NI miaka 24 sasa tangu Small Simba ya Zanzibar ipotee katika ramani ya soka la kiushindani, ambapo timu hiyo yenye rekodi na mafanikio makubwa ilianzishwa mtaani ikijulikana kwa jina la ‘Sunderland’, kisha baadaye kubadilishwa.

Timu hiyo ilipiga hatua zaidi miaka ya 1970–1980, ambapo mwaka 1977, timu hiyo ilishiriki Ligi Daraja la Pili na ikapata nafasi ya kupanda Ligi Kuu ya Zanzibar, ingawa hadi sasa imetimiza miaka 24, tangu iliposhuka daraja rasmi mwaka 2001.

Kutokana na historia kubwa ya timu hiyo iliyoipata kwa miaka ya nyuma, Mwanaspoti liliweka kambi visiwani Zanzibar na kuzungumza na aliyekuwa mchezaji na kocha wa kikosi hicho, Masoud Salum Masoud, aliyefunguka mambo mengi yaliyoiangusha.

SMAL 01

UBABAISHAJI WA VIONGOZI

Masoud anasema kati ya sababu kubwa zilizochangia timu hiyo kupotea katika ramani ya soka ni kutokana na baadhi ya watu wasioitakia mema kuingia na kuutoa uongozi uliokuwapo kipindi hicho chini ya muasisi wa kikosi hicho, Abdulghan Msoma.

“Msoma hakuwa muasisi tu bali alikuwa kiongozi na kocha ila walimfukuza kipindi kile kwa ajili ya maslahi yao binafsi, ingawa ni mtu aliyekuwa na mapenzi mema na timu na hata ukizungumza naye unaona inamuumiza,” anasema Masoud na kuongeza;

“Nakumbuka ilikuwa mwaka 1996, wakati ambao Msoma alifukuzwa tena na watu ambao aliwakaribisha mwenyewe na kitu ambacho aliwaambia kama mimi (Msoma) na Masoud ndio waanzilishi wa hii timu na mnatufukuza kwa sababu ya pesa, klabu haitafika popote.”

Masoud anasema mbali na baadhi ya watu kumuondoa Msoma, sababu nyingine iliyochangia kikosi hicho kushuka daraja na kupotea katika ramani ya soka ni kutokana na uchumi mdogo wa uendeshaji, ambao kwa kipindi hicho ulikuwa ni changamoto.

UDUGU NA SIMBA

Anasema mwaka 1969 klabu ya Kikwajuni ilitembelewa na Mwenyekiti wa Sunderland kwa sasa Simba ya Dar es Salaam, ambapo kiongozi huyo aliyemtaja kwa jina la Chimwaga aliwakuta vijana wadogo wakicheza na kupendekeza waitwe, Small Sunderland.

“Kipindi hicho Kikwajuni na Sunderland kwa sasa Simba zilikuwa na undugu wa kisoka na hata baadhi ya wachezaji wetu kwa wakati huo walikuwa wanaipenda, urafiki wetu ukaanzia hapo ingawa ni timu mbili tofauti na watu wanavyozichukulia sasa.”

Masoud anasema hata baada ya Simba kubadilisha jina kutoka Sunderland, ndivyo ambavyo nao pia waliamua kubadili na kujiita Small Simba.

SMAL 02

YANGA YAIPA MAUJANJA

Anasema wakati kikosi hicho kilipokuja jijini Dar es Salaam kutembelea Redio Tanzania kwa wakati huo, walipata nafasi ya kucheza mechi ya kirafiki na Yanga na kupoteza bao 1-0, la Charles Albert, hivyo kuanzia hapo ndipo wakapewa maujanja.

“Wakati tuko daraja la chini tulikuwa tunajichanganya na wachezaji mbalimbali ila baada ya mechi yetu na Yanga kuisha tu, wakatuambia mbona mna timu nzuri sana sasa kwa nini msicheze wenyewe, kuanzia hapo tukachukua ushauri wao,” anasema.

Masoud aliyewahi kuzifundisha pia timu mbalimbali zikiwemo za African Sports na Coastal Union za Tanga na FC Arusha, anasema hata kwa sasa Yanga ni kati ya klabu bora zilizofanikiwa zaidi katika Ukanda wa Afrika Mashariki na Kati.

“Sababu kubwa ya kufanikiwa kwao ni uongozi imara, wamejipanga na hata ukiangalia mambo yao wanayofanya unaona kabisa ni timu itakayofika mbali zaidi, tofauti na kwa wapinzani wao wakubwa hapa nchini Simba wanaoendelea kujitafuta taratibu.”

MECHI ASIZOZISAHAU

Licha ya kucheza na kufundisha soka ndani na nje ya nchi, Masoud anasema kati ya mechi ambazo hatokaa azisahau katika maisha yake yote ni wakati akikichezea kikosi cha Kikwajuni na ilikuwa ni kila walipokutana na timu ya Miembeni.

“Kikwajuni na Miembeni ni timu zilizokuwa na ushindani mkubwa sana kipindi hicho, watu wa Zanzibar wanatamani kuziona tena zikirudi katika mstari kama ilivyokuwa Small Simba, kiukweli tunakosa ile ladha halisi ya soka,” anasema Masoud.

Anasema mbali na timu hizo, hata alipokuwa anakutana na Sigara kipindi ambacho aliichezea African Sports na Coastal Union, zilikuwa pia mechi ngumu na za ushindani mkubwa, kutokana na aina ya wachezaji wakubwa waliokuwapo wakati huo.

SMAL 03

URAFIKI NA KAYUNI, SIMKOKO

Masoud anasema miongoni mwa watu anaojivunia kufanya nao kazi katika sehemu mbalimbali ni makocha, Sunday Kayuni na John Simkoko, ambao katika soka la Tanzania wameweka rekodi nzuri ambazo zitaendelea kuishi na kukumbukwa na vizazi vijavyo.

“Unapotaja makocha kama Kayuni na Simkoko unanikumbusha mbali sana kwa sababu licha ya kucheza nao wakiwa timu tofauti ila nimesoma nao kozi ya ukocha pamoja, ni watu wanaojua wanapaswa kufanya nini na kwa wakati gani pia,” anasema Masoud.

MIKAKATI NA RAIS WA ZFF

Anasema Rais wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Zanzibar (ZFF), Suleiman Mahmoud Jabir, alikuwa mchezaji wa Small Simba na sasa kuna mikakati bora inaundwa kwa ajili ya kuhakikisha kikosi hicho kinarudi tena katika ramani ya soka kama mwanzo.

“Tunachohitaji ni kuona tunarejesha tena heshima iliyokuwapo miaka ya nyuma, kwa sasa Jabir tunatambua anauguliwa sana na baba yake, lakini tunapambana kuhakikisha tunashirikiana naye ili tuweze kufanikisha malengo tuliyojiwekea,” anasema.

MAKOMBE YALIANZIA HAPA

Masoud anasema mwaka 1975 aliungana na Abdulghan Msoma kuwafundisha vijana na mwaka mmoja baadaye ilianzishwa Ligi ya vijana ambao hadi sasa timu hiyo inashiriki, ikipambana kujitafuta upya ili kurejea katika makali yake iliyojizoelea.

“Mwaka 1977, ilibadilishwa jina na kuitwa Central Ligi, ambayo hadi sasa tunashiriki tukianzia kwa vijana, ilisimamiwa kwa karibu na Maalim Rajabu tukishirikiana na Msoma, Hafidh Badru na wengine waliokuwepo kikosini hapo,” anasema Masoud.

Anasema mwaka 1981, timu hiyo iliingia Daraja la Pili ikitokea Central, kisha ikachukua ubingwa na mwaka 1983 ikaingia Daraja la Kwanza na kutwaa ubingwa Zanzibar, kisha kuibuka mbabe kwenye michuano ya Super League kwa kuifunga Yanga bao 1-0.

“Unapoielezea Small Simba ni timu yenye historia kubwa sana katika soka la Zanzibar, hii Mlandege, KMKM ambazo kwa sasa ndizo zenye mashabiki wengi ukiwauliza hata viongozi wao watakuelezea kipindi hicho tulikuwa ni wa aina gani,” anasema.

SMAL 04

WAZAWA WANAJITAMBUA

Anasema katika kipindi ambacho alikuwa anacheza wachezaji wengi wazawa walikuwa wanafanikiwa zaidi kutokana na kucheza kwa malengo hasa ya kujitambua, licha ya ukweli walikuwa wanacheza katika mazingira ya kujitolea tofauti na ilivyo sasa.

“Kipindi chetu tulikuwa tunacheza kwa kujitolea sana kwa maana hata fedha tulizokuwa tunapata ni tofauti na wachezaji wa sasa wanazozipata, jambo la kusikitisha wakati huu ambao ni mzuri zaidi ila wamezidi kubweteka na mafanikio yao madogo.”

Masoud anasema hashangazwi kuona idadi kubwa ya wachezaji wa kigeni wakiingia hapa nchini, kwa sababu wanachangia kiasi kikubwa kuongeza ushindani kwa wazawa, kwani hata ligi zilizoendelea ikiwamo ya England (EPL) wengi wao wanatoka nchi nyingine.

ANGUKO LILIPOANZIA

Anasema mwaka 1997 hadi 1998, timu hiyo ilipambana katika Ligi ya Zanzibar, ila ilishindwa kurudi kwenye kasi ya mwanzo na kuanza kuporomoka polepole hadi sasa haipo tena, jambo ambalo linamuumiza kila uchao kutokana na historia iliyopo.

“Tuna wachezaji kutoka Bara na visiwani tuliowaweka katika akademia ya Small Simba kwa lengo la kuendeleza vipaji vyao, Serikali ya Zanzibar imetusaidia kuboresha viwanja vya Gombani (Pemba), New Amaan Complex na Mao Tse Tung vya Unguja.”

Masoud anasema maboresho makubwa ya viwanja hivyo yamesaidia sana kuwapa motisha ya kupata sehemu mbalimbali za kufanyia mazoezi na kuwaweka wachezaji katika mazingira rafiki, jambo ambalo wao kama viongozi na benchi la ufundi wanajivunia.

BARA WAMEPIGA HATUA

Masoud aliyefundisha pia timu ya taifa ya Zanzibar na Tanzania ya vijana chini ya umri wa miaka 23, anasema Ligi ya Bara imepiga hatua kubwa zaidi kutokana na ufadhili wa taasisi mbalimbali zilizowekeza, tofauti na visiwani Zanzibar ambazo ni chache sana.

“Kwa sasa jitihada tunaziona kwa maana ya Serikali yetu ya Bara na visiwani zinapopambana kukuza soka la nchi yetu kwa miaka ya hivi karibuni, kuna mwanga unaonekana huko mbele, japo juhudi zaidi zinahitajika hususani kwa hapa Zanzibar.”

KUREJESHA MASHABIKI

Anasema licha ya mashabiki wengi wa Small Simba kuhamia timu mbalimbali kutokana na kikosi hicho kupotea katika ramani ya soka, bado wana matumaini makubwa ya kuendelea kupambana kuhakikisha waliopo wanaendelea kutoa sapoti ya kutosha.

“Miaka 24 ni mingi sana na kiukweli ni rahisi kupoteza mashabiki kwa sababu hawana tena timu ya kuishangilia, natambua ni kazi kubwa kuwapata kama ilivyokuwa mwanzoni, ingawa tutakaporejea katika ramani ya soka walioondoka watarudi na tutapata wengine wapya.”

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *