Chanzo cha picha, URT
-
- Author, Laillah Mohammed
- Nafasi, BBC News Swahili
Nilipofika kwenye mgahawa wa TAMUTAMU uliopo katikati ya mji wa Nairobi Kenya mapema asubuhi, nilikutana na mmiliki wa Mgahawa huo Sam Nkya akiwa katika pilikapilika za maandalizi ya chakula cha mchana.
“Jamani tufanye chap chap (harakaharaka) wateja wa lunch (chakula cha mchana) huja mapema Alhamisi”, Nkya aliwaeleza wafanyakazi wake katika mgahawa huu unaoandaa vyakula vya asili vinavyoliwa uswahili na asili ya pwani ya Afrika Mashariki.
”Nilipenda tu mapishi ya vyakula hivi vya Kiswahili. Mama aliopenda sana kutuandalia mapochopocho tukiwa watoto na nikatamani sana kuwa mpishi maarufu na kuamua kufanya biashara hii, kitu ambacho nakipenda sana,” alisema Sam.
Japo angeendeleza ndoto yake nyumbani Dar es Salaam, Tanzania anawaandalia wateja wake katika migahawa kadhaa jijini Nairobi ambapo amepaita nyumbani kwa zaidi ya miaka mitano sasa.
Kwa pamoja na mke wake, wanakuza familia yao changa na kujitafutia Riziki ya kila siku mbali na nyumbani kwao Sam ambaye anasema siku moja angependa kurejea na kupanua biashara yake huko na labda kuwapa Watoto wao nafasi ya kuijuwa Tanzania kama anavyoifahamu yeye.
”Hilo litafaa sana ikiwa wanangu wangeweza kufurahia uraia pacha. Nimetamani sana jambo hilo kwa muda sasa. Lakini kwa sasa hilo haliwezekani kwa sababu Tanzania haikubalii raia wake kuwa na uraia pacha,” alisema Nkya.
Katiba ya sasa ya Tanzania haiwaruhusu raia wa nchi hiyo kuwa na uraia pacha. Sheria hiyo iliyopitishwa mwaka 1965 inasema Mtanzania mwenye uraia wa nchi nyingine anapotimiza umri wa miaka 18 anapoteza uraia wake wa Tanzania moja kwa moja.
Serikali ya Tanzania imekuwa ikitetea msimamo wake kuhusu sheria hii kwa kusema kwamba huenda ikaleta sintofahamu, kukosa kuwepo kwa uwazi na kutishia utambulisho wa kitaifa na uhuru wa kitaifa.
Lakini mchambuzi Philemon Mbughuni Muhando ambaye ni raia wa Tanzania anayeishi na kufanya kazi Marekani anasema kwamba hilo ni wazo linalotakiwa kuangaziwa upya kwa kuwa dunia ipo katika nyakati tofauti na zamani na watu wanasafri na kuishi popote duniani ambapo wanaweza kupata kipato chao cha kila siku.
”Nchi nyingi za kiafrika kama vile Kenya na Afrika Kusini wamewezesha utaratibu huo, lakini vile vile katika jambo la kiuchumi, ni kwamba inatoa mianya na kufungua milango zaidi kwa jamii ya diaspora kushiriki katika uzalishaji wa uchumi. Kumekuwa na hoja kwamba nchi nyingi za kiafrika zinapoteza utaalamu unaotoka Afrika kwenda kwenye nchi zingine. Hili ni jambo la kufungua nafasi zaidi ya watanzania wanaoishi nje ya nchi ‘Diaspora’ na itasaidia kuleta na kurudisha utaalamu pamoja na rasilimali kwa njia ya uwekezaji,”alisema Muhando katika mahojiano na BBC.
Aidha Muhando anhisi kwamba suala la uraia pacha linaambatana kwa karibu na uwezo wa raia wa Tanzania wanaoishi nje ya nchi kushiriki katika uchaguzi mkuu na kupata fursa angalau ya kumchagua Rais wa nchi hiyo.
Suzzana Mule ni mwandishi kutoka Tanzania ambaye kwa sasa anaishi nchini Kenya anapofanya kazi na akiishi na família yake. Anasema kwamba kitambulisho cha kupiga kura anacho na angetamani kabisa kutekeleza wajibu wake wa kikatiba akiwa Kenya kwa sababu majukumu ya kikazi huenda yasimruhusu kusafiri hadi nyumbani Tanzania.
”Nilipokuwa mwandishi nchini Tanzania sikupata nafasi ya kupiga kura kwa sababu mara nyingi nilikuwa kazini wakati wa uchaguzi na kwa sasa ninafanya kazi ambayo inaweza kunipa fursa ya kupiga kura. Ingewezekana kuwa fursa ya kupiga kura kwenye ubalozi wa Tanzania hapa Nairobi na kurejea kazini mara moja. Kwa sababu watoto wangu ni wadogo na sina nafasi ya kusafiri kwa sasa,” alisema Suzzana.
Mule ameishi nchini Kenya kwa miaka minane sasa, baada ya kufunga ndoa na mpenzi wake waliyekutana kazini jijini Nairobi Suzzana alipokuwa amekuja Kenya kupata mafunzo ya kikazi.
“Suala la Diaspora kupiga kura limeunganishwa moja kwa moja na suala la kupata katiba mpya. Na kama tunavyojua kwamba rasimu tayari alishaiandaa Jaji Warioba na imefika miaka takriban kumi sasa kama sijakosea lakini mpaka sasa bado hilo halijatekelezwan,” anasema Muhando.
