AZAM FC inayonolewa na kocha Florent Ibengé, imetinga hatua ya makundi kwa kishindo, baada ya kuifunga KMKM kwa jumla ya mabao 9-0, ugenini na nyumbani.

Mechi iliyopigwa leo Oktoba 24, 2025 kwenye Uwanja wa Azam Complex, uliopo Chamazi jijini Dar, imeshinda mabao 7-0 dhidi ya KMKM, wakati mechi ya kwanza ilishinda kwa mabao 2-0, ikipigwa Uwanja wa New Amaan Complex, uliopo Zanzibar, wikiendi iliyopita.

AZA 01

KIPINDI CHA KWANZA 4-0

Katika kipindi cha kwanza, Azam ilitumia dakika sita kupata mabao matatu ya harakaharaka, ukiacha kosakosa zilizokuwepo, kisha wakafunga bao la nne dakika ya 43.

Fei Toto alitoa pasi ya bao la kuongoza lililofungwa na Iddy Nado dakika 23 ambapo alikwenda kushangilia na wenzake kisha akaenda kumkumbatia kocha Ibenge.

Dakika ya 26, Nado alitoa pasi ya bao la pili lililofungwa na Jephte Kitambala na dakika ya 29 Fei Toto alitoa pasi kwa Kitambala akiifungia Azam bao la tatu, hivyo mchezaji huyo kafunga mabao mawili ndani ya dakika tatu na kutoa asisti moja.

Baada ya Kitambala kufunga bao lake la pili, alipiga goti kishika Fei Toto akauweka mguu wake na kufuta kiatu chake.

Dakika ya 43, Nado alifunga bao la nne, mpira ulianza kwa Abdul Suleiman ‘Sopu’ aliyempa mpira Kitambala akatoa pasi ya mwisho ya bao, hivyo dakika 45 za kipindi cha kwanza Azam FC ilikuwa inaongoza kwa mabao 4-0.

AZA 02

KIPINDI CHA PILI

Dakika ya 47, Azam ilipata bao la tano, lililofungwa kwa kichwa na Pascal Msindo, dakika ya 53 Abdul Suleiman ‘Sopu’ alifunga bao la sita, akipokea pasi ya Fei Toto, Sopu alifunga bao lingine dakika ya 55 likiwa la saba kwa Azam pasi ya Fei Toto.

AZA 03

Vaibu la mashabiki lilikuwa juu, huku wengine wakionekana na bango lililokuwa linamhusu kocha wa timu hiyo lilioandikwa ‘In Ibenge We Trust’ kwa Kiswahili wakimaanisha kumwamini kocha huyo. Bango lingine liliandikwa ‘Welcome Ibenge, tunataka ubingwa na makundi. Asante Ibenge.’

Azam ikiwa imetangulia kuingia makundi michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika, zinasubiriwa Yanga inayocheza kesho Jumapili dhidi yaSilver Strikers na Simba dhidi ya Nsingizini Hotspurs, keshokutwa Jumapili, hizo zitachezwa Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar katika Ligi ya Mabingwa Afrika, wakati Singida Black Stars dhidi Flambeau du Centre, mchezo huo utapigwa kesho Jumamosi Uwanja wa Azam Complex ikiwa ni Kombe la Shirikisho Afrika.

AZA 04

Azam imefuzu makundi ya michuano ya CAF kwa mara ya kwanza katika historia ya klabu hiyo iliyoanzishwa mwaka 2004 baada ya kujaribu kwa misimu 10 bila mafanikio.

Kikosi cha Azam: Zuberi Foba, Lusajo Mwaikenda, Pascal Msindo, Yoro Diaby, Zouzou Landry, Yahya Zayd, Abdul Suleiman ‘Sopu’, Himid Mao, Jephte Kitambala, Feisal Salum ‘Fei Toto’ na Iddy Nado.

Kikosi cha KMKM: Adam Rihaji, Ahmed Isahaka, Arafat Farid, Mohamed Ali, Firdaus Seif, Imran Mohamed, Nasir Sheha, Jasper Yaw, Mzee Hassan, Ali Hassan na Haji Makame.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *