Dar es Salaam. Nimekumbuka mbali sana. Nimekumbuka enzi zile za methali kama “Koti la babu, halikosi chawa”. Kumbukumbu hizo zilinijia nikiwa na rafiki zangu katika moja ya kijiwe nongwa tunachopenda kukaa kila siku jioni baada ya kazi. 

Kumbukumbu hizo zilinijia baada ya kumuona mzee mmoja akiwa anatembea kwa madoido huku mwilini kavalia koti la suti, tai na suruali kaipandisha mpaka tumboni.

Mzee alinyata na kutembea kwa manjonjo. Baada ya kuuliza nikajibiwa siri ya mwendo ule ni nguo aliyovaa yaani suti. Kama kawaida ya kijiwe nongwa tukaanza kumjadili wapo waliodai  bado anaenzi thamani ya suti kwani zamani hizo vazi hilo lilikuwa likiheshimika sana na halikuvaliwa ovyo.

Wenye shuhuda za miaka hiyo ya nyuma wakaendelea kudai waliokuwa wakilivaa sana vazi hilo ni walimu na wanasiasa. Wakafananisha na sasa ambapo suti inavaliwa na kila mtu na cha ajabu koti na suruali kila kimoja hununuliwa sehemu yake. Hapo ndipo wakakazia kuwa vazi hilo limeshika thamani.

Lakini hapo hapo walikuwapo wale wa kupinga, wakadai suti bado ipo kwenye hadhi tena kwa sasa inatamba balaa. Mijadala hii ikafanya niendelee kukumbuka baadhi ya matukio kama lile la muuza kahawa ambaye vazi lake kuu ni suti wakati akifanya biashara zake na hata yule muuza mitumba ambaye huvaa suti wakati akinadi mitumba yake.

Haikuishia hapo kiherehere changu kuhusu vazi hilo kikanituma niwatafute wanamitindo na wabunifu mbalimbali wa mavazi. Ili nipate mitazamo yao kuhusu hadhi ya vazi hilo

Kwa upande wake mbunifu wa mavazi maarufu nchini Ally Rehmtullah anasema suti ni vazi rasmi unaweza kuvaa wakati wa mikutano au ofisini inategemea na aina ya kazi unafanya huku akikazia kuwa vazi hilo linapendeza katika mikutano au vikao maalumu.

“Suti inahusisha kuivaa pamoja ya shati la kuchomeka lenye mikono mirefu, suruali na jacket pamoja na tie. Kama suti ni ya kitamba ifanane na suruali na jacket. Sasa hivi ukiangalia watu wengi wanavaaa blazer na suruali. Hapo kitambaa cha suruali na blazer kinaweza kuwa tofauti.

“Hata mara nyingi vijana kwenye corporate companies wanavaaa jeans na blazer juu. Suti bado thamani yake ipo kwenye events za formal na kwa kazi za ofisini rasmi. Zamani hakukuwa na blazer siku hizi zipo kwa hiyo watu wengi wanachagua kuvaa suti juu mpaka chini au blazer na jeans, hali ya hewa ya jua pia inaweza kusababisha watu wasivae full suit na wanapendelea kuvaaa blazer,” anasema nguli huyo katika mitindo.

Hata hivyo mjadala huu uliendelea kwa mwanamitindo mwingine Marthin Kadinda ambaye kwa upande wake alidai thamani ya vazi hilo imeshuka.

“Suti ni vazi la heshima haliwezi kuvaliwa kila sehemu. Linampa mtu hadhi kutokana na wapi anakwenda, kwa sababu washonaji ni wengi linapatikana kirahisi  kwa hiyo thamani yake imepotea lakini kibiashara washonaji wanapata pesa. 

“Pia limeshuka kwa sababu zamani lilikuwa linavaliwa na wanasiasa. Lakini sikuhizi sehemu yoyote mtu unakuta kavaa suti kwenye graduation, kipaimara. 
Upatikanaji ni jambo jema lakini thamani imepungua. Nikikurudisha miaka kumi ilikuwa ukivaa suti basi una hadhi fulani lakini bado ni mavazi ambayo yanakubalika. Anasema Marthin huku akiongezea kuwa ili iwe suti lazima vazi la juu na chini viendane

Aidha kwa upande wake mbunifu mwingine wa mavazi Zamda George anasema Suti inategemeana inavaliwa wapi. Lakini bado ina heshima yake ingawa zipo sababu zinazofanya ionekane kama imeshuka hadhi.

“Kilichobadilika haioneshi heshima kwa sababu imeondoka kwenye upande wa kuwa rasmi inavaliwa sehemu yoyote. Na hilo ni kwa sababu wabunifu wamelifanya livalike sehemu zote. Tulizoea liwe zito, lakini zipo ambazo ukitaka kwenda nayo beach unavaa na snika na ukapendeza.

“Lakini pia imefanya mpaka vijana wavae. Zamani lilikuwa vazi la wazee tu, sasa hivi hata juu unaweza kuvaa mpaka na kofia na bado ukapata mwonekano bomba. Limebadilika kutokana na material na uvaaji. Hata mtu akivaa bado atasikilizwa kwa umakini, zamani ilikuwa ni za rangi ya kijivu na nyeusi lakini siku hizi hata rangi yoyote mtu anavaa. Na sio tu awe wa kiume anavaa hata mwanamke,” anasema Zamda.

Anasema fashion haina sheria kwa hiyo hata mtu akivaa suti na raba ni sawa tu na ndivyo wengi wanafanya kwa sasa.

Akifunga mjadala huo Noel Kaminyoge kutoka Dar Suits anasema suti haijashuka thamani na haiwezi kushuka.

“Upande wa wanaume hiyo ndiyo nguo ya mwisho kwa ukubwa inaheshimika na mwanaume yoyote. Mimi naona imepanda thamani ndiyo maana wafanyabiashara wameendelea kuongezeka, ina maana watu wana mwamko wa kuvaa suti. Zamani walikuwa wanavaa sehemu rasmi tu lakini kwa sasa ni tofauti hata wateja tunapata tofauti.

“Hata kwa wakristo ni vazi ambalo mtu akifariki ndilo huwa linachaguliwa kama vazi la kumpumzisha kwa hiyo kwa upande wa mwanaume inathamani. Siku zinavyozidi kwenda linazidi kupanda thamani siku hizi hadi zina maua tofauti na zamani rangi zilikuwa za ofisini tu. Ukitaka kuheshimika vaa suti ndiyo maana hadi madalali wanava suti,” anasema Noel .

Mbali na hayo mijadala hii yote ikanirudisha katika utafiti wa ‘The Philosophy of Elegance: The Value of a Tailored Suit’ uliochapishwa na Sartoria Litrico mwaka huu 2025, umeeleza kwa kina falsafa na thamani ya kuvaa suti iliyoshonwa maalum kwa ajili ya  mtu binafsi. 

Utafiti huo unaonesha suti si kama vazi la kawaida tu, bali ni alama ya utu, heshima, na kujitambua. Kuvaa suti iliyoshonwa kwa uangalifu hubadilisha namna mtu anavyojihisi na jinsi jamii inavyomtazama. Mtu aliyevaa suti huhisi kujiamini zaidi, anaonekana mwenye mamlaka, huheshimika hata bila kusema neno. 

Hii ni kwa sababu suti hubeba falsafa ya ubora, nidhamu na ustaarabu . Aidha utafiti mwingime wa ‘Dress, Body and Self: Research in the Social Psychology of Dress’ uliofanywa na Kim K. P. Johnson, Sharron J. Lennon, na Nancy A. Rudd mwaka 2014, ulionesha mavazi yanavyoathiri nafsi ya mtu, mtazamo wa jamii, na mahusiano kati ya mwili na utambulisho wa mtu.

Utafiti huu uliwasilishwa katika jarida la Fashion and Textiles na uliweka msingi wa kuelewa saikolojia ya kijamii na mavazi.

Kwa mujibu wa watafiti hao, mavazi si tu nguo, bali ni lugha katika jamii inayowasilisha ujumbe kuhusu utu, nafasi ya kijamii, tabaka, na hata uwezo wa mtu. Mavazi hubeba maana inayoweza kubadilisha jinsi mtu anavyojiona mwenyewe na jinsi wengine wanavyomtazama.

Utafiti ulibaini kwamba watu huathiriwa kisaikolojia na wanachovaa. Mtu anapovaa mavazi rasmi kama suti, akili yake hujipanga katika hali ya kujiamini, mamlaka, na uwajibikaji zaidi. Hii ni kwa sababu mavazi hayo yanahusishwa na heshima, madaraka, na ufanisi. 

Waavaaji wa suti

Akizungumza na Mwananchi Hamidu Sulle mkazi wa Tabata jijini Dar es Salaam anasema suti ni vazi lililompatia madili mengi.

“Mimi navaa suti sio kwa bahati mbaya. Hili vazi watu wanaona kama najichosha lakini limefanya watu wengi waniheshimu wananiona wa hadhi ya juu na hata nikiongea wanapenda kunisikiliza. Hadi sasa nina zaidi ya suti 20  na imekuwa kawaida yangu kushona hata kama sina mahala pa kwenda,” anasema.

Naye Rose John mkazi jijini humo anasema kitu kizuri ni kwamba wabunifu wa mavazi kwa sasa wanaangalia kila jinsia katika mavazi hayo.

“Zipo aina nyingi za suti kwa wanawake yani kilichopo ni uchaguzi wako tu kwamba unataka suti ya aina gani. Zipo za gauni, suruali na hata sketi kwa hiyo wanawake pia tumekumbukwa katika hilo na tunafurahia sana kwa sababu tukivaa tunakuwa na muonekano wa kitajiri,”anasema Rose.
 

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *