Chanzo cha picha, Getty Images
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imeeleza kusikitishwa kwake na chapisho la shirika la Amnesty International lenye kichwa cha habari “Unopposed, Unchecked, Unjust: ‘Wimbi la Ugaidi’ Laikumba Tanzania Kabla ya Kura ya 2025”, na inabainisha masikitiko yake kuhusu madai yaliyomo humo.
Imesema katika taarifa yake kuwa ingawa Tanzania iko wazi kwa ushirikiano wa kujenga na washirika wa kimataifa, inasikitisha kwamba Amnesty International imechagua kuchapisha madai makubwa na yasiyo na uthibitisho bila kuipa Serikali fursa nzuri ya kujibu kabla ya kutolewa kwake.
Hatua hiyo inadhoofisha kanuni za usawa na heshima ya pande zote ambazo zinapaswa kuongoza mazungumzo ya kimataifa ya haki za binadamu.
Taarifa hiyo imeeleza kuwa Tanzania inathibitisha tena dhamira yake thabiti ya kulinda na kukuza haki za binadamu, kama ilivyoainishwa katika Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 (pamoja na marekebisho yake), na kwa mujibu wa mikataba ya kimataifa na ya kikanda ya haki za binadamu ambayo Tanzania ni mwanachama, ikiwemo Mkataba wa Kimataifa wa Haki za Kiraia na Kisiasa (ICCPR), Mkataba wa Afrika wa Haki za Binadamu na Watu, na Mkataba wa Kupinga Mateso.
”Uwasilishaji wa taarifa hiyo kuhusu Tanzania kama nchi inayoruhusu kukamatwa kiholela, kutoweka kwa watu kwa kulazimishwa, na kukandamiza uhuru wa raia hauendani na mifumo ya kisheria na taasisi zilizopo. Tanzania inatekeleza sera ya kutovumilia kabisa mateso na aina nyingine za adhabu au matendo ya kikatili na ya kinyama”.
”Madai ya utovu wa nidhamu kama huo yanachunguzwa na mamlaka husika kama vile Tume ya Haki za Binadamu na Utawala Bora (CHRAGG), Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP), na Mahakama, sambamba na Sheria ya mwenendo wa makosa ya jinai, Kanuni ya Adhabu, na Sheria ya Jeshi la Polisi na Huduma Saidizi”.Ilieleza taarifa hiyo.
Sambamba na kanuni ya uwajibikaji, wale wanaohusika na hilo watashughulikiwa kwa mujibu wa sheria za nchi.
Serikali inasisitiza zaidi kwamba uhuru wa kujieleza, kukusanyika kwa amani, na upatikanaji wa taarifa zinalindwa chini ya Katiba na kusimamiwa kupitia sheria kama vile Sheria ya Huduma za Vyombo vya Habari, Sheria ya Upatikanaji wa Taarifa, na Kanuni za Maudhui Mtandaoni.
Sheria hizi zinatekelezwa kwa mujibu wa Kifungu cha 19 (3) cha ICCPR, ambacho kinaruhusu vikwazo vichache vinavyohitajika kulinda usalama wa taifa, utulivu wa umma, na haki za wengine.
Kuhusu mchakato wa uchaguzi, Tume Huru ya Kitaifa ya Uchaguzi (INEC) inafanya kazi kwa uhuru kama ilivyohakikishwa na Kifungu cha 74 (11) cha Katiba.
Tanzania inaendelea kuruhusu na kuwezesha waangalizi wa uchaguzi kuhakikisha uchaguzi unakuwa wa haki. Pia inashikilia misingi ya uwazi, kutokupendelea upande wowote, na ushiriki sawa wa kisiasa kwa watu wote.
Serikali ya Tanzania inasisitiza kwamba haikubaliani wala kuvumilia vitendo vya watu kupotezwa kwa kulazimishwa au mauaji yanayofanywa nje ya mfumo wa sheria.
Kila tukio linaloripotiwa huchunguzwa kwa kina na kuchukuliwa hatua za kisheria. Mahakama zinaendelea kuwa huru, na kila mtu ana haki ya kupata usikilizwaji wa haki kulingana na sheria za ndani na za kimataifa.
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania inathibitisha tena dhamira yake ya kuendeleza utawala wa kidemokrasia, kuheshimu utawala wa sheria, na kulinda haki za binadamu kabla, wakati, na baada ya uchaguzi mkuu wa mwaka 2025.
Tanzania inaendelea kuwa wazi kwa mazungumzo na wadau wote wanaotaka kushirikiana kwa nia njema, na inahimiza taasisi zote kuwasiliana moja kwa moja na mamlaka husika kabla ya kuchapisha taarifa zinazoweza kupotosha umma.