
Dar es Salaam. Mamlaka ya Hali ya Hewa Tanzania (TMA) imetahadharisha kuwepo na uwezekano wa mvua kubwa, upepo mkali na mawimbi makubwa baharini.
Taarifa iliyotolewa na TMA leo Ijumaa Oktoba 24, 2025, imesema mvua hizo zitakazoambatana na upepo mkali unasababishwa na kimbunga kinachojulikana kama Tropical Storm Chenge ambacho kinatarajiwa kuathiri maeneo kadhaa nchini, ikiwemo Mkoa wa Dar es Salaam.
Mikoa mingine iliyotajwa ni Mtwara, Lindi, Pwani na Tanga pamoja na visiwa vya Unguja na Pemba inatarajiwa kupata mvua kubwa kuanzia Oktoba 26 hadi 28, mwaka huu.
TMA imesema utabiri wa hali ya hewa unaonyesha kuwa kimbunga hicho kinaendelea kusogea upande wa magharibi mwa Bahari ya Hindi huku kikipungua nguvu taratibu kadri kinavyokaribia pwani ya Tanzania.
“Hali hii inatarajiwa kusababisha ongezeko la mvua, upepo mkali na mawimbi makubwa katika maeneo ya ukanda wa pwani,” imesema sehemu ya taarifa ya TMA.
Hadi kufikia Ijumaa asubuhi, kimbunga hicho kilikuwa bado kiko katika Bahari ya Hindi, kaskazini-mashariki mwa Madagascar, takribani kilomita 1,680 kutoka pwani ya Mtwara.
TMA imesisitiza kuwa itaendelea kufuatilia mwenendo wa kimbunga hicho na kutoa taarifa zaidi kadri hali inavyoendelea kubadilika.
Wakati huohuo, mamlaka hiyo imewataka wavuvi, wasafiri wa baharini na wananchi kwa ujumla kuchukua tahadhari na kufuatilia ushauri wa wataalamu wa hali ya hewa ili kuepuka madhara yanayoweza kujitokeza.