
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam, imekataa maombi ya kusimamishwa shauri la kudharau amri ya mahakama linalowakabili viongozi wa Chadema, wakiwamo Makamu Mwenyekiti (Bara), John Heche na Katibu Mkuu, John Mnyika.
Shauri hilo la madai mchanganyiko namba 25480 la mwaka 2025 linatokana na kesi ya kikatiba inayokikabili Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kuhusu mgogoro wa mgawanyo wa rasilimali za chama baina ya Tanzania Bara na Zanzibar inayosikilizwa mahakamani hapo.
Kesi hiyo ya madai namba 8323 ya mwaka 2025 imefunguliwa na Said Issa Mohamed, ambaye ni Makamu Mwenyekiti mstaafu wa Chadema (Zanzibar) na wajumbe wa Bodi ya Wadhamini wa chama hicho kutoka Zanzibar, Ahmed Rashid Khamis na Maulida Anna Komu.
Walalamikiwa katika kesi hiyo inayosikilizwa na Jaji Hamidu Mwanga ni Bodi ya Wadhamini wa Chadema na Katibu Mkuu wa chama hicho.
Mbali ya kesi hiyo, walalamikaji wamefungua shauri la madai dhidi ya Heche, Mnyika na wenzao wakiwataka wajieleze ni kwa nini wasifungwe kama wafungwa wa madai kwa kudharau amri ya mahakama.
Wajibu maombi wengine ni Mayemba, Brenda Rupia, Hilda Newton, Twaha Mwaipaya, Gervas Lyenda na Bodi ya Wadhamini wa Chadema.
Wanadaiwa kuidharau mahakama kwa kukiuka amri ya zuio iliyotolewa Juni 10, 2025 dhidi ya wadaiwa katika kesi ya msingi, inayowazuia kufanya shughuli za kisiasa na kutumia mali cha chama mpaka kesi hiyo itakaposikilizwa na uamuzi kutolewa.
Jumatano Oktoba 22, 2025 mawakili wa wajibu maombi Mpale Mpoki na Hekima Mwasipu waliieleza mahakama kuwa wamefungua shauri la maombi ya Mapitio Mahakama ya Rufani dhidi ya mwenendo wa shauri hilo wa Oktoba 15, 2025.
Hivyo, waliiomba mahakama kusimamisha mwenendo wa shauri hilo kusubiri uamuzi wa lile la mapitio.
Mahakama katika uamuzi uliotolewa leo Oktoba 24 na Jaji Awamu Mbagwa, anayesikiliza shauri hilo imeyakataa maombi hayo ikisema hayana mashiko kwa kuwa amri wanazoombea mapitio hazistahili kisheria kuombewa mapitio.
Jaji Mbagwa ameamuru wajibu maombi wa kwanza (Heche) na wa tatu mpaka wa saba wawasilishe mahakamani viapo vyao kinzani Jumatatu Oktoba 27, 2025. Ameamuru shauri hilo lisikilizwe pingamizi na shauri la msingi Oktoba 28, 2025.
Katika pingamizi hilo, wajibu maombi wanadai kuna mgongano wa masilahi wa wakili wa waombaji wakidai ndiye aliyeshughulikia upatikanaji wa ushahidi wa kielektroniki unaodaiwa wa wajibu maombi kukiuka amri ya mahakama.
Sababu ya pili wanadai shauri hilo limefunguliwa nje ya ukomo wa muda wa kisheria wa siku 60 na tatu wanadai amri ya mahakama inayodaiwa kukiukwa inawahusu wadaiwa kwenye kesi ya msingi pekee.
Oktoba 22, mahakama pia ilielekeza wajibu maombi Heche na wenzake wengine kuanzia mjibu maombi wa tatu mpaka wa saba watangazwe gazetini kama wito mbadala kutokana na maombi ya mawakili wa waombaji.
Wakili wa waombaji, Shabani Marijani, aliieleza mahakama kuwa wameshindwa kuwafikishia wito wa kuhudhuria mahakamani kwa njia ya kawaida kwa kuwa wanakwepa kupokea hati hiyo.
Wakili Jebra Kambole, amefika mahakamani leo Oktoba 24, akajitambulisha kuwa anawawakilisha wajibu maombi hao waliotangazwa gazetini. Ameieleza mahakama amesoma tangazo kwenye Gazeti la Mwananchi la Alhamisi Oktoba 23, 2025.
Ameomba muda wa siku 14 aweze kuwasainisha wito huo, lakini wakili Marijani alipinga kuwa siku 14 ni nyingi kwa kuzingatia shauri hilo limefunguliwa kwa hati ya dharura, akapendekeza wapewe angalau siku saba.
Kambole alieleza wateja wake hawako sehemu moja bali mikoa tofauti, huku akieleza Heche anashikiliwa na vyombo vya dola.
Jaji Mbagwa amewaamuru wawasilishe viapo kinzani vyao Jumatatu, Oktoba 27, 2025.
Chanzo cha shauri hilo
Awali, waombaji na walalamikaji katika kesi ya msingi walifungua shauri dogo la maombi ya zuio la muda dhidi ya wadaiwa, wakiiomba mahakama itoe amri kuwazuia kufanya shughuli zozote za kisiasa na kutumia mali za chama mpaka kesi ya msingi itakapoamuliwa.
Juni 10, 2025 mahakama katika uamuzi ilikubali hoja za walalamikaji ikatoa amri hizo za zuio kama zilivyoombwa.
Waombaji wanadai wajibu maombi wamekuwa wakikiiuka amri hiyo, huku katika kiapo chao wakitaja tarehe za matukio wanayodai wakijibu maombi wamekuwa wakifanya shughuli za kisiasa walizozuiwa.