
Bunda. Kada wa Chama cha Mapinduzi (CCM), Ezekiah Wenje, amewataka wananchi kuondoa dhana kwamba mtu anapohama kutoka vyama vya upinzani, hususan Chadema, na kujiunga na CCM, anapoteza sifa zote nzuri alizokuwa nazo kabla ya kuhama.
Wenje ameyasema hayo mjini Bunda leo Oktoba 2025, wakati wa kufunga kampeni za CCM, ambapo pamoja na mambo mengine, ametumia fursa hiyo kumuombea kura mgombea ubunge wa Bunda Mjini, Ester Bulaya, pamoja na wagombea udiwani na mgombea urais kupitia CCM.
Amesema kuwa ni mtu mpumbavu pekee anayeshindwa kubadili mawazo yake, hata akikabiliwa na ushahidi, na kwamba yeye ameona mbali na anakubaliana na baadhi ya hatua zilizochukuliwa na CCM katika kuboresha maisha ya wananchi, ndiyo maana aliamua kuhamia CCM.
Wenje ambaye alikuwa Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Ziwa Victoria amesema inasikitisha kuona kuwa mtu anapokuwa kwenye vyama vya upinzani anachukuliwa kama mtu mwenye busara, mwenye akili, mzalendo, msema ukweli na asiyekuwa na njaa lakini anapohamia CCM sifa hizo zinatoweka na inakuwa kinyume chake.
“Ester wala usiogope, umefanya uamuzi mzuri na sahihi wewe umefanya hivi kwa masilahi ya wananchi hawa tembea kifua mbele hakuna jambo baya umefanya,” amesema Wenje.
Amesema Watanzania wanapaswa kujifunza kupitia kwa mwanasiasa mashuhuri wa nchini Kenya, marehemu Raila Odinga ambaye aliamua kuweka tofauti zao pembeni na kujiunga na Rais wa nchi hiyo, Dk William Ruto kunusuru nchi yao.
“Raila alipoona Serikali ya Ruto inazama aliamua kuweka tofauti zao pembeni na kujiunga na Ruto kwa ajili ya kesho nzuri ya Kenya,” amesema.
Amesema mbali na mafanikio yaliyopatikana nchini kupitia CCM, lakini pia aliamua kujiunga na chama hicho baada ya kuona chama chake kikipoteza mwelekeo.
“Mwaka 2014 tulikimbia Bunge la Katiba tumekimbia uchaguzi sasa, nani ana uhakika Chadema watashiriki uchaguzi mwaka 2030, yaani mimi niendelee kukaa kwenye chama kinachokimbia uchaguzi, mimi ni mwanasiasa bwana,” amesema.
Wenje amesema wananchi wanapaswa kuachana na propaganda zinazoenezwa na baadhi ya watu kuwa Serikali ya CCM haijafanya chochote, kwani madai hayo sio ya kweli isipokuwa yapo mengi yamefanywa na mengine yanaendelea kufanywa na Serikali.
Amesema Bulaya anao uwezo wa kuwawakilisha wana Bunda bungeni, hivyo ni wajibu wao kumchagua kwa kura nyingi kwa ajili yao.
“Mimi siungi mkono watu goigoi, Ester namfahamu nimekuwa naye bungeni sina mashaka kabisa anafaa na kutosha kwa nafasi hii,mpeni kura akawafanyie kazi,” amesema Wenje.
Akizungumza katika mkutano huo, Bulaya amesema anagombea nafasi hiyo ili kuwatumikia wananchi huku akikusudia kuacha alama ya maendeleo endelevu kwa mji wa Bunda.
“Natamani kuacha alama, nataka siku nikilala nikizikwa pale Manyamanyama mje mseme kuna binti yetu alifanya mambo haya ya maendeleo tunayonufaika nayo,” amesema.
Amesema kuwa, akichaguliwa kuwa mbunge, jambo la kwanza atalilenga ni kuhakikisha mji wa Bunda unapata hadhi inayostahili, ambapo atahakikisha wanapata barabara za lami zenye urefu wa kilomita 23, stendi, na soko la kisasa. Miradi hii, anasema, ikikamilika itachangia kuboresha uchumi wa mji wa Bunda na maisha ya wakazi wake.
Amesema kuwa maendeleo hayana itikadi ya vyama vya siasa, hivyo wakazi wa jimbo hilo wanapaswa kumchagua mtu mwenye uwezo ili awe mwakilishi wao bungeni kwa maslahi ya jimbo zima.
Bulaya ameeleza kuwa uwezo wake wa kuwatumikia wananchi wa Bunda unaonesha kuwa maendeleo ya mkoa wa Mara na jimbo la Bunda yataletwa na wenyewe wana Mara.
Mgombea ubunge viti maalumu Mkoa wa Mara (CCM), Ghati Chomete, amewaomba wana Bunda kukipigia kura chama hicho kwa ajili ya maendeleo yao, akisisitiza kuwa CCM kinalenga maendeleo na si vinginevyo.
Amesema kuwa ilani ya uchaguzi ya CCM 2025/30 inatakelezeka, na kuongeza kuwa ilani hiyo imenadiwa vyema wakati wa kampeni katika kata zote 13 za jimbo la Bunda Mjini.
Chomete aliongeza kuwa, kwa kuwa wana Bunda ni watu wa maendeleo, basi CCM ndiyo chama sahihi kwao.