‎‎Dar es Salaam. Tundu Lissu, mshtakiwa wa kesi ya uhaini na Jamhuri, kila upande umeutambia mwingine kuhusu hatima ya shauri hilo baada ya Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam kukataa kupokea vielelezo vya upande wa mashtaka.

Vielelezo vilivyokataliwa ni flash disk na memory card (vifaa vya kielektroniki vya kuhifadhi kumbukumbu) zilizokuwa na picha mjongeo (video) ya Lissu akitoa hotuba inayodaiwa kuwa na maudhui ya uhaini na ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa video hiyo.

Lissu jana Alhamisi Oktoba 23 na leo Ijumaa Oktoba 24, 2025, ametamka hakuna kesi tena akidai baada ya vielelezo hivyo kukataliwa hakuna ushahidi mwingine wa Jamhuri wa kuthibitisha shtaka linalomkabili.

Jamhuri kwa upande wake imemjibu yeye si mwendesha mashtaka mpaka ajue baada ya vielelezo hivyo kukataliwa kuna ushahidi gani, wala si mahakama mpaka aseme kuwa kesi imeisha.

Katika kesi hiyo Lissu, ambaye ni Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) anakabiliwa na shtaka la uhaini akidaiwa kutoa maneno ya kuitishia Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kinyume cha kifungu cha 39(2) (d) cha Sheria ya Kanuni ya Adhabu.

Anadaiwa Aprili 3, 2025, jijini Dar es Salaam, akiwa raia wa Tanzania mwenye utii kwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alitoa maneno ya kuitishia Serikali na kuonyesha nia hiyo kwa kuchapisha meneno hayo katika mitandao ya kijamii kuwa:

“Wakisema msimamo huu unaashiria uasi, ni kweli…, kwa sababu tunasema tutazuia uchaguzi, tutahamasisha uasi, hivyo ndivyo namna ya kupata mabadiliko…, kwa hiyo tunaenda kukinukisha…, sana sana huu uchaguzi tutaenda kuuvuruga kwelikweli…, tunaenda kukinukisha vibaya sana…”

Kesi hiyo inayosikilizwa na Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, mbele ya jopo la majaji watatu linaongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Masjala Ndogo Iringa, Dunstan Ndunguru. Majaji wengine ni James Karayemaha na Ferdinand Kiwonde.

Jana Oktoba 23, shahidi wa tatu wa Jamhuri, Mkaguzi wa Jeshi Polisi, Samweli Kaaya (39), mtaalamu wa picha, Kitengo cha Picha Kamisheni ya Uchunguzi wa Sayansi Jinai, Makao Makuu ya Jeshi la Polisi, Dar es Salaam, alihitimisha ushahidi wake.

Katika ushahidi wake wa msingi alieleza Aprili 8, 2025 alipokea flashi na memory card zenye video hiyo ya Lissu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Upelelezi Kanda Maalumu, Dar es Salaam ili kuchunguza uhalisia wake.

Aliieleza mahakama katika uchunguzi alibaini video hiyo ni halisi na haina pandikizi, kisha akaandaa ripoti ya uchunguzi huo.

Oktoba 17, 2025 aliiomba mahakama ipokee vifaa hivyo vya kielektroniki lakini Lissu alipinga. Mahakama katika uamuzi wa Jumatano Oktoba 22, 2025 ilikubali pingamizi ikakataa visitolewe kama kielelezo.

Baada ya uamuzi huo, Jamhuri iliomba ripoti ya uchunguzi wa uhalisia wa video hiyo ipokewe kuwa kielelezo cha ushahidi wake.

Lissu alipinga. Mahakama katika uamuzi wa Oktoba 23, mahakama ilikubali pingamizi hilo, ikakataa kupokea ripoti hiyo kama kielelezo.

Baada ya mapumziko akiwa kizimbani kabla ya majaji kuingia kwenye ukumbi wa mahakama, Lissu alisema: “Kuanzia sasa, kuanzia sasa, nakaa gerezani kwa sababu ya uchaguzi tu. Kesi kwisha.”

Alieleza hayo mbele ya wafuasi na wanachama wa Chadema na wasikilizaji wengine wa shauri hilo.

Baada ya majaji kuingia na shahidi kuhitimisha ushahidi wake, kiongozi wa jopo la waendesha mashtaka, Wakili wa Serikali Mkuu, Lenatus Mkude, aliiomba mahakama iahirishe kesi hiyo mpaka leo Oktoba 24, akiiarifu kuwa wanaendelea kutafakari kuhusu uamuzi dhidi ya vielelezo vilivyokataliwa.

Lissu alisema hana pingamizi na ombi la Jamhuri kuahirisha kesi, lakini katika tafakari yake pia itafakari kama baada ya uamuzi wa mahakama kuna sababu ya kuendelea na kesi hiyo.

“Sina pingamizi kuhusu kesi kuahirishwa mpake kesho (leo), lakini nina jambo moja dogo tu. Jamhuri katika tafakari yake hiyo itafakari kama bado kuna sababu ya kuendelea na kesi hii,” alisema.

Wakili Mkude, leo Oktoba 24, ameieleza mahakama mashahidi wao waliokuwa wanafuata wanahusiana na vielelezo vilivyokataliwa na kutokana na uamuzi huo wa kuvikataa hawatawatumia tena mashahidi hao, kwa sababu hiyo leo hawana shahidi.

Amesema kwa kuwa leo Oktoba 24 ndiyo siku ya mwisho ya kikao cha usikilizwaji kesi hiyo na hawana shahidi, ameiomba mahakama iahirishe kesi hiyo mpaka Novemba 3, 2025.

Lissu amepinga ombi hilo, akidai sababu iliyotolewa si ya msingi.

Amesema kesi hiyo inategemea vielelezo vilivyokataliwa na kwamba, mashahidi raia ushahidi wao unategemea waliyoyaona mitandaoni, isipokuwa watatu tu, ofisa Uhamiaji, mwanajeshi na Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, ambao amehoji watathibitisha nini.

“Kwa hiyo ombi hili ni la kurefusha shauri hili ili niendelee kukaa gerezani uchaguzi upite na hiyo ni imani yangu na ni msimamo wangu hakuna kingine chochote wanachoweza kuthibitisha,” amesema na kuongeza:

“Kwa maoni yangu baada ya uamuzi wa jana (Oktoba 23) hakuna kesi tena hapa. Kwa hiyo, wahesimiwa kama mtaona ni sawasawa kuahirisha shauri hili naombeni nipate dhamana ya Mahakama Kuu kwa mujibu wa kifungu cha 302(2) ili nisiendelee kuteswa bure.”

Amesema mpaka leo (Oktoba 24) ni siku ya 202 akiwa gerezani.

“Kwa hiyo rai yangu ombi la kuahirishwa likataliwe, Jamhuri walete shahidi tuendelee kama likikubaliwa nipewe dhamana ili nisiendelee kukaa gerezani, mimi siwezi kukimbia kwa sabu sina makosa,” amesema.

Akijibu hoja hizo, wakili Mkude amesema wameeleza sababu za ahirisho chini ya kifungu cha 302, akieleza kwa mujibu wa Ibara ya 59 (B) ya Katiba ufunguaji mashtaka unafinyika kwa mujibu wa sheria na Katiba.

Amesema suala la uchaguzi halina uhusiano wowote, maana unafanyika kwa mujibu wa Katiba na sheria na mashauri yanaendelea mahamani kwa mujibu wa sheria.

“Jambo la tatu upande wa mashtaka ndio umefungua kesi na ndio unajua una ushahidi gani na mashahidi wangapi na hatujafunga ushahidi. Kwa hiyo, kusema kuwa mpaka hapa tulipofikia hakuna ushahidi wowote kuthibitisha, hilo tunalifahamu upande wa mashtaka,” amesema na kuongeza:

“Mshtakiwa kusema kukataliwa vielelezo hakuna ushahidi mwingine ni kuingilia majukumu ya upande wa mashtaka.”

Amesema upande wa mashtaka wana mashahidi 30 na ndio kwanza wana shahidi wa tatu, lakini wameomba ahirisho kwa sababu za msingi walizozitaja.

Amesema watakapofunga ushahidi wao ndipo mahakama itaamua kama mshtakiwa ana kesi ya kujibu au la.

Kuhusu dhamana, amesema shtaka linalomkabili halina dhamana.

Wakili wa Serikali Mkuu, Nassoro Katuga, amesema hoja ya mahakama kuilazimisha Jamhuri kuendelea na ushahidi haikupaswa kutolewa na mwombaji mwenye uelewa wa sheria kwa sababu wamesema hawana shahidi na wameeleza sababu za msingi.

“Kusema vielelezo kukataliwa hakuna ushahidi tena ni kama mashahidi wote wamekataliwa. Maoni yake kwamba hakuna kesi tena inaonekana mshtakiwa katoka kuwa mshtakiwa kaenda kuwa mahakama, kuamua kuwa basi kwa kuwa vielelezo vimekataliwa hakuna kesi,” amesema.

Amesema mshtakiwa ametoa hoja hiyo kwa lengo la kupotosha na kuomba huruma kwa umma.

“Kwa hiyo vielelezo kukataliwa ina maana hata ushahidi wa kuona haupo?” amehoji.

Kuhusu dhamana amesema ombi hilo halitekelezeki kwa kuwa kifungu cha 151(5)(a)(I) shtaka lake halina dhamana. 

“Mshtakiwa kuomba dhamana mahakama hii ni kuiomba mahakama ivunje sheria, kwa hiyo ombi hili haliwezi kukubaliwa kwani linakiuka sheria,” amesema.

Uamuzi wa mahakama

Akitoa uamuzi, Jaji Ndunguru amesema suala la kuahirishwa kwa shauri pale panapokuwa hakuna shahidi lipo kwa mujibu wa taratibu isipokuwa pale kunapokuwa na uzembe wa Jamhuri.

“Hakuna siku tumekosa shahidi kwa upande wa mashtaka kutoleta shahidi,” amesema.

Kuhusu ombi la dhamana amesama kifungu cha sheria alichokitaja mshtakiwa kinatoa mazingira ya dhamana kunapokuwa na ahirisho kama hilo, lakini amesema kosa linalomkabili halina dhamana.

“Kwa hiyo tunashindwa kusema kwamba tunampa dhamana. Kwa kuwa leo ndio mwisho wa session (kikao) hii, shauri hili linaahirishwa mpaka Novemba 3, 2025 kama cause list (ratiba ya mahakama ya usikilizwaji kesi hiyo) inavyoonyesha,” amesema.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *