Punde alipowasili London, Rais Volodymyr Zelensky alikutana kwanza na Mfalme Charles III katika kasri lake. Baadaye, alikutana na Waziri Mkuu wa Uingereza Keir Starmer, atakayeandaa mkutano wa baadaye na viongozi wengine 20 wa Ulaya ambao wamesema wako tayari kuisaidia Ukraine kujilinda baada ya vita vya sasa kumalizika.
Mkutano huo pia utaangazia njia za kusaidia kulinda miundo mbinu ya nishati ya Ukraine dhidi ya mashambulizi ya mara kwa mara ya Urusi, yanayolenga pia mifumo ya nishati ya Ukraine kuelekea msimu wa baridi.
Njia hizo ni pamoja na kuimarisha mifumo ya ulinzi ya angani na kuipa Ukraine makombora ya masafa marefu yanayoweza kufyatuliwa hadi katikati ya Urusi.
Wito wa kuipa Ukraine makombora ya masafa marefu
Mazungumzo ya mjini London, yanalenga kuongeza shinikizo kwa Rais Vladimir Putin, baada ya hatua za hivi karibuni zaidi za Marekani na Umoja wa Ulaya kutangaza vikwazo vipya dhidi ya mafuta ya nchi yake.
Hadi sasa Putin hajaitikia miito ya mazungumzo na Zelensky ili kumaliza vita hivyo ambavyo vimedumu kwa zaidi ya miaka mitatu na nusu sasa.
Mapema Ijumaa, Keir Starmer alisema kupitia taarifa kwamba mara kwa mara wamempa Putin nafasi ya kumaliza uvamizi wake Ukraine, kuacha kuwaua raia na awaondoe wanajeshi wake. Lakini bila mafanikio. Starmer anasema wanaweza kupiga hatua mbele zaidi katika kuisaidia Ukraine.
“Nadhani bado kuna hatua zaidi tunazoweza kuchukua kuhusu uwezo wetu, hasa uwezo wa muda mrefu na wa masafa marefu, na bila shaka kazi muhimu ya Muungano wa nchi zenye Nia, inapohusiana na dhamana za kiusalama zinazohitajika.”
Muungano wa Wenye Nia kusaidia Ukraine baada ya vita
Wengine wanaotarajiwa kushiriki mkutano huo wa London ni pamoja na Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Kujihami ya NATO Mark Rutte, Waziri Mkuu wa Uholanzi Dick Schoof na Waziri Mkuu wa Denmark Mette Frederiksen.
Hadi sasa hakuna ishara yoyote kwamba mzozo wa Urusi na Ukraine unakaribia kumalizika.
Maelfu kwa maelfu ya wanajeshi wa pande zote mbili katika mzozo huo wa Urusi na Ukraine wanauawa katika uwanja wa mapambano huku droni na makombora zikiendelea kufyatuliwa na kusababisha maafa.
Mapema Ijumaa, wizara ya Ulinzi ya Urusi ilisema imekamata vijiji 10 vya Ukraine wiki iliyopita.
(AFPE; EBU)