
Dar es Salaam. Azam imeingia hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa staili ya aina yake baada ya leo kuichapa KMKM kwa mabao 7-0 katika Uwanja wa Azam Complex, Dar es Salaam.
Matokeo hayo ya leo yameifanya Azam isonge mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0 iliopata katika mechi mbili za raundi ya pili ya mashindano hayo.
Aidha, ushindi huo umeihakikishia Azam kuzoa Sh35 milioni kama zawadi ya Goli la Mama iliyoahidiwa na Rais Samia Suluhu Hassan katika mashindano ya kimataifa.
Ikumbukwe Rais Samia aliahidi Sh5 milioni kwa kila bao litakalofungwa na timu za ndani katika michuano ya CAF.
Mabao hayo yalitiwa kimiyani na Idd Selemani ‘Nado’ aliyetangulia kuifungia Azam FC bao katika dakika ya 22 akimalizia kwa shuti la mguu wa kulia pasi ya Feisal Salum ‘Fei Toto.
Azam ilisubiri kwa dakika nne tu kupata bao la pili katika dakika ya 26 kupitia kwa Jephte Kitambala aliyefunga bao hilo kwa kuunganisha pasi ya Nado.
Dakika ya 29, Kitambala aliipachikia Azam bao la tatu akimalizia kwa shuti la mguu wa kulia pasi ya kupenyeza kutoka kwa Fei Toto.
Mabao hayo manne yalidumu hadi pale mwamuzi Idris Osman kutoka Somalia alipoamuru kumalizika kwa dakika 45 za kipindi cha kwanza.
Kipindi cha pili kilianza kwa KMKM kufanya mabadiliko ya wachezaji watano ambapo iliwatoa Adam Shaban, Ally Saidy, Jasper Babalika, Haji Juma na Nassir Abdallah na kuwaingiza Mwinyi Mwinyi, Samir Said, Martin Londo, Mukrim Hassan na Yahya Simai.
Mabadiliko hayo hayakuwa na msaada wowote kwa KMKM kwani ilijikuta ikiendelea kuruhusu mvua ya mabao katika kipindi hicho cha pili huku pia ikizidiwa umiliki wa mchezo.
Safu ya ulinzi ya KMKM katika kipindi hicho cha pili imeonekana kushindwa zaidi kuwadhibiti washambuliaji wa Azam FC na ikajikuta ikiruhusu Sopu kufunga mabao mawili na lingine likifungwa na Pascal Msindo kufanya imalize mechi huku nyavu zake zikiwa zimetikiswa mara saba.
Katika kipindi hicho cha pili, Azam imewatoa Sopu, Yahya Zaydi, Himid Mao, Lusajo Mwaikenda na Jephte Kitambala na kuwaingiza Zidane Seleli, Sadio Kanoute, James Akaminko, Nathaniel Chilambo na Nassor Saadun.
Hiyo imekuwa ni mara ya kwanza kwa Azam FC kutinga hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika tangu klabu hiyo ilipoanza kushiriki Ligi Kuu Tanzania Bara mwaka 2008.
Azam FC inakuwa timu ya nne kutinga hatua hiyo kwa hapa nchini ambapo kabla yake, timu zilizowahi kucheza makundi ya mashindano ya Klabu Afrika ni Yanga, Simba na Namungo FC.
Azam sasa inasubiria droo ya hatua ya makundi ya mashindano hayo iliyopangwa kufanyika Novemba 3, 2025 huko Johannesburg, Afrika Kusini.