‎Dodoma. Viongozi wa dini kutoka mikoa ya Singida na Dodoma wamefanya dua maalum ya kuombea uchaguzi mkuu utakaofanyika Oktoba 29, 2025 na kuwataka wananchi kujitokeza kwa wingi kupiga kura ili kuwapata viongozi wataowaongoza kwa njia ya demokrasia.

‎Viongozi hao wa dini wameyasema hayo leo jumamosi Oktoba 25, 2025 jijini Dodoma ambapo pia waliomba amani kuelekea kwenye uchaguzi mkuu.

‎Akizungumza kwenye kongamano hilo, Shekhe wa Mkoa wa Dodoma, Mustapha Shaaban amewataka Watanzania kuwa wasikivu na watii kwa viongozi wao kwa mujibu wa maelekezo yanayotolewa kwa mujibu wa sheria.

‎”Oktoba 29 tujitokeza tukapige kura kwa ajili ya kuwachagua viongozi watakaotuletea maendeleo kwenye Taifa letu la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, kama maendeleo yaliyopo hivi sasa yaendelee kuwepo siku hadi siku tujitokeze tukapige kura kwa viongozi hao ambao tukiwa na kero ya maji, elimu, afya, umeme tutawafuata,” amesema.

‎”Lakini Alhamdulillah tuna utekelezaji wa asilimia 100 ya utekelezaji wa mambo hayo,” amesema Shekhe Shaaban.

‎Amewataka Watanzania kuwapuuza wanaohamasisha maandamano mitandaoni, kwani wanatafuta wafuasi wa kuwafuata kwenye mitandao yao ya kijamii ili walipwe pesa.

‎Naye Shekhe wa Mkoa wa Singida, Issa Nassor amewataka viongozi wa dini kusimamia maadili kwa waumini wao na kuacha kufuata mkumbo wa masuala ya kisiasa yanayoendelea nchini ikiwemo masuala ya utekaji.

‎Amesema kutokana na wimbi la utekaji lililopo nchini kuna baadhi ya viongozi wa dini (hakuwataja majina) wamejiteka na kuzua hofu na taharuki kwa jamii na familia zao lakini baada ya uchunguzi wa Jeshi la Polisi viongozi hao walipatikana na kuonekana kuwa hawakutekwa.

‎Amesema kwa kupitia dua na sala walizozifanya za kuombea uchaguzi mkuu viongozi wa dini mbalimbali wamejivua na lawama kwa wananchi, kwani wametimiza wajibu wao hivyo hawatalaumiwa kwa wale watakaovunja Sheria za nchi.

‎ Katibu wa umoja wa madhehebu ya Kikristo (CCT) Askofu Evance Chande amesema Tanzania imejengwa kwenye misingi ya maridhiano na amani hivyo Watanzania wanatakiwa kudumisha amani na utulivu kuelekea kwenye uchaguzi mkuu wa mwaka huu.

‎”Tumeshuhudia kampeni za wagombea wakinadi sera na ilani za vyama vyao kwa amani hivyo wajibu wetu ni kuombea amani kabla, wakati na hata baada ya uchaguzi maana amani ikitoweka hatuna nchi nyingine ya kukimbilia,” amesema Askofu Chande.

‎Askofu Mary Madelemu amewataka Watanzania kutubu mbele za Mungu ili aondoe ghadhabu yake na kuleta amani ambayo mataifa majirani ya Tanzania hawana.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *