SIKU moja baada ya Azam FC kutinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwake, waliokuwa mastaa wa timu hiyo wamewapongeza wachezaji, benchi la ufundi na uongozi huku wakiamini kuwa nafasi ya kutwaa kombe wanayo wakiendeleza vyema mapambano.

Azam FC jana imetinga hatua hiyo baada ya kuifunga KMKM kwa jumla ya mabao 9-0 kwenye mechi mbili za Kombe la Shirikisho Afrika na kuandika rekodi ya kutinga hatua hiyo baada ya miaka 21 tangu kuanzishwa kwa klabu hiyo.

Kiungo mshambuliaji wa zamani wa Azam FC ambaye kwa sasa anacheza MC Alger ya Algeria, Kipre Jr alitumia nafasi hiyo kuupongeza uongozi wa klabu hiyo kwa uwekezaji mkubwa, wachezaji kwa kupambania nembo na timu na benchi la ufundi kwa mbinu sahihi ilizoipa nafasi timu hiyo kufikia malengo.

KIP 01

“Lilikuwa ni suala la muda kwa timu hiyo kufikia mafanikio hayo baada ya kujaribu mara kwa mara sasa ni muda wa kufurahi na kuongeza nguvu kwenye uwekezaji ili kufikia mafanikio makubwa zaidi michuano ya kimataifa,” amesema na kuongeza:

“Wachezaji, viongozi na benchi la ufundi wamepata walichokuwa wanastahili, kikosi kina ukomavu mkubwa wa michuano baada ya kujaribu mara nyingi, walipo sasa sio sehemu ya kuridhika na matokeo wana nafasi ya kufika mbali zaidi waendelee kupambana.”

Kiungo wa zamani wa timu hiyo ambaye kwa sasa anakipiga ES Setif ya nchini Tunisia, Gibril Sillah amesema amefurahishwa na mafanikio ya Azam FC, anawatakia kila la kheri katika mapambano yaliyo mbele yao huku akiweka wazi kuwa anatamani kuona wakitwaa taji hilo.

KIP 02

“Haikuwa rahisi, wamepambana sana juhudi na mikakati thabiti imewafikisha hapo walipo, sasa natamani kuona wanasonga zaidi na hatimaye kutwaa taji la michuano hiyo, naamini inawezekana kwani wana kikosi bora,” amesema.

“Ndoto imetimia ni misimu mingi licha ya uwekezaji mkubwa tulijaribu na mimi nikiwepo mambo hayakwenda kama tulivyopanga walichokifanya sasa ni kikubwa hongera kwa benchi la ufundi, wachezaji na viongozi kwa kuto kuikatia tamaa timu umoja na furaha waliyonayo sasa wafiendeleze ili waweze kufika mbali zaidi hadi kutwaa taji.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *