
Akiwa mjini Geneva, mwakilishi wa WHO katika maeneo yanayokaliwa na Israel, Rik Peeperkorn, amesema usambazaji wa dawa na vifaa vya matibabu vilivyokuwa vimezuiwa kwa miezi kadhaa, umeanza kufikishwa katika baadhi ya maeneo ya Gaza.
Hata hivyo, Peeperkorn amesema ukweli kwamba Israel imefungua vivuko viwili pekee vya mpaka unafanya iwe vigumu kukidhi mahitaji makubwa ya kiafya ya eneo hilo.
Hospitali 14 pekee ndizo zinazofanya kazi kwa sehemu Gaza
Kwa mujibu wa WHO, ni hospitali 14 pekee kati ya 36 katika Ukanda wa Gaza zinazofanya kazi kwa sehemu, zikiwa na vituo 64 kati ya 181 vya afya na vyumba vya matibabu 109 kati ya 359.
Shirika hilo limeeleza kuwa lina vifaa vyote muhimu vya afya kwa ajili ya Gaza, lakini linahitaji utaratibu bora na wa haraka wa kufikisha misaada hiyo kwa walengwa.
Israel inadhibiti njia zote za kufika Ukanda wa Gaza na inahitajika kuidhinisha kila usafirishaji wa misaada ya kibinadamu inayoingia katika eneo hilo.