
Dar es Salaam. Singida Black Stars imetinga hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, baada ya kuifunga Flambeau du Centre ya Burundi mabao 3-1, katika mechi ya mkondo wa pili iliyopigwa kwenye Uwanja wa Azam Complex Chamazi, Dar es Salam.
Flambeau ilianza kupata bao kupitia kwa David Irishura kunako dakika ya 26, huku Singida ikijibu mapigo na kusawazisha dakika ya 55 ya kipindi cha pili kupitia kwa mshambuliaji nyota wa kikosi hicho raia wa DR Congo, Malanga Horso Mwaku.
Wakati timu hizo zikishambuliana kwa zamu, Flambeau ilijikuta ikicheza pungufu baada ya nahodha wa kikosi hicho, Amissi Asmani kuunawa mpira eneo la hatari na kusababisha penalti iliyopigwa na Clatous Chama na kuzama wavuni dakika ya 67.
Fursa hiyo ya Flambeau kucheza pungufu ilitumiwa vyema na Singida Black Stars ambayo iliendelea kulisakama lango la wapinzani wao na dakika ya 75, ilipata bao la tatu kupitia kwa Idriss Diomande na kuifanya kufuzu kwa jumla ya mabao 4-2, baada ya pambano la kwanza kutoka sare ya 1-1.
Singida ilianza hatua ya kwanza ya michuano hii kwa kuitoa Rayon Sports kutoka Rwanda kwa jumla ya mabao 3-1, huku kwa upande wa Flambeau iliyoaga rasmi katika Kombe la Shirikisho Barani Afrika ikiitoa Al Akhdar ya Libya kwa jumla ya mabao 4-3.
Kufuzu kwa Singida katika hatua ya makundi, inaifanya timu hiyo kuandika rekodi mpya na kuwa ya pili msimu huu katika michuano ya Kombe la Shirikisho Afrika kwa Tanzania, baada ya Azam FC kuiondosha KMKM ya Zanzibar kwa jumla ya mabao 9-0.
Mbali na Singida na Azam FC zilizofuzu hatua ya makundi ya Kombe la Shirikisho Barani Afrika, timu nyingine ni Yanga iliyofuzu kwenye Ligi ya Mabingwa Afrika, baada ya leo jioni kuiondosha Silver Strikers ya Malawi kwa jumla ya mabao 2-1.
Clatous Chama na Gadiel Michael sasa wanaingia katika historia ya kuwa wachezaji waliofuzu hatua ya makundi ya mashindano ya Klabu Afrika wakiwa na klabu tatu tofauti.
Wote wawili wamefuzu wakiwa na Yanga, Simba na Singida Black Stars kwa nyakati tofauti.