KOCHA Mkuu wa Coastal Union, Mohammed Muya ametoa siku saba za mapumziko kwa wachezaji wake kwa lengo la kwenda kupiga kura, pia kutoa nafasi kwa wachezaji kusalimia familia zao kabla ya kuvaana na Yanga Desemba 10 mwaka huu.

Muya alijiunga na timu hiyo akichukua mikoba ya Ali Muhammed Ameir, ameiongoza katika mbili akiambulia pointi mbili, kwa sare dhidi ya Mtibwa Sugar ugenini na dhidi ya Fountain Gate nyumbani.

Akizungumza na Mwanaspoti, Muya amesema baada ya mechi hizo, amebaini mapungufu kwenye maeneo machache na anatarajia kuyafanyia kazi siku chache baada ya kurejea kutoka mapumziko.

“Nimeiongoza timu kwenye mechi mbili nikiwa na siku chache baada ya kukabidhiwa. Kupata pointi mbili siyo mbaya sana japo hayakuwa matarajio yetu. Ugenini kupata sare ni afya kwetu lakini nyumbani hatukutarajia hili. Nimeona mapungufu kwenye baadhi ya maeneo, nafikiri tutakaporejea tutakuwa kwenye nafasi nzuri ya kuyafanyia kazi,” amesema na kuongeza;

COA 01

“Safu ya ulinzi, kiungo hakuna makosa mengi eneo la ushambuliaji nimeshindwa kufanya tathimini kwa sababu kuna wachezaji sikuwa nao walikuwa na ruhusa maalum nafikiri tutakaporudi baada ya mapumziko tutajua wapi tunaanzia kabla ya kuvaana na Yanga.”

Muya amesema mara baada ya kurudi benchi la ufundi watakuwa na wakati mzuri wa kuiweka sawa timu yao ili iweze kuwa katika nafasi nzuri kutoa ushindani kwa timu pinzani huku akiitaja Yanga ambayo ndio wanatarajia kuanza nayo.

COA 02

Muya ameikuta Coastal Union ikiwa nafasi ya 13 katika msimamo wa ligi, ikiwa imecheza mechi tatu, imefungwa mchezo mmoja, ushindi mmoja na sare mmoja timu ikiwa chini yake imekusanya pointi mbili baada ya sare mbili.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *