
Dar es Salaam. Kuna makabila au jamii zinazokosa herufi na maneno yanayotumika katika jamii zingine. Kwa mfano Wachina wana herufi zao zinazokosekana kwenye jamii zingine. Maandishi na matamshi yake ni sawa na sanaa ya ajabu kwetu sisi wengine. Lakini wenyewe wamefanikiwa kushikilia bomba wakiwa na sanaa yao mpaka kushawishi wengine wajifunze.
Ni kama vile Wamasai walivyo na herufi zisizoandikika. Kawaida ya maneno huenda nje ya mdomo, lakini wenzetu wana maneno yanayoingia mdomoni. Iwapo jamii ya Kimasai ingebuni vikaragosi vya kutambulisha herufi na maneno yake, bila shaka wangeweza kuishawishi dunia ijifunze lugha yao ukizingatia maisha yao yapo kwenye kanda za utalii.
Baadhi ya jamii zetu (hasa zinazotokea kanda za juu milimani) zinakosa herufi “R”. Sio jambo la kushangaza kwa kuwa lugha ni sauti za nasibu, na ni maridhiano tu yanayoifanya ikubalike au la. Pengine katika lugha zao asilia herufi hiyo haipo, hivyo wakazimika kutumia herufi “L” badala yake. Utasikia: “Kiongozi atakagua balabala ya Kilwa kabla ya kuludi Ikulu”.
Hawa wanatofautiana na kina Mura ambao hutumia “R” katika sehemu ya “L”. ukitaka kujua kuwa herufi “R” ni miongoni mwa zile maarufu kwenye jamii yao, anza na jina la kabila lao, halafu tazama majina ya koo zao maarufu yanavyotawaliwa na “R”.
Kuna taasisi ziliambukizwa na kuitumia herufi hiyo kama alama ya msisitizo. Ukisikia “Hiri razima rikarare rokapu” basi ujue kazi unayo. Lakini pia kuna swaga za vijana wa kileo katika matumizi ya lugha. Matamshi yao ya maneno yanaathiriwa kwa namna mbili, ya kwanza ni kulazimisha ladha ya lugha ngeni.
Vijana kwa kutaka kuonekana kuwa ni wasomi wanailazimisha herufi “R” katika maneno ya Kiswahili ili kuleta utofauti, na lugha ifanane na inavyotamkwa na mgeni.
Lakini pili hasa kwa walimbwende, ni kama ya kujitazama pozi za midomo na sura pale wanapoongea. Pindi wanapoona sura haileti mvuto kwa kutamka baadhi ya maneno ya Kiswahili, hutafuta mbadala wake unaokwenda kung’arisha sura.
Utasikia “rakini mimi siri ugari”. Si kwamba hapo ameathiriwa na utamaduni, bali hujihisi kuongeza urembo pindi akitamka maneno kama hayo. Vijana na jamii hizi zinajikuta wakati mwingine wanatumikia vyombo vya habari. Hapo ndipo hasa utakaposikia wale wenzetu wa milimani wakishindwa kuikwepa asili yao.
Sishangai pale watangazaji wanapokwenda kuwahoji wananchi na tukasikia maneno kama “mutu”, “ntoto” na maneno mengi ya kijadi. Nimesema lugha ni sauti za nasibu lakini zilizokubalika kimatumizi.
Hata majina ya maeneo maarufu yaliitwa tofauti na vile tunavyoyatamka sasa. Wagogo walimwona tembo akizama kwenye dimbwi dogo, wakaulizana “mbona idodomya?” kwa maana ya “mbona imezama?” Wazungu waliokuwa watawala wetu walishindwa kutamka “idodomya”, wakasema “dodoma”. Hiyo ikawa sababu ya eneo lile ambalo leo ndio Makao Makuu ya nchi kuitwa Dodoma.
Mnakumbuka kuwa Wazaramo walishindwa kutamka “Carrier Cops” na kuishia kutamka “Kariakoo”? Watani zangu wananiambia eti Msasani ilitokana na Wamakonde kuita “kwa Ncha Chani” badala ya “Kwa Mussa Hassani”! Inasemekana pia chanzo cha jina Newala kilikuwa ni ujenzi wa kisima kipya, chinga wakamsikia mzungu anakiita New Well. Haya yalikuwa maridhiano ya kuacha majina hayo yatumike kama yalivyokosewa.
Leo tunahesabu siku chache sana kabla ya kuifikia siku ya Uchaguzi Mkuu. Habari na matangazo kuhusu uchaguzi yamekuwa yakihanikiza nchini usiku na mchana. La ajabu makosa ya matamshi sasa hayana muda wa kurekebishwa hata na wanahabari. Wananchi na baadhi ya watangazaji wamekuwa wakisema “Twendeni tukapige kula” badala ya “Twendeni tukapige kura”.
Lugha inakubalika pale inaponyosha bila kuharibu maana ya maneno. Nakumbuka Charles Hillary, mtangazaji wa Radio Tanzania wa enzi zetu aliwahi kutangaza mtanage baina ya Timu ya Taifa ya Tanzania dhidi ya Timu ya Taifa ya Ghana. Jina la mmoja wa wachezaji wa Ghana lilikuwa na maana ingine kwa Kiswahili, na ambayo ingeweza kuleta taharuki. Mtangazaji hakulitaja kabisa jina hilo pamoja na mchezaji huyo kutawala sehemu kubwa ya mchezo.
“Kupiga kula” ni neno lenye maana ya “kupiga msosi” au kupiga menyu katika lugha yetu ya mtaani. Ukilipeleka kwenye uchaguzi, linaonesha mpigakura anakwenda kuhongwa. Mbaya zaidi ukisema “wagombea wanaomba kula”, hapo ndio unamaanisha wagombea wanatafuta nafasi ya kwenda kufilisi uchumi wa nchi. Ngoja nikupe athari za lugha pale maneno yanapopishana.
Kwenye nchi fulani huko ughaibuni, mwanasiasa mmoja kutoka kambi ya upinzani alikamatwa na kuwekwa kizuizini. Kiongozi wa nchi kwa kuhofia machafuko, akapeleka ujumbe mfupi kwa Mkuu wa Usalama ulioandikwa: “Kill him not, let him live”. Kwa tafsiri nyepesi ujumbe ulimaanisha: “Usimuue, mwache aishi”. Lakini aliyepeleka ujumbe ule alikuwa mnazi wa utawala. Akabadili nafasi ya alama ya mkato tu, na ujumbe ukasomeka: “Kill him, not let him live”, yaani “Muue, usimwache aishi”!
Lakini yote kwa yote nawatakia uchaguzi mwema. Sote tuzingatie Sheria ya Uchaguzi tuliyoelekezwa na Tume, tupige kura (sio kula) kwa wa amani na utulivu tukiidumisha tunu hii tuliyoachiwa na waasisi wetu.