Kundi la waasi nchini Jamhuri ya Kidemorasia ya Congo, M23 lilikanusha madai kwamba wapiganaji wake walipora takriban kilo 500 za dhahabu kutoka kwa kampuni ya Twangiza Mining iliyo mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, DRC.
Kampuni inayofanya kazi katika jimbo la Kivu Kusini, ambayo sehemu kubwa iko chini ya udhibiti wa M23, ilisema wiki hii kwamba M23 “imesafirisha dhahabu kwa njia ya siri.”
Pia ilishtumu waasi hao kwa kutumia wataalamu wa Rwanda kuchimba data za kijiolojia ili kuanza tena na kupanua uchimbaji madini.
Rwanda imekanusha mara kwa mara kuwaunga mkono waasi wa M23, licha ya madai ya kutoka kwa wataalamu wa Umoja wa Mataifa na serikali za Magharibi na za kanda.
Katika mkutano na waandishi wa habari siku ya Alhamisi, Corneille Nangaa, kiongozi wa muungano wa waasi unaojumuisha M23, alisema mgodi huo haufanyi kazi na kwamba wachimbaji wadogo pekee ndio wanaofanya kazi huko.
Alisema M23 haikuwa na vifaa muhimu vya kuendesha mgodi. Nangaa pia amevishtumu vikosi vya serikali ya DRC kwa kushambulia eneo hilo ikiwa ni pamoja na kulipua angani. Alisema raia wameuawa katika mashambulizi hayo lakini hakueleza idadi ya vifo.
Mashambulizi ya ndege zisizo na rubani mnamo Oktoba 15 yaliharibu miundombinu ya kuzalisha umeme kwenye mgodi huo, kampuni hiyo ilisema.