BEKI wa Simba, Antony Mligo ametaja sababu ya kukwepa kuvaa jezi namba 15 na kuchukua namba tano Msimbazi huku akimtaja nahodha wa zamani wa timu hiyo, Mohammed Hussein ‘Tshabalala’.
Wakati huohuo ameeleza kuwa hakuna mtu wa kuzuia mafanikio ya timu hiyo kutinga hatua ya makundi kuelekea mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Nsingizin Hotspurs itakayopigwa kesho, Jumapili, kwenye Uwanja wa Mkapa jijini Dar es Salaam.
Mligo ambaye amejiunga na Simba akitokea Namungo, amepishana na Tshabalala ambaye ametua Yanga baada ya kuitumikia timu hiyo kwa miaka 14. Mligo amechukua mikoba yake kwa kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mligo amesema anaheshimu makubwa yaliyofanywa na Tshabalala ndani ya Simba, lakini licha ya kupenda kuvaa jezi namba 15 hakutaka kuitumia na badala yake aliomba jezi namba tano huku akitaja sababu kuwa ni kutafuta rekodi zake mpya.
“Tshabalala amehudumu muda mrefu ndani ya Simba ameacha rekodi nyingi nzuri, ni kaka yangu na namheshimu. Kwa kuheshimu ubora wake sijataka kubeba mikoba yake kwa kuvaa jezi namba 15, nimetafuta kichaka changu.
“Napenda kuvaa jezi namba 15, ndio jezi yangu pendwa na Simba nilikuta haina mtu, sikutaka kuivaa nikaamua kutafuta namba tano ili na mimi nitengeneze rekodi zangu mwenyewe,” amesema.
Akizungumzia kuingia kikosini moja kwa moja, Mligo amesema ulikuwa ni muda sahihi kwake kujiunga na timu hiyo na atatumia kila dakika anayoipata kuipambania Simba iweze kufikia mafanikio huku akiweka wazi kuwa nafasi anayoipata anastahili.
“Sio rahisi kuingia moja kwa moja kikosi cha kwanza cha Simba naamini kujituma na kuamini kuwa kila kitu kinawezekana kwa kuweka jitihada mbele ndio siri ya mimi kuingia moja kwa moja kwenye kikosi, naahidi kila nafasi ninayoipata nitaitumikia kwa faida,” amesema na kuongeza:
“Simba ina kikosi kizuri na wachezaji wengi bora kujituma na kuonyesha nia ya kuwa na uthubutu kwa kupambana kuanzia uwanja wa mazoezi na kufanyia kazi dakika chache unazopewa na kocha kuipambania timu ndio kitu kinachonibeba na kunifanya nikaaminika na kupata nafasi ya kucheza sina sababu ya kuamini kuwa mimi ni bora zaidi ya wengine ila mimi ni mpambanaji ambaye sikubali kushindwa na ni mwanafunzi najifunza kila siku.”
Mligo alitumia nafasi hiyo pia kuwaita mashabiki wa Simba kujitokeza kwa wingi Jumapili kwenye uwanja wa Mkapa kuishuhudia timu yao ikifuzu hatua ya makundi kwa mara nyingine tena huku akiwahakikishia furaha ya ushindi.
“Mashabiki ni mchezaji wa 12 ujio wenu kwa wingi utaongeza chachu ya ushindani tupo tayari kuwafurahisha sapoti yenu ni muhimu tukutane kwa Mkapa bado hatujaridhika tunataka matokeo mazuri tutinge hatua ya makundi kwa rekodi nzuri ya kutoruhusu bao,” amesema.
Licha ya Mligo kuikataa jezi hiyo, sasa inavaliwa na David Kameta ‘Duchu’ ambaye awali alikuwa anavaa jezi namba tatu ambayo alimkabidhi mshambuliaji Jonathan Sowah.