
Dar es Salaam. Klabu ya Yanga imemtambulisha, Pedro Goncalves kuwa Kocha Mkuu wa kikosi hicho akichukua mikoba ya Roman Folz ambaye alitimuliwa.
Goncalves ametambulishwa usiku wa leo Oktoba 25, 2025 ikiwa saa chache baada ya Yanga kutinga hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika ikiichapa Silver Strikers mabao 2-0.
Mbali na kocha huyo pia Yanga tayari imemalizana na makocha wengine wawili ambao muda wowote kuanzia sasa watatambulishwa ndani ya timu hiyo ambao ni kocha msaidizi na kocha wa makipa.
Mwananchi limepenyezewa jina la kocha huyo msaidizi ambaye ni Filipe Pedro huku kocha wa makipa akiwa ni Fernando Perreira.
Pedro raia wa Ureno, anajiunga na Yanga akiwa na rekodi ya kuifikisha Angola hatua ya robo fainali kwenye Afcon iliyopita.
Pia aliiongoza Angola katika michuano ya CHAN 2024 iliyofanyika mwaka 2025 nchi za Tanzania, Kenya na Uganda.
Hersi katika mazungumzo yake baada ya leo Yanga kufuzu hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika kwa kuitandika, amesema wanashusha kocha mwenye rekodi ya kuipeleka timu hatua ya robo fainali.
“Tunatambulisha kocha mwenye ubora mkubwa, mwenye uzoefu mkubwa, kocha atakayetuvusha kwenye mashindano haya hadi hatua inayofuata,” amesema Hersi