
Mmoja wa Wajumbe wa Bodi ya Azam FC, Yusuf Bakhresa amezitakia kheri Yanga, Singida Black Stars na Simba akiziombea zifanye vizuri katika mechi zao za marudiano ya mashindano ya Klabu Afrika leo na kesho.
Akijibu ujumbe wa pongezi uliotolewa na Singida Black Stars kwa Azam FC baada ya timu hiyo kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika jana, Yusuf Bakhresa amesema anaziombea timu hizo zifanye vyema ili ziwakilishe vyema nchi.
“Asanteni sana Singida Black Stars. Mungu awasimamie kesho (leo) mfuzu pia. Nawaombea Dua njema pia Simba SC na Yanga SC, kufuzu hatua ya makundi tuipeperushe Bendera ya Tanzania vyema. All the best,” ameandika Yusuf Bakhresa.
Yanga leo kuanzia saa 11:00 jioni itakuwa na mchezo wa marudiano dhidi ya Silver Strikers ya Malawi ambao ni wa raundi ya pili ya Ligi ya Mabingwa Afrika msimu huu.
Katika mchezo huo ambao utachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga inahitajika kupata ushindi wa tofauti ya mabao mawili au zaidi ili iweze kutinga hatua ya makundi kwa vile ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Malawi wiki iliyopita.
Singida Black Stars yenyewe itakuwa katika Uwanja wa Azam Complex ikiikaribisha Flambeau Du Centre ya Burundi katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Ili itinge makundi, Singida Black Stars inahitaji ushindi wa aina yoyote au sare tasa kutokana na timu hizo kutoka sare ya bao 1-1 katika mechi ya kwanza.
Kesho kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Simba itaikaribisha Ndingizini Hotspurs ikiwa ni kama imeshaingiza mguu mmoja katika hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Katika mechi ya kwanza ugenini huko Eswatini, Simba ilishinda mabao 3-0 hivyo leo inahitaji ushindi au sare ya aina yoyote iweze kuingia hatua ya makundi.
Jana Azam ilikuwa timu ya kwanza ya Tanzania kuingia makundi baada ya kuibanjua KMKM kwa mabao 7-0 katika mechi ya marudiano ya raundi ya pili ya Kombe la Shirikisho Afrika.
Matokeo hayo yaliifanya Azam FC kusonga mbele kwa ushindi wa jumla wa mabao 9-0.