
Moshi. Msimamizi wa Uchaguzi wa Majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo, mkoani Kilimanjaro, Lucas Msele amewataka makarani waongozaji wapiga kura kuhakikisha wanatekeleza majukumu yao kwa weledi, uadilifu na kufuata taratibu zote za uchaguzi ili kuepuka malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa.
Akizungumza leo Oktoba 25, 2025 wakati akifungua mafunzo kwa makarani hao katika ukumbi wa CCP Moshi, Msele pia amewataka washiriki hao kushirikiana kwa karibu na mawakala wa vyama vya siasa watakaokuwepo vituoni kwa mujibu wa sheria.
“Jitahidini mjiepushe kuwa chanzo cha malalamiko kutoka kwa vyama vya siasa. Fanyeni kazi kwa ushirikiano, uadilifu na kwa kuzingatia kanuni, sheria na maelekezo yote yaliyotolewa na Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi,” amesema Msele.
Amesisitiza umuhimu wa makarani hao kusoma kwa umakini Katiba, sheria, kanuni, miongozo na maelekezo mbalimbali yaliyotolewa na yatakayotolewa na Tume ili waweze kutekeleza majukumu yao kwa ufanisi.
“Mkipata jambo lisiloeleweka, ulizeni mapema ili mpate kufafanuliwa. Mmepewa nyaraka muhimu, zitumieni kama rejea wakati wote wa utekelezaji wa jukumu hili,” ameongeza.
Aidha, amewataka makarani hao kuhakiki na kukagua vifaa vyote vya uchaguzi watakavyokabidhiwa kabla ya kuelekea vituoni, pamoja na kuhakikisha wanafika mapema ili kukamilisha maandalizi ya vituo kabla ya muda wa upigaji kura kuanza.
Msele pia amewakumbusha makarani hao kuonyesha unadhifu, kutumia lugha nzuri na kuwapa kipaumbele wapiga kura wenye mahitaji maalumu watakapofika vituoni
“Ninyi ndio watendaji mnaokutana moja kwa moja na wapiga kura, hivyo ni wajibu wenu kuhakikisha mnaweka taswira nzuri ya uchaguzi,” amesisitiza.
Mafunzo hayo yanawahusisha makarani 929 watakaosimamia shughuli za uchaguzi katika vituo 865 vilivyopo katika kata 32 za majimbo ya Moshi Vijijini na Vunjo.
Msimamizi Msaidizi wa Uchaguzi wa Jimbo la Moshi Vijijini, Josamu Kengia, amesema kuwa kwa upande wa jimbo hilo kuna jumla ya vituo 437 vya kupigia kura, ambavyo vitatumika katika uchaguzi mkuu oktoba 29, 2025.
Ameeleza kuwa kwa ajili ya kuhakikisha uchaguzi unafanyika kwa ufanisi, makarani waongozaji wapiga kura wanapatiwa mafunzo maalum ya kuwajengea uelewa juu ya majukumu yao na namna ya kusimamia taratibu zote za uchaguzi kwa mujibu wa sheria na miongozo ya Tume Huru ya Taifa ya Uchaguzi (INEC).