PRESHA kubwa ya Yanga ilikuwa Uwanja wa Benjamin Mkapa jijini Dar es Salaam kusaka tiketi ya kutua makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Silver Strikers, lakini kocha wao Mzungu ametua mjini Morogoro kwa mambo mengine.

Kocha aliyetua Morogoro ni Paul Mathew ambaye ni Mkurugenzi wa Ufundi wa Yanga, ameanza ziara ya mikoani akitafuta mastaa wapya wa baadaye kwa kikosi chao.

Mathew ambaye ni jina kubwa nchini Afrika Kusini kwa uvumbuzi wa vipaji, katikati ya wiki hii alikuwa na ziara ya kutembelea vituo vya soka mkoani humo kikiwemo cha Moro Kids.

Mathew ambaye ameambatana na mratibu wa timu za vijana za Yanga, Imani Karume, akiwa ndani ya kituo hicho Mwanaspoti linafahamu kwamba ameondoka na majina kadhaa ya wachezaji kwa lengo la kwenda kuongezwa kwenye vikosi vya vijana.

MZU 01

Awali kabla ya ujio wa Mathew ndani ya Moro Kids, Yanga iliingia mkataba na kituo hicho kwa lengo la kuchukua wachezaji vijana.

Akizungumzia ujio huo wa Mathew, Katibu Mkuu wa Moro Kids, Michael Kwembe amethibitisha ujio wa mkurugenzi huyo wa ufundi akisema ziara hiyo itawanufaisha wachezaji hao vijana ambao wanatamani kufanya makubwa.

MZU 04

“Nikweli tulikuwa na ugeni huo wa kutoka Yanga, walikuja watu wawili Mkurugenzi wa ufundi Mathew (Paul) na mratibu wa vijana Imani Karume,” amesema Kwembe.

MZU 02

“Ujio wao ulikuwa maalum kuangalia vijana kuanzia miaka 20 kushuka chini, ambao watavutiwa na vipaji vyao na kwenda kuwaongeza kwenye timu za vijana za Yanga.

“Sisi kama Moro Kids kwanza tumeishukuru Yanga kwa kutuletea mtu muhimu kama huyu kwa maendeleo ya soka kwenye timu kuja hapa lakini pia hata mkurugenzi wetu wa kituo Profesa Madundo Mtambo ameona namna ushirikiano baina ya taasisi hizi mbili unavyoendelea vizuri.”

MZU 03

Moro Kids ndio kituo ambacho kimewakuza mastaa baadhi wa Yanga wakiwemo Dikson Job, Kibwana Shomari na kipa Aboutwalib Mshery.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *