Dar wa Salaam. Lengo kuu la sharia ya Kiislamu ni kutimiza manufaa na kuzuia madhara. Sharia hii tukufu imehakikisha haki za watu binafsi na jamii nzima za kibinadamu. 

Miongoni mwa uzuri wa sharia ya Kiislamu ni kulinda haki za wanyonge, ikiwemo makundi maalumu kama watoto. 

Kwa ajili yao, Uislamu umeweka kanuni za jumla pamoja na sharia maalumu zenye maelezo ya kina, ikiwemo sharia za ulezi na utunzaji wa matoto (Al-Hadhana). 

Malezi katika Uislamu ni miongoni mwa mambo mazuri sana yaliyomo katika sharia hii tukufu.

Wanazuoni wa  Sharia ya Kiislamu (Fuqahaau) wa zamani na wa kisasa wametofautiana katika kueleza maana ya  malezi (Al-Hadhana) kwa maneno, ingawa maana yao kimsingi ni moja. Baadhi ya wanazuoni wa Kishafi  wameyaelezea malezi kuwa ni kumuangalia na kumtunza yule asiyeweza kutofautisha mambo au kujisimamia, kwa kumlea kwa yale yanayomfaa, na kumlinda dhidi ya mambo yanayoweza kumuangamiza.

Malezi  na utunzaji wa mtoto mdogo na kusimamia mambo yake ni jukumu la wajibu la wazazi wawili wanapokuwa bado katika ndoa.

 Ila mama ana nafasi kubwa zaidi katika haki ya malezi, kwani mara nyingi ndiye anayebeba jukumu la malezi kwa huruma na upendo. Baba naye ana nafasi, lakini ni ndogo zaidi kulingana na wajibu wa kijinsia na kimaumbile. Allah Mtukufu ameutaja wajibu huu ndani ya Qur’an: “Na useme: Ee Mola wangu, warehemu wazazi wangu kama walivyonilea utotoni.” (17:24). 

Aya hii tukufu imeonesha wazi kuwa malezi ni jukumu la lazima la wazazi katika kipindi cha utotoni. 

Hata hivyo, iwapo wazazi watatengana, suala la nani anayepewa haki ya kulea mtoto linaibuka: je, ni mama au baba? Na je, haki hiyo inamhusu mtoto wa kiume au wa kike?

Haki ya malezi kipindi cha talaka

Malezi na utunzaji wa mtoto unakuwa kwa wazazi wote wawili iwapo ndoa yao bado ipo. Lakini wakitengana kwa talaka, basi  ulezi wa mtoto unakuwa ni haki ya mama na jukumu la baba ni kuhudumia kwa makubaliano ya wanazuoni wote, kwa mujibu wa kauli ya Mtume ( Rehema na amani ziwe juu yake) aliyomwambia mwanamke aliyetalikiwa, na mtalaka wake akataka kumchukua mtoto aliyezaa naye: “Wewe (mke) una haki zaidi ya kumlea mtoto, maadamu hujaolewa.” 

Hivyo, kauli hii ya Mtume wa Allah ni hukumu ya lazima inayopaswa kutekelezwa. Iwapo mama ataolewa na mume mwingine ambaye si baba wa mtoto, basi haki hii ndio itaondolewa kwake.. 

Imamu Bukhari – Allah amrehemu- amenukuu Hadithi ya Al-Barrau bin Azib kuhusu haki ya kumlea binti wa Hamza (Allah Amridhie). Ali (Allah Amridhie) alisema: “Mimi nina haki zaidi naye, kwani yeye ni binti wa ami yangu. Huku Jafar  akisema: “Ni binti wa ami yangu, na mama yake mdogo ni mke wangu.” Zaid naye  akasema: “Yeye ni binti ya ndugu yangu.” 

Mtume  wa Allah akamhukumia mtoto huyo kwenda kulelewa kwa mama yake mdogo akasema: “Mama yake mdogo ni kama mama mzazi.” Hadithi hii inaonyesha uhalali wa  malezi kwa mama mdogo, na kwamba katika mgogoro anapewa kipaumbele kuliko ndugu wengine wa karibu wa mtoto.

 Aidha, miongoni mwa athari  na kauli za Masahaba wa Mtume zilizopokewa kuhusu jambo hili ni simulizi inayo muhusu Umar bin al-Khattab (Allah amridhie), ambaye alimtaliki mke wake wa Kiansar baada ya kuzaa naye mtoto aitwaye Asim. 

Baada ya mwanamke huyo kuolewa tena na mume mwingine, mtoto alilelewa na bibi yake mzaa mama. Umar (siku moja) alipokutana na mtoto  wake barabarani, alimkumbatia kwa mapenzi, lakini bibi yake (mzaa mama) alizozona na Umar na kumdai mtoto huyo.

Wakapeleka shauri hilo kwa khalifa (kiongozi) Abubakr as-Siddiq (Allah amridhie), naye akamhukumia mtoto abaki kwa bibi yake mzaa mama.

Sharti za mlezi

Miongoni mwa sharti ya mlezi: Mosi, awe mtu mzima, kwani mtoto mdogo hawezi kumlea mwenzake. Pili, awe na akili timamu. Tatu, awe na uwezo wa kulea vizuri Nne, awe mwadilifu na mwaminifu katika malezi. 

Tano,uislamu wa mlezi si sharti la msingi katika malezi; kwa sababu huruma ya asili kwa mtoto haipotei kwa tofauti ya dini. Ila kama kuna hofu kwamba mtoto ataathiriwa na ibada za dini nyingine.

Wanawake kwa ujumla wana haki zaidi ya malezi kuliko wanaume, na malezi hayo huanza tangu kuzaliwa kwa mtoto. Hata hivyo, muda wa kumalizika   kwa wanawake baada ya wanandoa kuachana, unatofautiana kati ya madhehebu ya Kiislamu. 

Kwa mujibu wa madhehebu ya Kishafi, malezi huendelea kwa mtoto  awe wa kiume au wa kike hadi anapofikia umri wa kutambua mambo (utambuzi).

 Umri huu unakadiriwa kuwa kati ya miaka saba hadi minane kwa kawaida. Mtoto akifika umri huu, hupewa haki ya kuchagua  kuishi na mmoja kati ya wazazi wake; akimchagua mmoja, basi hukabidhiwa kwake.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *