Mgombea ubunge Jimbo la Bukombe ambaye pia ni Naibu waziri Mkuu, Doto Biteko amemtaka mgombea ubunge wa Jimbo la Busanda kuwavumilia wananchi wake na kuwatumikia bila kujali pasipo ubaguzi atakaposhinda ubunge.

Biteko ametoa wito huo leo Oktoba 24, 2025 katika Kata ya Bukoli, Jimbo la Busanda mkoani Geita wakati akifunga Kampeni za uchaguzi katika Jimbo hilo ambapo alikuwa mgeni rasmi.

“Wasikilize watu hawa, kuna wengine watakuudhi wavumilie, akitokea mtu anakuchukia kwa kuwachukia watu mwachie Mwenyezi Mungu, hata ukimaliza kipindi chako cha ubunge rudi Busanda, wasikilize wananchi uwasaidie.”

Pia, Biteko ametoa rai kwa wananchi wa Jimbo hilo, kumpa ushirikiano mgombea ubunge wa Jimbo hilo Dk Jafari Seif, akifafanua kuwa licha ya mgombea huyo kutokuwa na mpinzani lakini amefanya kampeni maeneo yote kwa uaminifu.

“Mgombea ubunge wenu ana bidii ya kazi, anajituma amepita bila kupingwa agekuwa mwingine angelala ukimuuliza vipi anasema nilishamaliza kazi, mbunge mzuri anatengenezwa na wananchi wake akifanya vizuri mnamwambia songa mbele akifanya vibaya muiteni mumuonye,” amesema.

Aidha Biteko ameongeza kuwa nchi yoyote ya kidemokrasia, hupata viongozi wake kupitia uchaguzi hivyo kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi Oktoba 29, 2025 kumchagua kiongozi atakayewaletea maendeleo.

“Bukoli imetoka mbali wale tuliozaliwa maeneo haya tunafahamu, wakati mimi namaliza Shule ya Msingi Nyaruyeye hatukuwa na sekondari iliyokuwepo ni Shule ya Bukoli lakini kwa sasa tuna shule 16, hatukuwa na vituo vya afya,” amesema.

Ameongeza kuwa, “Shule mnazoziona Serikali imefanya kazi tumekuja kufunga ili tukumbushane yaliyofanywa na Serikali na tumekuja kuwaomba kura ili tulete maendeleo zaidi,” amesema Biteko.

Mgombea ubunge Jimbo la Busanda, Dk Seif ametumia mkutano huo kunadi ilani ya chama hicho akibainisha kuwa uko uhitaji wa kuongeza shule za sekondari, barabara na miundombinu ya afya.

“Jimbo la Busanda limeongezewa vituo vya Afya vitatu lakini katika ilani hii tunatarajia kupata hospitali ya wilaya itakayojengwa Nyarugusu, hivyo niwatoe hofu wananchi wa Busanda tuna shule 16 za sekondari lakini katika shule hizo, tuna shule moja pekee ya kidato cha sita hivyo tukishinda kwa ilani hii ya uchaguzi inayokwenda kuleta maendeleo tuongezewe shule za high school kwakuwa ndiyo wanaotuhudumia kwenye vituo vyetu vya afya,” amesema.

Mgombea ubunge Jimbo la Geita Vijijini, Joseph Kasheku ‘Msukuma’ ambaye pia amehudhuria mkutano huo  ameonya kuwa licha ya kuwa mgombea ubunge hana mpinzani isiwe kigezo cha wananchi kupuuzia uchaguzi.

“Wakati wa Hayati Rais John Magufuli kwenye uchaguzi wa 2020 alikuwa anakubalika lakini tukajipa imani kuwa tutashinda kwa kishindo lakini baada ya uchaguzi tulipotoka kuapa nilikuwa watatu kutoka mwisho hivyo hata kama yuko peke yake tujitokeze kwa wingi kupiga kura,” amesema Msukuma, mgombea ubunge Jimbo la Geita Vijijini.

Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Geita, Nicholaus Kasandamila amewahimiza wananchi wa Busanda kujitokeza kwa wingi siku ya kupiga kura huku wakidumisha amani na utulivu hata baada ya kupiga kura.

“Kupitia uchaguzi huu tutengeneze mkoa wenye amani, tushirikiane, tupendane na tuvumiliane, CCM ni nzuri sana. Tarehe 29 Oktoba twende tukajipe raha kwenye vituo vya kupigia kura,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *