Raia wa Ivory Coast wapiga kura kumchagua rais mpyaRaia wa Ivory Coast wapiga kura kumchagua rais mpya

Idadi ya wapiga kura watakaojitokeza Jumamosi itakuwa muhimu kwenye uchaguzi huu. Takriban watu milioni tisa wanastahiki kupiga kura katika uchaguzi huu, ambao vituo vya kupigia kura vinatarajiwa kufungwa saa 12 jioni saa za Afrika magharibi, wakichagua kati ya wagombea watano, akiwemo rais wa sasa Alassane Ouattara, anayetarajia kuepuka duru ya pili ya uchaguzi.

“Maisha ya taifa yanategemea kupiga kura, hiyo ndiyo sababu yangu pekee ya kushiriki,” alisema Ibrahim Diakite, dereva wa basi aliyekuwa akipiga kura katika kitongoji kinachomuunga mkono Ouattara mjini Abidjan, alipoongea na shirika la habari la Ufaransa AFP.

Lakini wapinzani wakuu wa Ouattara — rais wa zamani Laurent Gbagbo na aliyekuwa Mkurugenzi Mtendaji wa benki ya Uswisi , Credit Suisse, Tidjane Thiam — wamezuiwa kugombea; wa kwanza kutokana na hukumu ya jinai, na wa pili kwa sababu ya kupata uraia wa Ufaransa.

Kwa kuwa upinzani umeitisha maandamano na machafuko kuongezeka katika siku za hivi karibuni, serikali imeweka marufuku ya kutotoka nje usiku katika baadhi ya maeneo na kupeleka mitaani vikosi vya usalama 44,000.

Wapiga kura waliozungumza na shirika la habari la Ufaransa AFP walionekana kuwa na matumaini.

“Katika miaka iliyopita, kulikuwa na mvutano zaidi kuliko mwaka huu,” alisema Mamadou Bamba, mwanamume asiye na ajira mwenye umri wa miaka hamsini huko Abobo, alipoongea na AFP. “Leo tunapiga kura kwa amani. Tumaini letu ni kwamba siku hii ipite bila tukio lolote,” alisema Severine Kouakou, mpiga kura mwenye umri wa miaka 46 huko Bouake, jiji la pili kwa ukubwa nchini.

“Ni vigumu kutarajia mshangao wowote mwishoni mwa uchaguzi huu… kwa kuwa vigogo wa upinzani hawapo,” alisema Gilles Yabi kutoka taasisi ya tafiti ya Wathi alipoongea na AFP.

Kupigwa marufuku mikutano ya kisiasa

Waandamani wakiomba kutokuwa na muhula wa nne kwa rais Ouattara
Mikutano ya hadhara ilipigwa marufuku kwa hofu ya ghasiaPicha: Getty Images/AFP/I. Sanogo

Watu wanne, akiwemo polisi mmoja, wamefariki katika machafuko ya kisiasa ya hapa na pale katika wiki za hivi karibuni, huku Jumatatu jengo la tume huru ya uchaguzi likichomwa moto. Serikali imejibu kwa kupiga marufuku maandamano, na mahakama imewahukumu watu kadhaa kifungo cha miaka mitatu jela kwa kuvuruga amani.

Vikosi vya usalama vimepelekwa kote katika nchi hiyo yenye watu milioni 30 ili kudhibiti maandamano, hasa katika ngome za zamani za upinzani kusini na magharibi. Marufuku ya kutotoka nje usiku ilikuwa ikitekelezwa Ijumaa na Jumamosi katika eneo la Yamoussoukro, ambako ndiko mji mkuu wa kisiasa ulipo. Mamlaka zinasema zinataka kuepuka “vurugu” na kurudia machafuko ya uchaguzi wa urais wa mwaka 2020, ambapo watu 85 walipoteza maisha.

“Nawaomba mfuatilie kwa karibu maeneo yenu… Lazima tuwe tayari kuilinda Côte d’Ivoire,” alisema Ouattara katika mkutano wake wa mwisho wa kampeni Alhamisi. “Uchaguzi huu unatisha, lakini tunathubutu kuamini kutakuwa na hofu zaidi kuliko madhara,” alisema Ibrahime Kuibiert Coulibaly, mkuu wa Tume Huru ya Uchaguzi.

Jumatano, Laurent Gbagbo alilaani uchaguzi huo akisema ni “mapinduzi ya kikatiba” na “wizi wa uchaguzi.” “Wale ambao wangeweza kushinda wameondolewa. Sikubaliani na hili,” alisema bila kutoa maelekezo ya wazi kwa wafuasi wake kuhusu kura ya Jumamosi.

Wagombea wanne wa upinzani

Bi Simone Gbagbo mgombea urais
Mke wa rais wa zamani Simone Gbagbo alifanya mkutano wake wa mwisho katika eneo la Aboisso, mashariki mwa nchi hiyo huku Waziri wa zamani wa Biashara Jean-Louis Billon naye akifanya kampeni zake za mwisho huko Bouake, katikati mwa nchiPicha: Joseph Zahui/Matrix Images/IMAGO

Hakuna kati ya wagombea wanne wapinzani anayeiwakilisha chama kilichoimarika, wala hawana mtandao mpana kama chama tawala cha RHDP. Waziri wa zamani wa biashara na mfanyabiashara wa kilimo Jean-Louis Billon, mwenye umri wa miaka 60, anatumaini kuvutia wafuasi kutoka chama chake cha zamani, Chama cha Kidemokrasia.

Mke wa zamani wa rais, Simone Ehivet Gbagbo, mwenye umri wa miaka 76, anatafuta kura kutoka kwa wafuasi wa mume wake wa zamani.

Kura za mrengo wa kushoto zinaning’inia kati ya Simone Gbagbo na Ahoua Don Mello, mhandisi wa ujenzi na mwanaharakati huru wa Uafrika.

Kisha kuna Henriette Lagou, mgombea wa wastani ambaye pia aligombea katika uchaguzi wa urais wa mwaka 2015, akipata chini ya asilimia moja ya kura. Ouattara alichukua madaraka kufuatia mvutano wa uchaguzi wa urais wa 2010-2011 kati yake na Gbagbo, ambao ulisababisha vifo vya zaidi ya watu 3,000 miongoni mwa wafuasi wao.

Kuwa polisi ni mwiba Ivory Coast

To view this video please enable JavaScript, and consider upgrading to a web browser that supports HTML5 video

Serikali inaonyesha miaka kadhaa ya ukuaji wa uchumi wa kasi na usalama wa jumla, licha ya vitisho vya makundi ya kijihadi katika mipaka yake. Wakosoaji wanalalamikia kuwa ukuaji huo usiotiliwa shaka umewafaidi watu wachache tu, huku gharama ya maisha ikizidi kupanda kwa kasi.

Karibu waangalizi wa kiraia 1,000 kutoka asasi za kiraia wanachunguza uchaguzi huo, pamoja na wengine 251 kutoka jumuiya ya kiuchumi ya Afrika Magharibi (ECOWAS) na Umoja wa Afrika. Matokeo yanatarajiwa kutangazwa mapema wiki ijayo.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *