Dar es Salaam. Wakati uanzishwaji wa maeneo kwa ajili ya utunzaji wa mwili, afya na mapumziko (sauna na spa) ukiongezeka, angalizo limetolewa kuhusu huduma hizo ikielezwa baadhi hutweza utu, hususani kwa wanawake.

Sauna ni chumba maalumu chenye joto kali (kwa kawaida kati ya nyuzijoto sentigredi 70 hadi 100) kinachotumika kwa ajili ya kutoa jasho ili kusafisha ngozi na kutoa sumu mwilini.

Vilevile, hutumika kupumzisha misuli baada ya mazoezi au uchovu, kuhamasisha mzunguko wa damu kwa kuwa joto hupanua mishipa ya damu na kupunguza msongo wa mawazo na hivyo kutoa hali ya utulivu.

Spa au pia Spar ni kituo au sehemu inayotoa huduma mbalimbali za urembo, utulivu na afya, kikijumuisha huduma za kusinga ili kupumzisha misuli, kupunguza maumivu na msongo wa mawazo.

Huduma zingine ni za kusafisha na kutunza ngozi ya uso, usafi wa kucha za miguu na mikono,kuondoa ngozi iliyokufa na kufanya ngozi laini. Pia hutumia kutumia maji kwa ajili ya tiba na mafuta yenye harufu nzuri kwa utulivu wa akili na mwili.

Kwa wastani huduma hizi hugharimu kati ya Sh30,000 na Sh300,000 kulingana na inayotolewa, eneo na umaarufu wa eneo husika.

Usasa huu unaoambatana na matangazo kupitia mitandao ya kijamii ili kuvutia wateja, aghalabu husababisha mwili kutoonekana tena kama ni kitu cha kusitiri.

Hii ni kutokana na ukweli kuwa, katika spa na sauna, watu huvaa taulo au vazi jepesi kwa sababu mazingira ya maeneo hayo, yamejengwa kwa ajili ya matibabu ya mwili na ngozi.

Kwa jamii ya Kitanzania yenye misingi ya maadili ya dini na mila, kwa kiasi fulani usasa huu una hatari ya kupunguza heshima ya kusitiri mwili, kwani wapo ambao huyatumia maeneo hayo kunyoa nywele za kwapa na sehemu za siri na wengine wakisingwa maeneo nyeti na wahudumu wa jinsia zote.

Kwa mazingira ya sauna ambako wanaume au wanawake huvaa mavazi mepesi au kuwa watupu, yanaweza kuonekana kuwa ni kinyume cha maadili.

Watumiaji huduma

Mkazi wa Kinondoni, Dar es Salaam ambaye ni mmoja wa watumiaji wa huduma hizo aliyeomba kutotajwa jina, anaeleza alianza kutumia huduma za kusafisha mwili, ikiwamo sehemu za siri baada ya kuhamasishwa na rafiki zake.

“Nilikuwa nasikia kama ni kitu cha kifahari. Unakaa kwenye mvuke, unapewa dawa za asili, unahisi mwili umetulia. Sasa hivi nakwenda mara moja kila mwezi,” anasema.

Anaeleza wateja wengi wa vituo hivyo ni wanawake wa umri kati ya miaka 25 hadi 45, wakiwamo wafanyakazi wa ofisini na wajasiriamali wadogo.

“Binafsi sioni tatizo, ninachojali ni kuutunza mwili wangu, ikizingatiwa anayenihudumia ni mwanamke mwenzangu, hivyo hakuna cha ajabu atakiona kwangu,” anasema.

Mtazamo kimaadili

Mtaalamu wa saikolojia ya jamii, Frida Lema amesema huduma hizo zimeanza kuvuka mipaka ya heshima, hasa zinapohusisha kuguswa sehemu nyeti na watu wasio madaktari.

“Huduma za urembo ni halali, lakini tunapofika hatua ya mtu kuguswa au kunyoa sehemu za siri na mtu asiye na uhusiano wa kiafya, tunavunja maadili na heshima ya mwili,” anasema Frida.

Anaeleza vijana wengi wanachukulia huduma hizo kama fasheni, bila kutafakari madhara yake kiakili na kimaadili.

“Hii ni sehemu ya utandawazi unaoleta mchanganyiko wa tamaduni, lakini bila mwongozo, tunapoteza misingi ya utu,” anasema.

Tecla Mtambo, mkazi wa Mbagala Majimatitu, anasema kinachoendelea ni ushahidi kuwa wanawake wanashindwa kujihudumia hata miili yao, kiasi cha kuhitaji msaada wa mtu mwingine.

Tecla, mwenye umri wa miaka 80 anasema zamani haikuwa kawaida kwa mwili wa mwanamke kuonekana kama ilivyo sasa, lakini kutokana na uvivu uliokithiri imefikia hatua hata kujifanyia usafi hawawezi.

“Wanawake wa siku hizi hata kuinama kukata kucha miguuni hawawezi, unakuta kuna kijana wa kiume ndio anafanya kazi hiyo na kumsugua miguu, sisi zamani tulikuwa tunasugua wenyewe miguu kila unapooga,” anasema na kuongeza:

“Siku hizi nasikia hata usafi wa sehemu nyeti unaweza kufanywa na mtu mwingine, hii ni aibu, sijui huu utamaduni umetoka wapi. Mwili wa mwanamke haupaswi kushikwashikwa hovyo kwa kisingizio cha kusafishwa, ndiyo maana Mungu alitupa viungo kama mikono ili tujihudumie.”

Rajab Suba, mkazi wa Kimara anasema kinachofanyika ni maendeleo ya teknolojia na hakuna namna Watanzania wakaishi kama kisiwa.

“Huko duniani wanafanya hivyo ndiyo maana na sisi tunaiga, sioni shida ila kwa upande mwingine kuna namna inatusumbua wanaume, unajua mwanamume kamili hauwezi kuwa sawa kama unaingia mtandaoni kila dakika unaona picha na video zinazoonyesha wanawake wakiwa watupu wanasuguliwa mapaja au makalio,” anasema.

Sheikh Rashid Nsemo wa Msikiti wa Kisemvule anasema: “Usafi ni jambo jema, lakini haimaanishi kuvua nguo kwa mtu asiye mume wako. Mwanamke anapaswa kuwa na mipaka. Tunahitaji kurudisha heshima ya mwili.”

“Mwanamke ana wajibu wa kujitunza, lakini si kwa kuvua heshima yake au kujionyesha kwa namna inayovutia hisia za kimwili. Hii tabia ya kuingia kwenye vituo vya kusafishwa sehemu nyeti, mara nyingine ni kwenda mbali kupita kiasi,” anasema.

Anasema Serikali iangalie namna ya kuweka kanuni za maadili katika biashara za urembo kama inavyofanywa kwa huduma za afya.

Anashauri wanawake kuwa makini na huduma zinazohusisha kuguswa au kuangaliwa na watu wasio maharimu, akisema jambo hilo linaweza kuvunja maadili ya dini na desturi.

Mchungaji Joseph Mwinuka, anasema huduma hizo zinachochea mtazamo wa mwili wa mwanamke kama bidhaa ya burudani, badala ya sehemu takatifu ya utu na heshima.

Anasema vijana wengi wa kike sasa wanaanza kuziona huduma hizo kama ishara ya urembo au njia ya kumvutia mwenza, badala ya afya.

“Hii ni hatari kwa jamii inayojitahidi kulea vizazi vyenye maadili. Inafikia mahali mtu anahisi hana thamani bila huduma hizo,” anasema.

Kauli ya watoa huduma

Baadhi ya watoa huduma wanasema hakuna la ajabu katika wanachofanya.

“Tunatoa huduma ya kitaalamu. Hatuna mawazo ya kingono kama watu wanavyodhani. Wateja wanakuja kwa hiari yao na tunaheshimu faragha zao,” anasema Sharon Mtega, mmiliki wa spa iliyopo Sinza, Dar es Salaam.

Mtoa huduma mwingine ambaye hakutaka jina lake litajwe anasema tofauti na ilivyokuwa awali, suala la taaluma linazingatiwa na kupewa kipaumbele.

“Kipaumbele chetu ni kuzingatia faragha ya mteja, halafu huduma hii haitolewi na mtu asiyeelewa, ndiyo maana hata hizo video na picha huwa zinapigwa endapo mteja ataridhia na mara nyingi hazionyeshi sura. Inafanyika hivyo ili kuonyesha watu wengine manufaa yatokanayo na huduma hizo muhimu kwa mwili na mtu anayejipenda,” anasema.

Tahadhari yatolewa

Katika baadhi ya vituo huduma hutolewa kwenye vyumba vidogo vyenye mvuke unaotokana na mitishamba.

Miongoni mwa mitishamba inayotumika ni majani ya mlonge, mchaichai, mshubiri (aloe vera), mdalasini na karafuu, zikielezwa kusaidia kusafisha mwili wa mwanamke na hasa ukeni.

Daktari wa afya ya uzazi, Halima Sanga, anasema ingawa baadhi ya mitishamba inaweza kusaidia kupunguza harufu au maambukizi madogo, matumizi holela ya huduma hizo yanaweza kuwa hatari.

“Sehemu za siri za mwanamke zina mfumo maalumu wa kujisafisha zenyewe. Ukijaribu kutumia dawa au mvuke kupita kiasi unaharibu uwiano wa asidi na bakteria wazuri. Hilo linaweza kusababisha maambukizi makubwa au utasa,” anasema.

Anaeleza baadhi ya wanawake wameishia kupata maumivu, muwasho au hata vidonda kutokana na kutumia huduma hizo mara kwa mara.

Naye Dk Edward Komba natoa tahadhari akisema: “Ngozi ya sehemu za siri ni laini, hivyo mtu anaweza kupata michubuko au maumivu makali. Scrub (kusafisha ngozi kwa kusugua) inapofanyika kupita kiasi inaweza kuharibu ngozi na kusababisha muwasho au michubuko.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *