
Dar es Salaam. Refa Adissa Ligali kutoka Benin ndiye amepangwa kuchezesha mechi ya marudiano ya Ligi ya Mabingwa Afrika baina ya Yanga na Silver Strikers ya Malawi kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, leo.
Mchezo huo umepangwa kuanza saa 11:00 jioni kwa muda wa Afrika Mashariki.
Ligali katika mechi 12 za mashindano ya CAF, ametoa idadi ya kadi za njano 49 ikiwa ni wastani wa kadi nne (4) kwa kila mchezo.
Refa huyo ambaye ana umri wa miaka 39, alipata rasmi beji ya kimataifa ya Shirikisho la Mpira wa Miguu Duniani (FIFA) kwa mara ya kwanza mwaka 2016.
Katika mchezo wa leo atasaidiwa na refa msaidizi namba moja Lucien Hontonnou kutoka Benin na Lamine Adolphe wa Burkina Faso na refa wa mezani ni Dedjinnanchi Ahomlanto kutoka Benin.
Aliyepangwa kuwa Kamishina wa mchezo huo ni Ahmed Bowud kutoka Mauritius na Mtathimini wa marefa ni Andriamparany Rakotoarimanana kutoka Madagascar.
Katika mchezo huo ambaoutachezwa kwenye Uwanja wa Benjamin Mkapa, Yanga inahitajika kupata ushindi wa tofauti ya mabao mavili au zaidi ili iweze kutinga hatua ya makundi kwa vile ilifungwa bao 1-0 katika mchezo wa kwanza uliofanyika nchini Malawi wiki iliyopita.