Chanzo cha picha, Sputnik/Alexander Kazakov/Pool via Reuters and Reuters
Wiki moja iliyopita huku Marekani ikitoa vitisho kwa Urusi kuwa itapeleka makombora ya Tomahawk kwa Ukraine kama njia ya kuishinikiza Moscow kuachana na vita – Vladimir Putin na Rais Donald Trump walizungumza kwa simu. Matokeo ya simu hiyo, ni tangazo la mkutano wa Marekani na Urusi mjini Budapest.
Agosti iliyopita, huku kukiwa na vitisho vya vikwazo vya ziada vya Marekani dhidi ya Urusi, Putin alikutana na mjumbe maalum wa Trump Steve Witkoff. Matokeo: tangazo la mkutano wa Marekani na Urusi huko Alaska.
Mkutano wa Alaska ulifanyika, chini ya maandalizi madogo na matokeo kidogo. Lakini mkutano wa Budapest, Rais Trump ameuahirisha.
“Hakuna haja ya kufanya mkutano wa kupoteza muda,” rais wa Marekani aliwaambia waandishi wa habari.
Kama hilo halitoshi, hapo awali Trump alionekana kutumia mbinu ya kuuma na kupuliza katika kutekeleza shinikizo zake kwa Kremlin.
Kwa sasa hapulizi tena. Badala yake ameziwekea vikwazo kampuni mbili kubwa za mafuta za Urusi, Rosneft na Lukoil.
Hilo halitamlazimisha Rais Putin kkukomesha vita vyake. Lakini ni ishara ya kuchanganyikiwa kwa Trump na kutokukubaliana kwake na Ikulu ya Kremlin – kwa kutaka kufanya maafikiano au makubaliano yoyote ili kusitisha mapigano nchini Ukraine.
Kipi kimebadilika?
Urusi haifurahishwi na mbinu hiyo.
Siku ya Alhamisi, Rais Putin aliwaambia waandishi wa habari kwamba vikwazo vipya vya Marekani ni “kitendo kisicho cha kirafiki” na ni uamuzi wa kujaribu kuiwekea Urusi shinikizo.
“Lakini hakuna nchi inayojiheshimu na hakuna watu wanaojiheshimu wanaofanya maamuzi kwa sababu ya shinikizo.”
Rais wa zamani wa Urusi Dmitry Medvedev hakutumia lugha ya kidplomasia.
“Marekani ni adui yetu na mropokaji wao kuhusu amani, sasa amejiweka katika njia ya vita na Urusi,” aliandika kwenye mtandao wa kijamii. “Maamuzi ambayo yamechukuliwa ni kitendo cha vita dhidi ya Urusi.”
Toleo la Alhamisi asubuhi la jarida la udaku la Moskovsky Komsomolets lilikuwa la kustaajabisha kidogo. Jarida hilo linakosoa “kutobadilika na kutotabirika kwa mshirika mkuu wa [Urusi] katika mazungumzo.”
Badala ya kukimbilia kwenye mkutano wa pili, kama alivyofanya katika mkutano wa kilele wa kwanza, wakati huu Rais Trump amekuwa mwangalifu zaidi.
Alimtaka Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio kufanya mkutano na Waziri wa Mambo ya Nje wa Urusi Sergei Lavrov ili kuhakikisha kuwa kuna umuhimu wa kwenda kufanya mkutano Budapest.
Na ikawa wazi kuwa hakuna umuhimu wa kufanya mkutano wa Budapest, mkutano mpya usingeweza kuleta mafanikio.
Urusi inapinga vikali wazo la Donald Trump la kuacha mapigano nchini Ukraine.
Kremlin imedhamiria kuchukua udhibiti, angalau, wa eneo lote la Donbas mashariki mwa Ukraine.
Lakini Rais Volodymyr Zelensky anakataa kukabidhi eneo hilo kwa Urusi, na sehemu za Donbas ambazo Ukraine bado inadhibiti.
Moscow inataka mkutano?
Chanzo cha picha, Reuters
Mkutano wa kwanza, huko Alaska, yalikuwa ni mapinduzi ya kidiplomasia na kisiasa kwa Kremlin. Kukaribishwa katika zulia jekundu huko Anchorage kuliashiria kurejea kwa Urusi katika jukwaa la kimataifa na kushindwa kwa nchi za Magharibi kuitenga Moscow.
Katika wiki iliyopita vyombo vya habari vya serikali ya Urusi vimekuwa vikifurahia wazo la mkutano na Rais Trump barani Ulaya, lakini bila Umoja wa Ulaya mezani. Wachambuzi wa Urusi walionyesha mkutano uliopendekezwa huko Budapest kama kofi kwa Brussels.
Wakati huo huo, wachache walionekana kuamini kwamba, hata kama utafanyika, mkutano wa Budapest utatoa aina ya matokeo ambayo Moscow inayataka.
Baadhi ya magazeti ya Urusi yamekuwa yakitoa wito kwa jeshi la Urusi kuendelea na mapigano.
“Hakuna sababu hata moja ambayo Moscow inapaswa kukubali kusitisha mapigano,” alitangaza Moskovsky Komsomolets jana.
Hiyo haimaanishi kwamba Kremlin haitaki amani.
Inataka. Lakini kwa masharti yake. Ni masharti ambayo hayakubaliki kwa Kyiv na sasa inaonekana hayakubaliki na Washington.
Masharti hayo yanahusisha zaidi eneo. Moscow inadai kwamba kile inachokiita “sababu kuu” za vita vya Ukraine kushughulikiwa: kusitisha upanuzi wa Nato kuelekea mashariki.
Moscow pia inaaminika kwa kiasi kikubwa katika lengo la kuilazimisha Ukraine kurudi kwenye himaya ya Urusi.
Je, Donald Trump yuko tayari kuongeza shinikizo kwa Urusi?
Anaweza kuongeza.
“Katika mchezo wa kuvuta kamba wa Trump, Urusi inaongoza tena,” aliandika Moskovsky Komsomolets baada ya mkutano wa kilele wa Budapest kutangazwa.
“Katika wiki chache kabla ya mkutano wa Budapest, Trump atavutwa upande mwingine kwa simu na ziara kutoka Ulaya. Kisha Putin atamvuta tena upande wetu.”
Imetafsiriwa na Rashid Abdallah na kuhaririwa na Ambia Hirsi