Viongozi wa Umoja wa Ulaya wameitaka Halmashauri Kuu ya Umoja huo kuendeleza mpango wa kuihudumia kifedha Ukraine kwa kipindi cha miaka miwili ijayo, huku wakiacha wazi mjadala kuhusu uwezekano wa kutumia mali za Urusi zilizozuiwa katika nchi wanachama kufadhili mikopo hiyo mikubwa.
Katika maazimio yao yaliyotolewa baada ya mazungumzo marefu mjini Brussels, Ubelgiji, viongozi wa Umoja wa Ulaya hawakuidhinisha rasimu ya kutumia euro bilioni 140 zilizozuiliwa kutokana na mali za Urusi kama sehemu ya fedha za kuifadhili Ukraine. Badala yake, wameahirisha uamuzi huo muhimu hadi mwezi Desemba.
Wanadiplomasia wanasema rasimu hiyo ni hatua moja mbele kuelekea makubaliano, japokuwa imekumbwa na upinzani kutoka kwa Ubelgiji, nchi ambayo benki zake zinahifadhi sehemu kubwa ya dhamana za Benki Kuu ya Urusi tangu uvamizi wa Ukraine ulipoanza mwaka 2022.
Ulaya yaihakikishia Ukraine ufadhili
Rais wa Baraza la Ulaya, Antonio Costa, alisema Umoja huo umejitolea kuhakikisha mahitaji ya kifedha ya Ukraine yanatimizwa kwa miaka miwili ijayo. Amesisitiza kuwa Urusi inapaswa kuelewa kuwa Ukraine itaendelea kuwa na rasilimali za kifedha zinazohitajika kujilinda.
“Kwa ufupi, tunaendelea kutumia njia zote tulizo nazo kuiweka Ukraine katika nafasi ya nguvu. Mazungumzo na Putin yakianza, na tunatumai yataanza karibuni, hali haitabadilika. Ujumbe wetu ni wazi: Ulaya haitaiacha Ukraine,” amesema Costa.
Umoja wa Ulaya ulizuia takriban euro bilioni 200 za mali za Benki Kuu ya Urusi baada ya uvamizi wa mwaka 2022. Hata hivyo, Tume ya Ulaya inapendekeza fedha hizo zitumike kutoa mikopo mikubwa kwa Kyiv bila kuzitaifisha moja kwa moja.
Ursula von der Leyen: Bado kuna kazi ngumu juu ya pendekezo lenye utata
Rais wa Ukraine, Volodymyr Zelensky, aliyeshiriki mkutano huo wa kilele mjini Brussels, alikaribisha maamuzi hayo kama ishara ya msaada wa kisiasa kutoka Ulaya katika azma ya kutumia mali za Urusi kuisaidia Ukraine kuendelea kupambana.
Mapema Ijumaa, Waziri wa Uchumi wa Ujerumani, Katherina Reiche, aliwasili mjini Kyiv kwa ziara inayolenga kuonyesha utayari wa Ujerumani kuisaidia Ukraine kukarabati miundombinu yake ya nishati iliyoharibiwa na mashambulizi ya Urusi.
Wakati huo huo, Rais Zelensky anatarajiwa kuelekea London, ambako mwenyeji wake, Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, amesema atatoa wito kwa viongozi wa Ulaya kuongeza msaada wa kijeshi kwa Ukraine, ikiwemo kuipatia makombora ya masafa marefu.
(AFPE, RTRE;EBU)