
-
- Author, Alfred Lasteck
- Nafasi, BBC Swahili
Kila msimu wa uchaguzi ufikapo nchini Tanzania, hufungua tena majeraha ya zamani ya Mariam Staford mwenye umri wa miaka 42.
Kwa wengi, mikutano na nyimbo, pamoja na jumbe za kampeni, zote zinaashiria fursa kwa watu kupaza sauti zao. Lakini kwa wale wenye ualbino, mambo hayo huleta hofu.
“Jambo la kwanza linalonijia ni hofu,” anaiambia BBC, wakati huu watu wakijiandaa kumpigia kura rais na wabunge siku ya Jumatano.
“Najua kwamba mauaji ya watu wenye ualbino hutokea hasa wakati wa uchaguzi nchini Tanzania, pale imani za uchawi zinapoongezeka. Ndiyo maana sishiriki katika kampeni … naogopa sana.”
Ualbino, ambao unaathiri takriban watu 30,000 nchini Tanzania, ni tatizo la kimaumbile ambalo hupunguza melanini – inayoifanya ngozi, macho na nywele kuwa na rangi.
Ushirikina umefanya wale walio na hali hiyo kulengwa. Imani potofu kwamba viungo vya watu wenye ualbino vinaleta utajiri, bahati, au mafanikio ya kisiasa vimechochea mashambulizi dhidi yao kote Tanzania.
Wanaharakati wanasema imani kama hizo huongezeka wakati wa maandalizi ya uchaguzi, muda watu wakitafuta ushawishi wa kisiasa.
Mariam anaijua hatari hii.
Mkasa wa Mariam
Mwaka 2008, moja ya miaka ya umwagaji damu zaidi kwa watu wenye ualbino nchini Tanzania wakati maandalizi ya uchaguzi wa mitaa yakiendelea, wanaume waliokuwa na mapanga walivamia chumbani kwake Kagera, eneo la mpaka lilo kaskazini-magharibi mwa Tanzania.
“Walikuja usiku wa manane, wakakata mkono wangu wa kulia [kutoka juu ya kiwiko] na kisha wakakata mkono wangu wa kushoto, na kuondoka nayo …
“Siku iliyofuata nilipelekwa kwenye zahanati, nikiwa nimepoteza fahamu, na daktari aliyeniona alisema: ‘Huyu tayari amekufa, mrudishe nyumbani mukamzike.'”
Mbali na matarajio ya wengi, Mariam alipona; lakini alikuwa na mimba ya miezi mitano na mtoto wake aliyekuwa tumboni hakupona.
Shambulio hilo si tu kwamba lilimsababishia ulemavu wa kudumu bali lilimlazimu kuondoka Kagera, moja ya vitovu vya mauaji ya watu wenye ualbino wakati huo.
Hatimaye aliishi katika amani mkoani Kilimanjaro, ambapo kikundi cha kutetea haki za watu wenye ualbino, Under the Same Sun, kilimjengea nyumba na kumfundisha kutumia mashine ya kushona. Sasa anatengeneza masweta.
Miaka kumi na saba baadaye, hofu haijaondoka.
“Hata sasa, wakati mwingine huota tukio hilo,” Mariam anasema. “Ninapoamka, ninagusa mikono yangu na kukumbuka kuwa haipo. Ni kitu ambacho sitawahi kukisahau.”
Kilichomtokea Miriam ni moja ya mashambulizi mengi yaliyolenga watu wenye ualbino na viungo vyao vya mwili.
Takwimu zinasemaje?
Chanzo cha picha, AFP via Getty Images
Shirika la Under The Same Sun linasema kumekuwa na matukio 211 ya aina hiyo nchini Tanzania kuanzia mwaka 2008 hadi sasa.
Mashambulizi sabini na tisa yalimalizika kwa waathiriwa kuuawa, katika visa vingine 100 watu walikatwa viungo lakini walipona, waathiriwa watatu hawakujeruhiwa, na katika visa viwili walengwa walitekwa nyara na bado hawajapatikana. Aidha, makaburi 27 yamefukuliwa huku sehemu za mwili zikiondolewa.
Mwaka 2008 pekee watu 35 wenye ualbino waliuawa, vifo vingine vingi huenda havikuripotiwa.
Mauaji hayo yalileta ukosoaji wa kimataifa, na kusababisha msako mkali wa serikali. Rais wakati huo Jakaya Kikwete alilaani mashambulizi hayo na kutaka wauaji wachukuliwe hatua kali.
Kutokana na hali hiyo, Tanzania iliongeza kasi ya uchunguzi lilipokuja suala la mauaji yanayohusiana na uchawi kwa watu wenye ualbino na kuimarisha sheria dhidi ya ubaguzi.
Pia kumekuwa na majaribio ya kuongeza uelewa wa umma kuhusu suala hilo.
Katika makutano ya barabara katika mji wa Sengerema kaskazini-magharibi mwa nchi, mnara umejengwa kuwakumbuka watoto, wanawake na wanaume wenye ualbino ambao wamepoteza maisha au kulemazwa katika mashambulizi.
Sanamu ya chuma inamuonyesha baba akiwa amembeba mtoto mwenye ualbino kwenye mabega yake huku mama akimkinga na jua.
Jina la Mariam limechongwa kwenye mnara huo.
Ndivyo ilivyo kwa Mariamu Emmanuel, ambaye alikuwa na umri wa miaka mitano tu alipouawa mwaka 2008.
Akiwa ameketi nyumbani kwao Mwanza, kaka yake, Manyashi Emmannuel, ambaye sasa ana umri wa miaka 25, anakumbuka siku hiyo. Uchungu bado unamuandama.
“Nilikuwa na umri wa miaka minane, na niliona miguu yake, mikono na ulimi vikikatwa na washambuliaji… Tangu wakati huo, nimekuwa na hofu. Ni hali ngumu sana wakati mwingine tunaposikia mashambulizi karibu na uchaguzi.”
Tukio moja limeripotiwa mwaka huu, katika mji wa kaskazini-magharibi wa Simuyu, mwezi Juni. Mwathiriwa hakujeruhiwa lakini sasa amehamishwa na kupelekwa kwenye nyumba salama.
Juhudi za Serikali

Rais Samia Suluhu Hassan hivi karibuni alionya dhidi ya kile alichokiita imani potofu za kimila akisema hazina nafasi katika uchaguzi wa Tanzania.
Senyi Ngaga, mkuu wa wilaya ya moja ya maeneo yanayokumbwa na mashambulizi hayo, anasema kampeni za elimu za serikali zimeleta uelewa, lakini maeneo ya vijijini yanasalia kuathiriwa na imani potofu pamoja na unyanyapaa.
Anataka ushiriki zaidi kutoka kwa kila mtu katika jamii kukomesha mashambulizi haya.
“Hivi majuzi tulifanya tamasha na waganga wa kienyeji ambapo tulikaa pamoja na kuzungumza,” mkuu huyo ameimbia BBC.
“Wakati uchaguzi unakaribia tuliwashauri pia wawe mabalozi wazuri wa kuwaambia wengine wakatae vitendo hivyo na kuhakikisha watu wenye ualbino wanalindwa.”
Wakati makundi ya kampeni na walionusurika wanasema kazi nyingi zaidi bado zinahitajika kufanywa na serikali, baadhi ya maendeleo yamepatikana.
Kampeni za uhamasishaji, programu za mashirika ya kiraia, na mipango ya ujumuishaji wa shule, yamesaidia kupunguza matukio katika baadhi ya maeneo.
Jamii inaanza kuelewa polepole kwamba watu wenye ualbino hawajalaaniwa na ushirikina unaweza kuwa na matokeo mabaya.
Lakini mauaji ya mwaka jana ya mtoto Asimwe Novath, aliyetekwa nyara nyumbani kwao mkoani Kagera, ni ukumbusho kwamba suala hilo halijaisha.
Walioshuhudia walisema mtoto huyo alichukuliwa kwa nguvu na watu wawili wasiojulikana alipokuwa akicheza na mamake.
Siku kumi na saba baadaye, sehemu za mwili wa Asimwe zilipatikana kwenye gunia, zimetupwa chini ya daraja katika eneo hilo hilo. Mabaki yake yalizikwa baadaye katika nyumba ya familia yake.
Washukiwa tisa wameshtakiwa kwa mauaji ya kukusudia kuhusiana na mauaji hayo, lakini kesi hiyo haijakamilika.
Kwa Mariam, kesi hiyo ilileta kumbukumbu zenye maumivu.
“Ilinirudisha kwenye usiku wangu wa kushambuliwa mwaka 2008. Najua maumivu hayo, na najua mama yake hatayasahau.”
Aliyoyapitia yanamaanisha kuwa hofu ni sehemu ya maisha yake ya kila siku. Huepuka maeneo ya watu wengi na mara chache huondoka nyumbani bila kusindikizwa.
Wakati uchaguzi wa Jumatano unakaribia Mariam anasema hatapiga kura, akiwa na mashaka kwamba kura hiyo haitoleta tofauti yoyote katika maisha yake.
Badala yake ataitumia siku hiyo kimya kimya nyumbani Kilimanjaro.