya watu wasioona (tactile ballot folder) na imeanza kutoa mafunzo kuhusu namna ya kutumia kifaa hicho.
“Tume inajivunia kuwa na nyinyi katika safari ya kuimarisha usawa, heshima na haki kwa kila raia wa nchi yetu,” amesema Kamishna Idrissa.
Kwa upande wao, washiriki wa mafunzo hayo waliipongeza ZEC kwa hatua hiyo muhimu, wakisema imeonyesha dhamira ya kweli ya kuhakikisha kila raia, bila kujali hali yake anashiriki ipasavyo katika uchaguzi mkuu.
“Kwa hili tunapongeza sana, maana tumekuwa wategemezi wa kupigiwa kura, jambo ambalo huwa linaondosha usiri ambayo ni haki yetu kikatiba,” amesema Ahmed Hassan.
Naye Amina Msellem amesema wamekuwa wakikabiliwa na changamoto hiyo kwani wakati mwingine inakuwa vigumu kuamini kama wanachaguliwa watu wanaowataka kwa sababu hawaoni.
Wasioona wakipewa mafunzo ya kutumia kifaa maalumu kitakachowasaidia kupiga kura bila kutegemea msaada wa mtu yeyote Ili kulinda faragha yao
“Kweli unaweza kumwambia mtu hata kama ni ndugu yako kuhusu kiongozi unayemtaka lakini hujui yeye anafikiria nini, sasa hilo litakuwa limeondoka na unakuwa na uhakika unayemtaka ndiye uliyempigia kura,” amesema.
Mbali na wasioona, ZEC imesema itahakikisha makundi yote ya watu wenye mahitaji maalumu yanashiriki kikamilifu katika Uchaguzi Mkuu wa mwaka 2025 bila kubaguliwa.
Jecha amesema tume imejiandaa kikamilifu kuhakikisha haki ya kila raia ya kupiga kura inalindwa na kutekelezwa kwa usawa.
Amesema Tume hiyo inatambua umuhimu wa watu wenye ulemavu, wazee na makundi mengine maalumu katika mchakato wa kidemokrasia, hivyo imeweka mikakati madhubuti ya kuhakikisha hakuna anayebaki nyuma.
“Tume inatambua kuwa kila raia ana haki sawa ya kushiriki katika maamuzi ya taifa, tutahakikisha watu wenye ulemavu wanapata msaada unaostahili siku ya kupiga kura,” amesema Jecha.
Ametoa wito kwa jamii kushirikiana na Tume hiyo kwa kutoa taarifa za watu wenye mahitaji maalumu katika maeneo yao ili kuwezesha maandalizi bora kabla ya siku ya kupiga kura.
Kwa upande wake, Mkuu wa Kurugenzi ya Elimu ya Wapigakura na Mawasiliano kwa Umma, Juma Sanifu Juma akiwasilisha mada kuhusu nafasi ya makundi maalumu katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu, alibainisha kuwa ZEC inatekeleza sera ya kuyapa kipaumbele makundi hayo.
Sanifu amesema Tanzania ikiwemo Zanzibar imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa inayolenga kulinda haki za watu wenye ulemavu, hivyo ni wajibu wa kila taasisi kuhakikisha makubaliano hayo yanatekelezwa kwa vitendo.
Mmoja wa washiriki wa mkutano huo, Abdul Abasi Ali amepongeza ZEC kwa hatua yake ya kuwashirikisha watu wenye ulemavu kuanzia hatua za awali za maandalizi ya uchaguzi hadi mwisho wa mchakato.
Ameiomba Tume hiyo kushirikiana na Msajili wa Vyama vya Siasa kuhakikisha kila chama kina mtaalamu wa kushughulikia masuala ya watu wenye ulemavu wakati wa kampeni, ili kuepuka changamoto wanazokutana nazo wanapohudhuria mikutano ya kisiasa.
Naye Rawiya Simai Jecha kutoka Jumuiya ya Wanawake Wenye Ulemavu Zanzibar, aliitaka jamii kuacha kufanya vurugu wakati wa uchaguzi, akisema vitendo hivyo huwanyima fursa watu wenye ulemavu kushiriki kwa amani.
“Wapo wengi miongoni mwetu hawawezi kukimbia wala kujihami wakati wa vurugu, ni vyema uchaguzi ukafanyika kwa amani ili kila mmoja aweze kushiriki,” amesema Rawiya.
Kwa upande wake, Hassan Haji Kombo amesema idadi ya watu wenye ulemavu wanaotarajiwa kupiga kura mwaka huu ni ndogo, hivyo ameiomba ZEC kushirikiana na taasisi za watu wenye ulemavu ili kuongeza ushiriki.
Kombo amebainisha kuwa kwa mujibu wa sensa ya mwaka 2022, kundi la watu wenye ulemavu ni kubwa, lakini ni wachache wanaojitokeza kujiandikisha au kushiriki kikamilifu katika uchaguzi.
Biubwa Said Abdulahim, mmoja wa washiriki wa mkutano huo, alisisitiza umuhimu wa elimu endelevu kwa wapiga kura wenye mahitaji maalumu ili wajue haki zao na wajibu wao katika michakato ya uchaguzi.
Naye Abdallah Alawi Abdallah, Katibu wa Jumuiya ya Viziwi Zanzibar, amependekeza kuwepo kwa wakalimani wa lugha ya alama katika vituo vyote vya kupigia kura ili kuhakikisha kundi hilo halinyimwi haki ya kuelewa taratibu za kupiga kura.