Dar es Salaam. Kati ya vitu anavyovipigania zaidi Marioo katika muziki wake kwa sasa, basi ni kolabo na Diamond Platnumz, mwanzilishi wa WCB Wasafi na mshindi wa MTV EMAs mara tatu, akiwa kinara barani Afrika.
Pengine hii ndio sababu amekubali kuwepo katika video ya wimbo mpya wa Diamond, Sasampa (2025) licha ya kuwepo madai kuwa hawana uhusiano mzuri wa kikazi, na hata kutibuliana mipango.
Kwa baadhi ya mashabiki imekuwa ni mshangao kuona hilo, na wengine kwenda mbali zaidi wakidai ni kama anajipendekeza kwa sababu Diamond hajawahi kuonekana akimuunga mkono katika jambo lolote lile.
Wanaosema hivyo ni wale waliomini kuwa Marioo pekee ndio anaweza kushindana na Diamond kwa kutoa ngoma zinazovuma (hit songs) hapa Bongo, lakini sasa inakuwaje anaenda kuungana na mshindani wake!?
Ila kweli ni kwamba Marioo kazisoma vizuri alama za nyakati, anajua kabisa huu ndio wakati sahihi wa yeye kuipata kolabo na Diamond, na urahisi wa kuipata unatokanaje.
Hapo awali, wengi waliamini Diamond na WCB Wasafi wana wivu na mafanikio ya Marioo, wanamuogopa au wanataka kutembelea upepo wake baada ya kuona kuna kundi kubwa la mashabiki wanaomuunga mkono.
Mathalani Desemba 2022, Diamond aliibuka na kudai kuwa Marioo aliwahi kuomba kusainiwa WCB Wasafi ili amsaidie kupeleka muziki wake kimataifa, madai yaliyoacha maswali kibao!
Kati ya maswali hayo, ni kwanini aseme hivyo kipindi Marioo anafanya vizuri? Je, wasanii wote aliowahi kuwasaini WCB Wasafi wamefanya vizuri kimataifa? chukua mfano wa Lava Lava.
Jambo hilo na mengine mengi, ndio yaliibua hisia kuwa WCB Wasafi waliamua kumtumia Mbosso ili kushindana na Marioo, kitu kilichofanya wasanii hao kuwa na migongano ya kila mara.
Marioo aliwahi kumtuhumu Mbosso kwa madai ya kungojea kila anapotoa wimbo, basi naye atafanya hivyo siku chache zijazo (wanaita kupandishiana nyimbo) kwa lengo la kuupoteza wake.
Kwa upande wake Mbosso alimtuhumu mshindani wake kwa kufuta vesi yake katika wimbo waliorekodi pamoja ambao ulitarajiwa kuwamo katika albamu ya kwanza yake Marioo, The Kid You Know (2022).
Ni kweli kwa sehemu wasanii hao walikuwa na ushindani tunaoweza kuita wa kuviziana au usio wa wazi, kila mmoja alitoa ngoma kali ambayo mashabiki walijaribu kuipambanisha na ya mwenzake.
Mapema mwaka huu, Mbosso aliondoka na WCB Wasafi na kisha kutoa Extended Playlist (EP), Room Number 3 (2025) ikiwa na nyimbo saba. Kati ya hizo, wimbo wake ‘Pawa’ ndio uliofanya vizuri na Mbosso kuutaja kuwa namba Tanzania.
Punde tu, Marioo akatoa toleo dogo (Deluxe) la albamu yake, The God Son (2024), kati ya nyimbo zilikuja na mradi huo, ni ‘Dunia’ ambao naye aliutaja kama wimbo namba moja Tanzania, kitu kilichoonyesha ushindani wa wazi.
Na baada ya Diamond kudai alishiriki kuandika wimbo wa Mbosso ‘Pawa’, kitu kilichosababisha kurushiana maneno mtandaoni, Marioo aliibuka na kauli ambayo ilitafsiriwa kumlenga Mbosso.
“Tangu Mama Amina mpaka leo sijapoa, sijaboa, na nakumbuka sijawahi kubebwa na lebo yoyote kubwa wala kuandikiwa wimbo. Na bado kuna wasanii wametoka kupitia mimi,” alieleza Marioo.
Hivyo kwa sasa ambapo Mbosso hayupo WCB na ameshapishana kauli na Diamond, Marioo anaona ndio wakati wa kupata kolabo yake na Diamond.
Na kwa jinsi Bongofleva ilivyo na tabia zake za kipekee, Diamond lazima atafanya kolabo hiyo kwa lengo tu la kumuinua Marioo juu zaidi ya mshindani wake ambaye ni Mbosso.
Diamond amekuwa na tabia ya kushirikiana na wale waliokinyume na washindani wake au aliopishana nao kauli katika muziki. Kivipi?
Mfano Diamond aliwahi kudai Joh Makini alimkatalia kufanya kolabo. Baadaye Diamond huyo akaja kushirikiana na G Nako aliyepo kundi moja na Joh Makini (Weusi), kolabo ambayo wengi hawakuitarajia.
Sasa endapo Marioo atafanikiwa kuipata kolabo na Diamond, basi ni atakuwa amemaliza kazi na wale wasanii wanaoikimbiza Bongofleva baada ya hapo awali kushirikiana na Harmonize, Alikiba na Rayvanny.
Mathalani, Marioo na Harmonize wameshirikiana katika nyimbo tano – Naogopa (2022), Away (2024), Disconnect (2024), Wangu (2024) na Pere (2025) ambao Rayvanny pia alishiriki.
Kiu ya Marioo kwa sasa ni kuona muziki wake unaenda kimataifa, kwa Bongo mtu pekee aliyesalia anayeweza kumsaidia kufanikisha hilo ni Diamond. Kolabo na kina Harmonize na Alikiba zimeishia hapa hapa Bongo kama kazi nyingine ambazo hazikupaa kimataifa.