Musoma. Sekta ya kilimo nchini imeelezwa kuwa sekta muhimu katika kufanikisha lengo la Serikali la kuifanya nchi ya Tanzania kuwa ya uchumi wa kati wa juu ifikapo mwaka 2050 endapo wataalamu wa sekta hiyo watatekeleza kwa ufanisi mpango wa mageuzi ya kilimo 2050.

Mpango huo pamoja na mambo mengine unalenga kumuinua mkulima wa kawaida hasa waliopo vijijini kuachana na kilimo cha mazoea cha kulima kwa ajili ya kujikimu badala yake wajikite katika kilimo biashara na kushindana katika soko la dunia.

Akifungua warsha ya kuwajengea uwezo  wataalamu kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara pamoja na wa Mamlaka ya Serikali za Mitaa mkoani Mara, Katibu Tawala wa Mkoa wa Mara, Gerald Kusaya amesema  wataalamu hao wanapaswa kuhakikisha wanaondoa dhana iliyojengeka katika jamii kuwa kilimo ni adhabu.

“Tunataka mabadiliko ya kilimo yaonekane kwa macho, tuachane na kilimo cha mazoea kilichosababisha kilimo kuonekana kama kitu cha ajabu sana na kinachofanywa na watu masikini,” amesema.

Kusaya amesema wataalamu hao wana wajibu wa kuondoa kilimo katika hali ya sasa na kukifanya kuwa miongoni mwa sekta muhimu ambayo ikitumika vema itamkomboa mwananchi kuondokana na umasikini kwa ngazi ya familia hadi taifa.

Amesema ili kufanikisha lengo hilo, wataalamu hao pia wanapaswa kusimamia kilimo kwa kuunganisha sekta za kilimo, uvuvi na mifugo ili kuleta tija sambamba na uchumi jumuishi kwa wananchi.

“Huu npango wa mageuzi ya kilimo 2050, mafanikio yake yako mikononi mwetu wataalamu, Watanzania wamechoka kuimba kilimo ni uti wa mgongo bila kuona matokeo, sasa wanataka matokeo halisi wanataka kuhama walipo kwenda mbele zaidi, kila mmoja kwa nafasi yake akatimize wajibu wake ili mpango huu utekelezwe kwa vitendo,” ameongeza.

Baadhi ya wataalamu wa sekta ha kilimo kutoka Ofisi ya Mkuu wa Mkoa wa Mara na Mamlaka za serikali za mitaa wakiwa kwenye warsha ya kujengewa uwezo juu ya utekelezaji wa mpango wa mageuzi ya kilimo 2050. Picha na Beldina Nyakeke

Mkurugenzi kutoka Ofisi ya Mageuzi ya Kilimo, Elizabeth Misokia amesema Serikali imeanzisha mpango huo kutokana na umuhimu wa sekta ya kilimo katika kufanikisha malengo ya dira ya taifa ya 2025/50.

Amesema utekelezaji wa mpango huo pamoja na mambo mengine utasaidia kufanya mageuzi makubwa katika sekta ya kilimo na kuwa sekta yenye tija na mchango mkubwa kwa ukuaji wa pato la mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Amesema sekta ya kilimo ina fursa nyingi katika kuchangia uboreshaji wa uchumi wa nchi na watu wake lakini sekta hiyo bado haijatumika vema, hivyo Serikali imeamua kwa makusudi kuhakikisha sekta hiyo inaleta mabadiliko katika maedeleo ya nchi.

Misokia amesema mpango huo unahusisha kilimo cha mazao 20 ambayo yatatumika kwa ajili kuleta mageuzi ya kilimo ambapo mazao hayo yatakuwa kwa ajili ya usalama wa chakula pamoja na kilimo biashara kinacholenga soko la ndani na nje ya nchi.

Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Musoma wamesema utekelezaji wa mpango huo ni jambo la muhimu huku wakisema masuala ya kilimo cha umwagiliaji na upatikanaji wa pembejeo kwa wakati ni miongoni mwa mambo yatakayosababisha mpango huo kuleta tija.

“Huo mpango usiwe wa kwenye makaratasi tunataka utafsiriwe kwa vitendo, wakulima wana changamoto nyingi zinahitaji suluhisho la kudumu na kama hilo litafanyika basi tujiandae kuwa na mabilionea wengi kutoka sekta ya kilimo kuanzia vijijini huko,” amesema Mwita Masirori.

Kabula Daniel amesema mabadiliko ya tabianchi yamesababisha wakulima kukata tamaa kutokana na kukosa mavuno ya kutosha hali ambayo pamoja na mambo mengine inasababisha mashaka kuhusu usalama wa chakula, hivyo mpango huo ukitekelezwa kwa vitendo mbali na kuwepo na uhakika wa chakula pia utasaidia katika kuboresha uchumi wa wakulika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *