
Dar es Slaam. Wakati Yanga na Simba zikitarajia kucheza mechi zao za marudio za mtoano za Ligi ya Mabingwa Afrika kesho na keshokutwa, Jeshi la Polisi limesema litafanya ukaguzi kuhakikisha kuna usalama wa hali ya juu.
Katika mchezo wa kwanza uliopigwa nchini Malawi Yanga ilichapwa bao 1-0 na Silver Strikers hivyo kesho inatakiwa kupata ushindi mnono ili iweze kufuzu kwa hatua ya Makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Kwa upande wa mechi ya kwanza ya Simba ilichezwa Oktoba 19, 2025 ilishinda ugenini katika ardhini ya Eswatini mabao 3-0 dhidi ya Nsingizini Hotspurs kwenye Uwanja wa Somhololo Lobimba huku marudio ya mechi hiyo ikitarajiwa kuchezwa Oktoba 26, katika Uwanja wa Benjamini Mkapa, huku kikosi hicho chini ya kocha Dimitar Pantev kikiwa na nafasi kubwa ya kwenda makundi.
Akizungumza leo Oktoba 24, 2025, Kamanda wa Kanda Maalum ya Dar es Salaam, Jumanne Muliro amesema maandalizi ya kiusalama yamekamilika kwa kiwango cha juu ili kuhakikisha michezo hiyo inachezwa katika mazingira salama na yenye amani, huku mashabiki wakihimizwa kuzingatia maadili na kufuata maelekezo ya vyombo vya dola.
“Jeshi la Polisi limejipanga kuhakikisha michezo yote miwili inafanyika kwa amani. Mashabiki wote wa soka waingie uwanjani wakiwa salama na watoke wakiwa salama, bila kujali matokeo yatakuwaje,” amesema Kamanda Muliro.
Kamanda Muliro amesema Uwanja wa Benjamin Mkapa una uwezo wa kuchukua watazamaji 60,000, hivyo mashabiki wametakiwa kufika mapema ili kuepuka msongamano, huku wakitakiwa kuwa watulivu na kufuata maelekezo ya walinzi.
“Tumeimarisha ulinzi katika mageti yote, hakuna mtu atakayeruhusiwa kuingia na silaha ya aina yoyote, ikiwemo vitu vinavyoweza kuleta madhara au kuhatarisha usalama,” amesema.
Amefafanua kuwa upekuzi wa hali ya juu utafanyika kabla ya mashabiki kuingia uwanjani, na askari wenye mamlaka ya kisheria pekee ndio watakaoruhusiwa kuwa na vifaa vya kiusalama.
Pia, amesema barabara ya Duce itafungwa kwa muda wakati wa mchezo wa Yanga, huku barabara ya Mandela ikitumika kwa kuingia na kutoka kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa.
Kwa upande wa mchezo wa Simba, amesema barabara zinazozunguka Uwanja wa Uhuru pia zitakuwa chini ya uangalizi maalumu wa polisi, na wananchi wanatakiwa kufuata maelekezo ya maofisa wa usalama watakaokuwa eneo hilo.
Kamanda Muliro amewakumbusha mashabiki wote wa Yanga na Simba kuwa wastaarabu, kujiepusha na lugha za matusi au maneno ya uchochezi na kuheshimu utamaduni wa Tanzania wa upendo na burudani.
“Soka ni burudani watu wanakuja na wake zao, waume zao na watoto, hatutavumilia matusi, kejeli au vitendo vya uchochezi. Atakayekiuka tutamchukulia hatua papo hapo,” amesema Muliro.
Amesema pia matukio ya uvunjifu wa amani ndani au nje ya uwanja hayataruhusiwa, na kwamba Jeshi la Polisi halitasita kumchukulia hatua mtu yeyote atakayevunja sheria, bila kujali timu anayoishabikia.