WINGA wa Mashujaa FC, Salum Kihimbwa amesema msimu huu ni dume, lakini anataka kuendeleza ubora wake wa msimu uliopita na kufunga mabao zaidi.

Msimu uliopita Kihimbwa akiwa na Fountain Gate alimaliza na mabao manne na asisti tano, lakini ndoto yake msimu huu ni kuhakikisha anafunga 10 na asisti 10 ingawa bado hajafungua akaunti ya mabao.

“Bado nina muda wa kupambana ili kuendeleza ubora wa kiwango nilichokuwa nacho msimu uliopita, najipanga naamini nitakuwa na mchango mkubwa kikosini,” amesema.

Msimu huu hadi sasa amecheza mechi tano, huku nne alitokea benchi na moja alianza na amesema hilo linampa chachu ya kujituma kwa bidii kujihakikishia namba kikosi cha kwanza.

Mashujaa imeshinda mechi moja, imefungwa mbili na sare mbili na ipo nafasi ya nane katika msimamo na pointi tano.

“Rekodi ya mabao saba na asisti 10 niliyafunga nikiwa na Mtibwa Sugar katika michuano ya Kombe la FA na timu ilinyakua ubingwa, natamani nilifanye hilo msimu huu,” amesema.

Amesema ushindani uliopo katika timu unamsaidia kumjenga na kufanya mazoezi na kuepuka kubweteka na kila mchezaji anapambania nafasi ya kucheza.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *