Meneja wa zamani wa Liverpool na Real Madrid, Rafa Benitez ataandika rekodi ya kuwa Meneja wa kwanza kulipwa fedha nyingi zaidi katika historia ya Ligi Kuu Ugiriki ikiwa mpango wake wa kujiunga na Panathinaikos utakamilika hivi karibuni.
Benitez mwenye umri wa miaka 65 kwa sasa hana kazi tangu alipoachana na Celta Vigo Machi 12, 2024 baada ya timu hiyo ya Hispania kupata ushindi katika mechi tano tu kati ya 28 za Ligi Kuu Hispania ‘La Liga’ jambo lililoiacha ikiwa pointi mbili juu ya mstari wa kushuka daraja.
Ripoti kutoka Ugiriki zimebainisha kwamba Benitez anakaribia kujiunga na Panathinaikos kwa mkataba wa miaka miwili.
Katika mkataba huo, Benitez atalipwa kiasi cha Pauni 3.47 milioni (Sh11.5 bilioni) kwa mwaka, kiasi ambacho ni kikubwa zaidi kuwahi kulipwa kwa meneja au kocha katika ligi hiyo.
Kujiunga huko kwa Benitez na timu ya Panathinaikos kutamfanya pia awe meneja aliyezifundisha timu nyingi zaidi ambapo klabu hiyo ya Ugiriki itakuwa ya 17 kwake.
Miongoni mwa timu hizo ni zile zinazoshiriki Ligi kubwa duniani za Italia, England na Hispania.
Katika timu hizo 16 ambazo Benitez amefundisha, ameshinda mataji mawili ya La Liga, Kombe moja la UEFA, taji moja la Ligi ya Mabingwa Ulaya, taji moja la FA, taji moja la Klabu Bingwa ya Dunia na taji moja la Europa League.
Timu ambazo Benitez amewahi kuzifundisha
Real Madrid C
Real Madrid B
Valladolid
Osasuna
Extremadura
Tenerife
Valencia
Liverpool
Inter Milan
Chelsea
Napoli
Real Madrid
Newcastle United
Dalian Professional
Everton
Celta Vigo