
Dar es Salaam. Mahakama Kuu Masjala Ndogo Dar es Salaam imetupilia mbali shauri la maombi ya amri ya kumfikisha mahakamani au kumwachia kwa dhamana (Habeas corpus), Humphrey Polepole, ikieleza hakuna ushahidi kuwa wajibu maombi ndio waliomchukua.
Uamuzi huo ulioandikwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Salma Maghimbi, aliyesikiliza shauri hilo umesomwa leo Oktoba 24, 2025 na Naibu Msajili wa mahakama hiyo, Livin Lyakinana.
Hata hivyo, Peter Kibatala, wakili wa Polepole, aliyewahi kuwa Balozi wa Tanzania nchini Cuba, amesema wanakwenda Mahakama ya Rufani kupinga uamuzi huo kwa kuwa wanaamini kuna hoja za msingi ambazo mahakama hiyo inapaswa kuziangalia.
Shauri hilo la maombi namba 24514/2025 lilifunguliwa mahakamani hapo Oktoba 7, 2025 na Kibatala kwa niaba ya Polepole, chini ya hati ya dharura.
Wajibu maombi katika shauri hilo kwa mpangilio ni Mkuu wa Jeshi la Polisi (IGP), Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP), Mwanasheria Mkuu wa Serikali (AG), Mkuu wa Upelelezi wa Kanda Maalumu Dar es Salaam (ZCO) na Kamanda wa Polisi wa kanda hiyo (ZPC).
Katika hati ya maombi ya dharura iliyothibitishwa na Kibatala anaeleza Polepole aliripotiwa kutekwa na watu wanaodhaniwa kuwa ni maofisa wa Jeshi la Polisi waliovamia nyumbani kwake Ununio, wilayani Kinondoni, Dar es Salaam, Oktoba 6, 2025,
Alidai mpaka sasa hajashtakiwa kwa kosa lolote la jinai katika mahakama yoyote ya kisheria na inaaminika amewekwa kizuizini mahali kusikojulikana na wajibu maombi.
”Hivyo haki zake za kikatiba zimekiukwa bila sababu za msingi. Ustawi wa mwombaji unahitaji uangalizi na uingiliaji wa haraka, ikiwemo kujua hali ya maisha yake,” alisema Kibatala katika hati hiyo.
Aliiomba mahakama iwaelekeze wajibu maombi wamuachie huru mwombaji (Polepole) kwa dhamana au wamfikishe katika mahakama ya kisheria na kumshtaki kwa mujibu wa sheria.
Katika kiapo kilichounga mkono maombi hayo, Kibatala alieleza mwombaji ni raia wa Tanzania ambaye ameitumikia nchi yake katika nafasi mbalimbali za Mkuu wa Wilaya ya Ubungo, Dar es Salaam na Balozi wa Tanzania nchini Malawi na Cuba.
Alieleza katikati ya mwaka huu, kwa hiari alijiuzulu wadhifa wa ubalozi, huku akieleza sababu mbalimbali zikiwamo kutokuridhika na namna mambo yanavyoendeshwa ndani ya Serikali na nchini Tanzania.
Kibatala alieleza katika taarifa zake ambazo amekuwa akizitoa mara kwa mara, Polepole amekuwa akilalamika kuwa usalama wake uko hatarini kutokana na vitisho ambavyo amekuwa akipokea kutoka kwa watu wasiojulikana kutokana na msimamo wake katika masuala mbalimbali.
“Haya yamethibitishwa kwa umma na kaka wa mwombaji, Godfrey na Agustino Polepole, kama ilivyothibitishwa katika taarifa za vyombo vya habari vya ndani,” alisema Kibatala katika kiapo.
Alieleza mjibu maombi wa tano (ZPC – Jumanne Muliro) amenukuliwa katika taarifa za vyombo vya habari akitoa taarifa za kupuuza tuhuma hizo nzito za utekwaji wake.
Alisisitiza mpaka wakati anaapa kiapo hicho, Polepole hajulikani alipo na hakuna hata mmoja kati ya wajibu maombi ambaye ametoa mrejesho wowote kuhusu alipo, hali yake ya ustawi na hadhi yake ya kisheria jambo linaloongeza kiwango cha wasiwasi nchini.
“Nina sababu za kuamini kwamba wajibu maombi na hasa mjibu maombi wa tano ZPC ana ufahamu na yuko na mamlaka ya kumshikilia mwombaji,” alisema.
Uamuzi wa mahakama
Shauri hilo lilisikilizwa kwa njia ya maandishi. Mahakama katika uamuzi uliotolewa leo Oktoba 24, imesema mwombaji alishindwa kutekeleza jukumu lake la kuithibitishia mahakama kuwa wajibu maombi hao ndio waliomchukua.
Badala yake imesema kilichowasilishwa mahakamani ni hisia tu kuwa wajibu maombi ndio waliomchukua au wanajua aliko.
“Hivyo, mahakama hii inajizuia kutoa amri zilizoombwa. Kwa sababu hizo shauri hili linakataliwa,” amesema Naibu Msajili Lyakinana.
Akizungumzia uamuzi huo, Kibatala amesema wanakwenda kuukatia rufaa Mahakama ya Rufani na kwamba tayari wameshachua hatua hizo.
“Tayari tumeshawasilisha notisi ya kusudio la kukata rufaa na tumeshaiandikia Mahakama Kuu barua ya kuomba kumbukumbu za rufaa (nyaraka zinazohusiana na shauri hilo) na tayari ziko kwenye mfumo wa mahakama,” amesema.