Chanzo cha picha, URT
Kwa hilo bado ni jambo ambalo halina uhakika kwa sababu mpaka hivi sasa, tanzania inatumia katiba ya zamani pamoja na kwamba kumekuwa na ahadi nyingi na kupitisha rasimu ya katiba mpya , mpaka hivi sasa bado hakuna dalili kwa maana ya kwamba uhakika kwamba itatekelezwa lini! Pengine labda ni jambo ambalo tunasema tusubiri baada ya huu mchakato wa uchaguzi na awamu nyingine kuingia kama litatekelezwa ama la,’alisema mchambuzi Mbughuni Muhando.
Mnamo 2021 mbunge maalum Adha Abdul Juma wa chama tawala cha CCM aliomba serikali kuwaruhusu raia wa Tanzania kupiga kura katika balozi mbali mbali za Tanzania kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu unaofanyika Octoba 29, kama juhudi za taifa hilo kuimarisha misingi yake ya Kidemokrasia.
Alipotoa jibu lake Bungeni, waziri Mkuu Kassim Majaliwa alikiri kwamba kuwakubalia watanzania kupiga kura popote walipo duniani ni jambo ambalo limetajwa na serikali kama sera ya kitaifa inayopaswa kuwepo kwa mkakati madhubuti wa serikali.
‘Ningetaka sana kupata nafasi ya kupiga kura kwenye ubalozi wetu wa Tanzania hapa Kenya, manake nina majukumu Mengi yanayonizuia kusafiri hadi nyumbani kutekeleza wajibu ambao nauhisi ni muhimu kwangu,’ alisema Sam Nkya.
Baada ya kuasisiwa kwa katiba mpya mnamo agosti 27 2010, wakenya wamefurahia uhuru wa kushiriki kwenye uchaguzi mkuu mara tatu ambapo serikali imekuwa ikipanua mataifa zaidi ambayo raia wa Kenya wanaweza kupiga kura kwenye ofisi za ubalozi.
Kuna cha kujifunza Kenya?
Mnamo 2013 raia wa Kenya waliokuwa wakiishi katika mataifa matatu ya Afrika Mashariki ya Tanzania, Uganda na Rwanda na Afrika Kusini.
Waliporejea kufanya uchaguzi wa 2017 idadi ya mataifa yaliyoweza kushiriki iliongezeka kwa mataifa ya Afrika Magharibi na Marekani na Uingereza.
Waliposhiriki uchaguzi wa 2022 wakenya wanaoishi Los Angeles na miji mingine kwenye majimbo yaliyopo magharibi mwa Marekani walipata fursa ya kushirki uchaguzi kw akupiga kura kwa ofisi ndogo ya ubalozi wa Kenya iliyopo jimbo la Carlifornia.
Kufuatia hatua hii iliyopigwa na Kenya , raia wa Tanzania wameonyesha hamu kubwa ya kujumuishwa kwenye uenzi wa taifa lao ambalo wanasema wanachangia pakubwa.
Katika miesi sita ya mwisho wa mwaka wa 2024 watanzania wanaoishi nje ya nchi walituma nyumbani takriban dola milioni 810 za kimarekani ambazo zimechagia pakubwa akatiak ukuaji wa uchumi w anchi hiyo.
”Sio tu kutua hela nyumbani, tuna matamanio ya hata kuwekeza kule na kujifaa sisi na pia nchi yetu,” alisema Nkya.
Mbali na masuala ya uwekezaji na utekelezaji wa haki zao za kikatiba wengi kama Suzzan Mule wanahisi kwamba kuwepo kwa uraia pacha kutawapunguzia changamoto za usafiri kati ya nchi zao za makao na Tanzania.
Kulingana na takwimu za serikali ya Tanzania, takriban Watanzania milioni 1.5 walikuwa wanaishi nje ya nchi barani Afrika na ughaibuni – mwishoni mwa 2024. Na inaelezwa kwamba idadi hii huenda ikawa kubwa zaidi kwa sababu walioripotiwa kuishi nje ni wale waliojisajili rasmi kupitia ubalozi wa Tanzania wanapoishi au katika nchi ambazo zina ofisi za ubalozi wa Tanzania karibu na walipo.
Kati yao kuna wale wenye vyeti vya ukazi wa kudumu na wengine ambao wameukana uraia wa Tanzania na kuchukuwa uraia wa mataifa ambapo wanaishi.
Mchambuzi Philemon Mbughuni anasema: “Nadhani watu wengi pia wangependa kuona kwamba kama taifa pasipo kujali kwamba watu wako wapi, ni jambo ambalo lina mgusa kila mtu kuona taasisi na mifumo ya kisiasa ikiwa ni mifumo ambayo inawajumuisha watu wote, na kupata serikali ambayo watu wameipigia kura na kujisikia kwamba ni sehemu ya mchakato wa kisiasa pamoja na kiuchumi. Na mwisho wa siku ni wote kujiskia kwmaba ni taifa moja.”
Katika hotuba yake kwa bunge la taifa mjini Dodoma, Rais Samia Suluhu Hassan aliahidi kufungua mchakato wa kuifanyia mabadiliko katiba ya Tanzania ambayo watanzania wengi kama Sama Nkya na Suzzane Mule wanategemea kwamba ndoto yao ya kujumuishwa kwenye ujenzi wa taifa ikiwemo siasa na maendeleo, hata wakiwa mbali itatimia siku moja.
Lakini kwa sasa wanasalia kusubiria serikali na bunge la kitaifa kubuni sera ambazo angalau zitawapa matumaini.