
Dar es Salaam. Yanga imeondoka katika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam leo Jumamosi, Oktoba 25, 2025 kifua mbele baada ya kuibuka na ushindi wa mabao 2-0 dhidi ya Silver Strikers ya Malawi ambao imeifanya itinge hatua ya makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.
Aliyeanza kuipa Yanga matumaini ya kutinga robo fainali jana alikuwa ni beki Dickson Job ambaye aliifungia bao la kuongoza katika dakika ya sita ya mchezo baada ya kuunganisha kwa mguu wa kulia kona ya Mohamed Doumbia.
Baada ya kuingia kwa bao hilo, Yanga iliendeleza kutawala mchezo na kupeleka mashambulizi ya mara kwa mara langoni mwa Silver Strikers ambayo hata hivyo safu yake ya ulinzi ilijitahidi kuzuia yasiwe na madhara makubwa langoni mwao.
Hata hivyo juhudi hizo za Silver Strikers kujilinda zilikwama katika dakika ya 33 pale Pacome Zouzoua alipoifungia Yanga bao la pili kwa mguu wa kulia akimalizia kwa shuti la wastani pasi ya Maxi Nzengeli.
Mabao hayo yalidumu hadi refa Adissa Ligali alipopuliza filimbi ya kuashiria muda wa mapumziko.
Katika kipindi cha pili, Yanga ilionekana kuendelea kumiliki mchezo na kutengeneza nafasi lakini nyingi ilizopoteza.
Kama Prince Dube angekuwa makini kutumia angalau nafasi moja kati ya nyingi alizopoteza, Yanga ingemaliza na idadi kubwa zaidi ya mabao hayo lakini nyota huyo wa Zimbabwe hakuwa na shabaha mbele ya lango.
Miongoni mwa nafasi hizo ni ile aliyopata katika dakika ya 78 ambapo alipewa pasi na Pacome Zouzoua akiwa analitazama lango lakini alishindwa kuumalizia mpira huo na ukaokolewa na walinzi wa Silver Strikers.
Hata hivyo, pamoja na nafasi nyingi ilizopotea, Yanga ilifanikiwa kulinda vyema lango lake na hadi filimbi ya mwisho ilipopulizwa, ilifanikiwa kuondoka na ushindi huo ambao umeifanya itinge hatua ya makundi.
Katika mchezo huo wa leo, Yanga ilifanya mabadiliko ya kuwatoa Mudathir Yahya, Mohamed Doumbia na Prince Dube ambao nafasi zao zilichukuliwa na Andy Boyeli, Edmund John na Offen Chikola.
Ushindi huo wa leo umeifanya Yanga kuvuna kitita cha Sh10 milioni ambacho ni fedha ya bonasi kutoka kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan.