Viongozi hao wameweka masharti ikiwemo kuacha nafasi yamakubaliano hayo kupitiwa upya tena katika siku zijazo.
Hakuna uamuzi wa mwisho uliofikiwa na hakutarajiwi uamuzi, ila mazungumzo hayo ya viongozi hao yanatarajiwa kutoa mwelekeo wa makubaliano ndani ya wiki mbili zijazo.
Viongozi wa mataifa 27 ya Umoja wa Ulaya wamefanya mazungumzo mjini Brussels kujaribu kupata mwafaka kutokana na malengo yao kadhaa waliyo nayo, ambayo ni kuunga mkono biashara za umoja huo zinazodorora ikiwemo sekta ya magari na kwa upande mwengine, kuongoza katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya tabia nchi.
Mazingira mazuri yawekwa
Mkutano huo unafanyika wakati ambapo Umoja wa Ulaya unakabiliwa na shinikizo la lengo lao kubwa la kupunguza utoaji wa gesi chafu kuelekea mkutano mkuu wa mazingira wa Umoja wa Mataifa utakaofanyika nchini Brazil mnamo Novemba 10.
Rais wa Baraza la Umoja wa Ulaya Antonio Costa amesema mkutano huo wa Alhamis uliweka mazingira mazuri ya kuelekea kufikia lengo hilo la Ulaya la mwaka 2040.
Mnamo mwezi Julai, Tume ya Ulaya ilisema inataka kupunguza utoaji wa gesi chafu ya kaboni kwa asilimia 90 ifikiapo mwaka 2040 ikilinganishwa na viwango vya miaka ya tisini.
Lakini kuna idadi inayoongezeka ya nchi ambazo hazijaridhika kama vile Poland na Jamhuri ya Czech zinazosema kuwa lengo hilo la Ulaya haliwezi kufikiwa.
Mataifa yaliyotia saini Mkataba wa Mazingira wa Paris wa mwaka 2010, yanatarajiwa kuwasilisha mpango wa kupunguza utoaji wa gesi chafu kufikia mwaka 2035 huko Brazil, mpango ambao Ulaya ilikuwa inalenga kuutoa kutoka kwenye mpango wake wa mwaka 2040.
Wafanyabiashara wengine wanalalamika kuwa wanatakiwa kuwekeza katika kuzifanya biashara zao kuwa za kijani wakati ambapo mivutano ya kibiashara na ushindani kutoka China unazibana faida zao.
Umoja wa Ulaya una dhamira kati ya watoaji wakuu wa gesi chafu
Wanaharakati wanasema hatua hiyo iliyopigwa na Umoja wa Ulaya leo inatoa nafasi ya kuangazia hofu za kisiasa zilizopo na kutoa mwelekeo unaohitajika kusonga mbele na maamuzi muhimu ya kisera.
Linapokuja suala la utoaji wa gesi chafu mbali na China, Marekani na India, Umoja wa Ulaya ndio mojawapo ya watoaji wakuu wa gesi chafu waliodhamiria kuchukua hatua, huku umoja huo ukiwa tayari umepunguza utoaji wa gesi hiyo chafu kwa asilimia 37 ikilinganishwa na viwango vya mwaka 1990.
Wanaharakati wa mazingira lakini wanasema hatua zaidi zinahitajika kuchukuliwa ili kuzuia athari mbaya zaidi za ongezeko la joto duniani na kuwashawishi wale ambao hawajachukua hatua zozote, kufuata mkondo wa Ulaya.
Wanaharakati hao vilevile wanasema ni muhimu kwa Ulaya kuekeza na kuwa mstari wa mbele katika teknolojia ya kijani na usiachwe nyuma na China.
Vyanzo: AFPE/DPA