
BAADA kutoka suluhu dhidi ya Dodoma Jiji, Kocha mkuu wa Mtibwa, Awadh Juma amesema wakati wanajipanga kwenda kukutana na Yanga, anataka kuhakikisha muda uliosalia wanatafuta suluhusho la kupata mabao.
Mtibwa inashika nafasi ya sita kwenye msimamo wa ligi, ikiwa na pointi tano baada ya kucheza michezo minne hadi sasa.
Akizungumza na Mwanaspoti, Awadh amesema licha ya kutoruhusu bao dhidi ya Dodoma Jiji, lakini matokeo hayo kwa sasa hayapo tena kwenye vichwa vya wachezaji wake.
Amesema pointi moja ilizoziokota zimeshapita na sasa nguvu kubwa wanaiwekeza kwenye mechi ijayo ambayo kwa upande wao haitakuwa rahisi.
“Kucheza na Yanga haitakuwa rahisi, lakini nataka kuwasoma Mabingwa hao kwenye mapungufu yao kwenye mchezo dhidi ya Silver Strikers.
“Mchezo uliopita dhidi ya Dodoma tulitawala vizuri, lakini tukashindwa kutumia nafasi, huo ndiyo udhaifu wa timu yangu kwa sasa na kabla ya kwenda Dar es Salaam tutajipanga kutafuta suluhusho.
Aliongeza; “Kikosi changu kimerudi Morogoro kupata baraka za nyumbani kikitokea Dodoma, ambako ndiko uwanja wetu wa nyumbani, tutatokea hapo kuja kuwafuata Yanga, naamini mchezo huo utakuwa mgumu.”
Mtibwa itaikaribishwa na Yanga, Jumatano Oktoba 29, saa 1:00 jioni katika Uwanja wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam.