
-
- Author, Ione Wells & Joshua Cheetham
- Nafasi, BBC
Kwa muda wa miezi miwili, jeshi la Marekani limekuwa likiunda kikosi cha meli za kivita, ndege za kivita, wanajeshi wa majini, ndege zisizo na rubani na ndege za kijasusi katika bahari ya Caribbean. Ni kikosi kikubwa zaidi kwa miongo kadhaa.
Ndege za kivita zimefanya Mashambulizi katika pwani ya Venezuela. Trump ameidhinisha kutumwa kwa majasusi wa Shirika la Kijasusi, CIA nchini Venezuela pia, huku hali ya wasiwasi ikiongezeka.
Marekani inasema imewauwa makumi ya watu katika mashambulizi dhidi ya boti ndogo kutoka Venezuela ambazo inadai zinabeba “mihadarati” na “magaidi wa mihadarati,” bila kutoa ushahidi au maelezo kuhusu waliokuwemo.
Mashambulizi hayo yamelaaniwa katika eneo hilo na wataalam wametilia shaka uhalali wake. Marekani inasema ni vita dhidi ya ulanguzi wa dawa za kulevya lakini dalili zote zinaonyesha kuwa hii ni kampeni ya vitisho inayotaka kumuondoa Rais wa Venezuela Nicolás Maduro madarakani.
“Hili linahusu mabadiliko ya serikali,” anasema Dk Christopher Sabatini, mtafiti wa masuala ya Amerika ya Kusini kutoka Chatham House.
Anasema lengo la kuwekwa kikosi cha jeshi ni “kuongeza hofu” miongoni mwa wanajeshi wa Venezuela na watu wa karibu wa Maduro ili wamsaliti.
BBC imefuatilia taarifa kuhusu meli na ndege za Marekani katika eneo hilo – pamoja na picha za satelaiti na picha kwenye mitandao ya kijamii – ili kujaribu kujenga picha ya mahali majeshi ya Trump yalipo.
Eneo kilipo kikosi hicho limekuwa likibadilika. Kufikia tarehe 23 Oktoba, tulitambua meli 10 za kijeshi za Marekani katika eneo hilo, zikiwemo zile za makombora na meli za mafuta za kujaza meli za kivita.
Yupo wa kumgeuka Maduro?
Sio siri kwamba utawala wa Marekani, hasa Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio, anataka kuona Maduro akipinduliwa.
Mapema mwaka huu, aliiambia Fox News, Maduro ni “dikteta wa kutisha” na alipoulizwa kama anataka Maduro aondoke, alisema: “Tutafanyia kazi sera hiyo.”
Hata kwa wakosoaji wa wazi wa Maduro kama Rubio, ni vigumu kutoa wito wa wazi wa mabadiliko ya utawala huo unaoungwa mkono na jeshi – jambo ambalo upinzani wa Venezuela umetamani litokee.
Donald Trump alifanya kampeni 2016, kwa ahadi ya “kuacha kupindua serikali za kigeni”, na hivi karibuni amelaani Marekani kujihusisha na “vita visivyokwisha.”
Marekani haimtambui Maduro kama rais wa Venezuela, baada ya uchaguzi uliopita wa 2024 kukosolewa na mataifa mengi na upinzani nchini Venezuela, kuwa haukuwa huru na wa haki. Ubalozi wa Marekani huko Caracas ulifungwa wakati wa muhula wa kwanza wa urais wa Trump mwaka 2019.
Marekani imeongeza donge nono kwa atakaye toa taarifa zitakazopelekea kukamatwa kwa Maduro hadi dola za kimarekani milioni 50, kama motisha kwa wale walio karibu naye ili wamtie ndani. Lakini hilo halijatokea.
Profesa wa sheria wa Venezuela na mtafiti katika taasisi ya fikra tunduizi juu ya masuala ya usalama ya CSIS, Jose Ignacio Hernández, anasema dola milioni 50 “ni pesa ndogo kwa watu wake wa karibu.”
Kuna pesa nyingi zinapatikana kupitia ufisadi katika nchi hiyo yenye utajiri wa mafuta. Mkuu wa zamani wa Hazina Alejandro Andrade, alitoa hongo ya dola bilioni 1 kabla ya kuhukumiwa.
Wachambuzi wengi wanakubali kwamba jeshi la Venezuela lingekuwa muhimu kwa mabadiliko yoyote ya serikali, lakini kwa wao kumgeuka Maduro na kumwondoa madarakani, wanataka pia ahadi za kinga dhidi ya kushtakiwa.
Hernández anaongeza: “Watafikiri, kwa namna fulani, wanajihusisha katika shughuli za uhalifu.”
Michael Albertus, profesa wa sayansi ya siasa katika Chuo Kikuu cha Chicago ambaye huandika sana kuhusu Amerika ya Kusini, hana hakika kwamba hata dola milioni 500 inaweza kuwashawishi watu wa karibu wa Maduro kumgeuka.
“Viongozi wanaotawala kimabavu siku zote huwa na mashaka na watu wao wa karibu, na kwa sababu hiyo, wanaunda mifumo ya kuwafuatilia na kuhakikisha uaminifu wao,” anasema.
Vikwazo vya kiuchumi kwa Venezuela vimezidisha mzozo mkubwa wa kiuchumi, lakini havijafaulu kuwashawishi viongozi wakuu kumpinga rais wao.
Ni kuhusu dawa za kuleyva pekee?
Chanzo cha picha, Reuters
Donald Trump ametangaza kuwa hivi ni vita dhidi ya walanguzi wa mihadarati na kusema boti moja ambayo Marekani iliishambulia, tarehe 16 Oktoba, ilikuwa “imejaa dawa za kulevya aina ya fentanyl.”
Lakini fentanyl inazalishwa nchini Mexico – sio Amerika Kusini – na inakuja Marekani kupitia mpaka wa kusini.
“Sio kuhusu dawa za kulevya,” anasema Dk Sabatini. “Anaona utawala wa Venezuela sio tu ni udikteta – ni utawala wa wahalifu.”
Tangu 2020, Idara ya Sheria ya Marekani imekuwa ikimshutumu Rais Maduro kwa kuongoza shirika la ulanguzi wa dawa za kulevya na ugaidi wa mihadarati, jambo ambalo anakanusha.
Trump amesema ameidhinisha CIA kufanya operesheni za siri nchini Venezuela dhidi ya “dawa za kulevya zinazoingia” kutoka Venezuela.
Venezuela haizalishi kiasi kikubwa cha kokeini – nchi kama Colombia, Peru na Bolivia ndio zinazalisha zaidi. Kuna baadhi ya kokeini inayouzwa kupitia Venezuela, ambayo serikali hiyo inasema inapambana nayo.
Ripoti ya Mamlaka ya Udhibiti wa Dawa za Kulevya Marekani ya mwaka 2025 inasema asilimia 84 ya kokeini iliyokamatwa Marekani inatoka Colombia na kutaja nchi nyingine lakini si Venezuela katika ripoti hiyo juu ya kokeini.
Marekani haijatoa ushahidi wa tuhuma kuwa Maduro anaongoza shirika la ulanguzi wa dawa za kulevya. Maduro amekanusha mara kwa mara tuhuma hizo, na kwa upande wake anaituhumu Marekani kwa ubeberu na kuzidisha mzozo wa kiuchumi wa nchi hiyo kupitia vikwazo.
Kuna kesi zinazojulikana za walio karibu naye kufunguliwa mashtaka.
Mwaka 2016, mahakama ya shirikisho ya New York iliwatia hatiani wapwa wawili wa mkewe kwa kula njama ya kuagiza kokaine nchini Marekani. Kesi hiyo inasema walipanga kutumia baadhi ya pesa hizo kufadhili kampeni za kisiasa za mkewe. Baadaye waliachiliwa.
Kuimarisha nguvu za Marekani
Kukamata dawa za kulevya baharini hakuhitaji nguvu kubwa kama Marekani inavyofanya sasa, kulingana na wachambuzi wa masuala ya kiusalama.
Pamoja na meli za Marekani tulizozifuatilia kote Puerto Rico – ambako Marekani ina kambi ya kijeshi – picha za satelaiti pia zilionyesha meli mbili takriban maili 75 (123km) mashariki mwa Trinidad na Tobago.
Marekani imeimarisha uwepo wake wa anga katika eneo hilo – BBC imezitambua ndege za kijeshi za Marekani katika eneo la Puerto Rico.
Mapema mwezi Oktoba, BBC ilifuatilia ndege tatu za B-52 ambazo ziliruka katika visiwa vya Karibiani na karibu na pwani ya Venezuela.
Jeshi la anga la Marekani baadaye lilithibitisha kwamba ndege hizo zilishiriki katika “shambulio.”
Ndege za B1 na ndege za kijasusi za P-8 Poseidon pia zimeonekana kwenye mitandao ya kufuatilia ndege.
Picha kwenye mitandao ya kijamii pia zimeonyesha helikopta za kijeshi zikipita katika pwani ya Trinidad na Tobago.
Baadhi ya ndege hizo ni Boeing MH-6M Little Birds – zilizopewa jina la utani “Killer Eggs” – zinazotumiwa na vikosi maalum vya Marekani
CIA itafanya nini Venezuela?
Alipoulizwa ikiwa CIA imepewa mamlaka ya kumtoa Maduro madarakni, Donald Trump alikwepa swali hilo na kusema itakuwa “ajabu” kujibu.
Pia amesema Marekani inaangalia uwezekano wa operesheni za kijeshi katika ardhi ya Venezuela.
CIA inatazamwa kwa mashaka mengi na wengi katika Amerika ya Kusini kwa sababu ya historia ndefu ya uingiliaji kati wa siri, majaribio ya mapinduzi ya serikali, na misaada kwa madikteta wa kijeshi wa mrengo wa kulia, haswa nchini Chile na Brazil.
Ned Price, naibu wa mwakilishi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa na aliyekuwa mchambuzi wa CIA na mshauri mkuu wa Wizara ya Mambo ya Nje, amesema, operesheni za siri za CIA ziko za namna nyingi.”
“Zinaweza kuwa operesheni za kupata taarifa. Operesheni za hujuma. Kufadhili vyama vya upinzani. Zinaweza kuwa hata kupindua utawala. Kuna operesheni nyingi kati ya kubwa na ndogo.”
Dk Sabatini anasema kutokana na kuwa Venezuela si kituo kikuu cha uzalishaji wa dawa za kulevya, hakuna kokeini au maabara ya fentanyl, lakini kuna viwanja vya ndege au bandari ambazo Marekani inaweza kuzilenga.
“Au kushambulia kambi ya kijeshi, ambazo zinatuhumiwa kujihusisha na ulanguzi wa kokeini. Au kujaribu kumkamata Maduro au baadhi ya watu wake wa karibu na kuwafikisha mahakamani nchini Marekani.
Ikiwa lengo kuu la shughuli hizo za kijeshi ni kumtishia Maduro, haijulikani ikiwa zitatosha kuchochea uasi.