Takriban watoto watatu wanakufa kila siku katika mji wa El-Fasher, mji mkuu wa jimbo la Darfur Kaskazini nchini Sudan, kutokana na utapiamlo na magonjwa, kulingana na taarifa iliyotolewa na Kundi la Madaktari la Sudan siku ya Ijumaa.

“Kwa zaidi ya mwezi mmoja, hali ya kibinadamu mjini El-Fasher imezidi kuwa mbaya sana, huku idadi ya vifo vya watoto ikiendelea kuongezeka kutokana na uhaba wa chakula na kuongezeka kwa visa vya utapiamlo, bila ya kuwa na dalili za kufunguliwa kwa njia yoyote ya misaada ya kibinadamu ambayo ingeweza kuokoa maelfu ya watoto,” ilisema taarifa hiyo.

Kundi hilo limesema “tunafuatilia kwa wasiwasi mkubwa hali hiyo ya kusikitisha kupitia wafanyakazi wetu huko El-Fasher. Tunwathibitishia jumuiya ya kimataifa kwamba hali ya kibinadamu imezidi kuzoroteka kutokana na uhaba wa chakula na dawa unaosababishwa na kizuizi kinachoendelea,” iliongeza taarifa hiyo.

Taarifa hiyo iliongeza: “Kila siku inayopita, tunapoteza takriban watoto watatu kutokana na utapiamlo, magonjwa, na uhaba mkubwa wa rasilimali za matibabu na kibinadamu.”

Alhamisi, mashirika manne ya Umoja wa Mataifa — Shirika la Kimataifa la Uhamiaji, UNICEF, Mpango wa Chakula wa Dunia, na shirika la wakimbizi la UN — yalieleza katika taarifa ya pamoja kuwa raia 260,000, ikiwa ni pamoja na watoto 130,000, wamekwama El-Fasher, bila chakula, maji, na huduma za afya.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *