Kitendo cha Linnie kumfanyia mpango wa kuishi Sweden kilikuwa ni ushindi mkubwa katika maisha ya Muddy, kuliko hata kushinda shindano kubwa la bahati nasibu.
Kubwa alilokuwa akilitaka lilikuwa ni kupata maisha ya Ulaya; hakujali ni nchi gani, alimradi tu asirudi Tanzania. Kwake, haikuwa lazima aende Uholanzi, kwani hata Sweden angeweza kujipanga na kutafuta maisha ili kufanikisha kile alichokuwa akikidhamiria.

Kwa dhati kabisa kutoka moyoni mwake, Muddy alimshukuru Linnie kwa kumwamini na kumpa nafasi ya kuanza maisha mapya Sweden. Aliapa kuitumia fursa hiyo kuleta manufaa kwa jamii na kujenga maisha yenye matumaini.

Pamoja na kupewa kibali cha kuishi Sweden, bado Muddy alionekana kutokuamini kilichokuwa kimemtokea. Mara kwa mara alikuwa akimgeukia Linnie na kumshukuru kwa kile alichokifanya. Aliona huo ulikuwa ni uungwana wa hali ya juu ambao hakuwahi kufanyiwa katika maisha yake.
Aliamini hakuwa amekosea kumwamini mwanamke huyo wa kizungu, kama vile hisia zake zilivyomwelekeza tangu walipokutana na kuzungumza kwa mara ya kwanza.

Kitendo cha Linnie kilimfanya Muddy awe na uhakika wa kubaki Ulaya na kuepukana na kifungo ambacho kingemkabili endapo angerudishwa Tanzania.
Alijihisi kana kwamba hata ile ndoto aliyoiota akiwa gerezani, moja ya magereza ya Tanzania, ilikuwa tu ni ndoto nyingine kama zile alizokuwa akiota akiwa nyumbani.
Hakutaka tena kukumbuka kesi yake ya kumuibia pesa na mali raia wa Kongo, Kamba Makambo.

Muddy aliamini kesi hiyo ilikuwa imekufa kifo cha kibudu kutokana na kitendo cha Linnie kumpatia kibali cha kuishi Sweden.
Kibali hicho cha miezi mitatu kingewafanya polisi wa Tanzania watafute kazi nyingine, si kumtafuta tena yeye.

“Na sitakaa miezi mitatu,” aliwaza Muddy. “Nikimaliza miaka mitano ndipo nitafikiria kurudi Tanzania. Nani atakayekumbuka kesi yangu?”

Linnie alikuwa akiishi peke yake katika nyumba iliyoko nje kidogo ya Jiji la Stockholm, kwenye mji mdogo uitwao Sigtuna, umbali wa takribani kilomita hamsini kutoka mji mkuu.
Alianza maisha hayo ya upweke baada ya kuachana na mwanaume aliyekuwa akiishi naye bila ndoa.

Mara baada ya kutoka uwanja wa ndege, Linnie na Muddy walipanda treni iliyowapeleka hadi Sigtuna.
Hivyo ndivyo Muddy alivyobaki Sweden na kuanza maisha mapya nyumbani kwa Linnie, akiwa na shukrani isiyo na kifani.

Linnie alimkaribisha Muddy kwa upendo mkubwa nyumbani kwake na kumpa chumba kilichokuwa na kila kitu ndani yake. Wawili hao walikubaliana kila mmoja kuhifadhi faragha yake kwa kulala vyumba tofauti.

Muddy alikuwa mgeni kwa kila kitu; utamaduni, mazingira, na hata hali ya hewa. Hakuwa amewahi kuona milima ya barafu, lakini taratibu alianza kuizoea.
Linnie alimsaidia kupata mafunzo ya lugha ya Kiswidi na Kiingereza cha ufasaha, pamoja na kumfundisha mfumo wa maisha nchini Sweden.

Wakati mwingi Linnie alipokuwa kazini, Muddy alikuwa akibaki nyumbani akisaidia kazi mbalimbali. Mbali na kusafisha nyumba, alijitahidi pia kupika. Hapo ndipo alipomwonyesha Linnie ufundi wa vyakula vya Kiswahili — akamfundisha kula ugali na vyakula vingine vya asili ya Tanzania.
Kwa upande wake, Linnie alimfundisha Muddy kupika vyakula vya Kiswidi alivyovipenda.

Ndani ya nyumba kulikuwa na vifaa vya mazoezi, ambavyo Muddy alivitumika kikamilifu kuujenga mwili wake.

Miezi mitatu ya kuishi pamoja ilitosha kuimarisha uhusiano wao. Wote wawili walizidi kuwa karibu, wakijifunza tabia na hulka za kila mmoja. Hatimaye waligundua kuwa walikuwa na mengi ya kushirikiana.

Linnie alimuongezea Muddy kibali cha kuishi Sweden, safari hii akiwaombea kibali cha muda mrefu zaidi.
Pia alimsaidia kupata kazi ya udereva katika kampuni moja ya usafi jijini Stockholm, baada ya Muddy kuhudhuria mafunzo mapya ya udereva na kupewa leseni inayotambulika kote Ulaya.

Maisha yao yaliendelea vizuri. Wote sasa walikuwa wakitoka asubuhi na kurudi usiku. Linnie ndiye aliyekuwa akiwahi kurudi, hivyo mara nyingi ndiye aliyekuwa akipika au kubeba chakula kutoka mgahawani.

Walikuwa na bajeti ya pamoja ya matumizi ya mwezi mzima, ambayo wote walichangia.
Siku za wikendi hawakwenda kazini; walitumia muda huo kufanya usafi, kufua nguo kwa mashine, na kupamba mazingira ya nyumba yao.
Baada ya chakula cha jioni, walipenda kuketi pamoja sebuleni kuangalia runinga — michezo ya mpira, au filamu walizozipenda wote.

Baada ya burudani, walipendelea kuzungumza mambo mbalimbali yahusuyo maisha kwa ujumla.
Hata hivyo, kipindi hicho kilikuwa kigumu kwao kufichua hisia zao za mapenzi zilizokuwa zikikua kwa kasi mioyoni mwao.
Kila walipoamua kwenda kulala vyumbani mwao, ilikuwa kama walikuwa wakifanya hivyo kwa shingo upande — kila mmoja akitamani mazungumzo yaendelee, au la, walale chumba kimoja.

Hisia zao zilikuwa dhahiri; macho na mioyo yao vilizungumza zaidi ya maneno, lakini hakuna aliyekuwa na ujasiri wa “kumfunga paka kengele.”

Siku moja walikuwa wameketi sebuleni wakitazama filamu ya mapenzi. Nje kulikuwa na baridi kali, hivyo walikaa karibu zaidi huku moto ukichoma taratibu kwenye jiko maalum la ndani.

Katika mazungumzo yao, Muddy alimwambia Linnie:

“You are an important person in my life… (Wewe ni mtu muhimu katika maisha yangu…)”

Linnie alitabasamu, akamjibu:

“And you too… I’m glad to know you. You made me believe life can be beautiful once again. (Na wewe pia… Nimefurahi kukufahamu. Umenifanya niamini maisha yanaweza kuwa mazuri kwa mara nyingine tena.)”

Muddy aliendelea kwa sauti ya utulivu:

“I don’t think you realize how much you’ve changed my life. (Nadhani hufahamu ni kwa kiasi gani umeyabadilisha maisha yangu…)”

Linnie akajibu kwa upole, macho yake yakiangaza:

“Even my life was dominated by loneliness, you have changed it to a very large extent. (Hata mimi maisha yangu yalikuwa yametawaliwa na upweke, wewe umeyabadili kwa asilimia kubwa sana.)”

Baada ya maneno hayo, waligeukiana — macho yao yakagongana na kuzungumza zaidi ya maneno. Walizidi kusogea karibu, wakivutwa na nguvu ya kimya isiyoelezeka.

“I don’t like to lie in my life… (Huwa sipendi kusema uongo katika maisha yangu…)”
alisema Linnie kwa sauti ndogo, huku akimwangalia Muddy kwa macho ya upendo.

“And I don’t like to hide my feelings the way they send me. (Na huwa sipendi kuficha hisia zangu jinsi zinavyonituma…),”
aliongeza akizungumza kwa sauti ya chini, lakini yenye uzito wa hisia.

“I would like to tell you clearly that I happened to love you from the first day… (Napenda kukuambia wazi kwamba nilitokea kukupenda tangu siku ya kwanza…),”
aliongeza Linnie, akifichua siri ya moyo wake.

“It’s true… (Ni kweli…),”
Muddy alimjibu taratibu, macho yake yakikazia yale ya Linnie, akiamini maneno hayo yalikuwa ni uthibitisho wa hisia ambazo naye alikuwa nazo tangu siku walipokutana katika Uwanja wa Ndege wa Arlanda.

Walitazamana bila kupepesa macho. Hisia zilipanda kilele, joto la mapenzi likazidi kuwatamalaki.
Walisogeleana zaidi, miili yao ikagusana. Kisha Muddy akasogeza uso wake karibu na ule wa Linnie, akafungua kinywa chake taratibu.
Linnie naye akajibu mwito huo; ndimi zao zikakutana kwa mara ya kwanza, zikawa ndimi za mapenzi.
Wakarudia kitendo hicho mara kadhaa, kisha wakakumbatiana, mikono yao ikianza safari ya kugusa na kuhisi miili ya kila mmoja — joto la upendo likazidi kushamiri.
Inaendelea…

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *