Dar es Salaam. Zikiwa zimesalia siku tatu pekee kabla ya Watanzania kwenda kupiga kura kumchagua Rais, wabunge na madiwani, Chama cha Ukombozi wa Umma (Chaumma) kimeahidi kufuta tozo za daraja la Nyerere.

Wakijikita katika Jimbo la Kigamboni kwenye kampeni za kata kwa kata leo Jumapili Oktoba 26, 2025, mgombea mwenza wa urais wa chama hicho, Devotha Minja na mgombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni, Yeriko Nyerere wametoa ahadi hiyo wakisema ni kinyume na katiba ya Tanzania.

“Suala la kivuko hapa ni tatizo, mnatozwa tozo kuvuka daraja kwenda mjini kwenye shughuli zenu, hii si haki, mkituchagua Chaumma tutafuta gharama zote mvuke bila usumbufu,” amesema Devotha.

Mgombea ubunge wa Jimbo la Kigamboni, Yeriko Nyerere

Akitaja mikakati ya kufuta tozo hizo, mgombea ubunge wa jimbo hilo, Yeriko Nyerere amesema baada ya kuapishwa rais atakayetokana na chama hicho endapo atachaguliwa, atatangaza kusitishwa mara moja kwa gharama hizo.

“Tozo hizi hazifai na zinavunja ibara ya 13 ya Katiba ya Tanzania inayokataza kuwagawa watu. Serikali inawagawa wanaKigamboni kwa kuwatoza fedha kuvuka daraja wakati madaraja mengine zaidi ya 2,000 nchini watu hawatozwi tozo kama hizo.

“Sisi mkituchagua, rais, Salum Mwalim atatumia mamlaka ya urais, atatangaza kukoma kwa gharama hizo siku hiyo hiyo,” amesema.

Mbali na hilo, chama hicho kimeahidi kushughulikia tatizo la maji ambalo kimedai limekuwa kero sugu katika kisiwa hicho kilichozungukwa na maji ya Bahari ya Hindi pande tatu.

Akieleza mipango ya chama hicho ya kiuchumi katika wilaya hiyo, Devotha amesema Chaumma imelenga kujenga viwanda na kuimarisha sekta ya uvuvi na utalii ili kukuza uchumi.

“Kigamboni hapa inatakiwa kuwa na vitega uchumi imara na soko lake kubwa kama Kariakoo, inatakiwa kuwa na viwanda vikubwa ili kuwa na uchumi wake imara,” amesema Minja, akisisitiza mpango wa Chaumma wa kujenga viwanda katika eneo hilo.

“Tupeni Chaumma tukajenge uchumi wa Kigamboni, tuajiri vijana ili kila mwananchi apate nafasi ya kuboresha maisha yake,” ameongeza Devotha.

Mgombea mwenza huyo amesema Tanzania haipaswi kuwa na uhaba wa wafanyakazi katika sekta ya umma kwa kuwa wasomi wapo wa kutosha nchini.

Mgombea mwenza wa urais Chaumma, Devotha Minja

“Wasomi wamejaa mitaani, watafiti wanasema ualimu ndiyo fani inayoongoza kusomwa na watu wengi, lakini chini ya Serikali ya CCM shule zetu zina uhaba wa walimu, hospitali pia hazina wataalamu wa kutosha. Tupeni Chaumma tukawaajiri vijana wetu kumaliza kero hii.

Akimuombea kura mgombea ubunge wa jimbo hilo, Devotha amesema Yeriko ndiye kijana anayestahili kuwakilisha jimbo hilo bungeni kwa kuwa anazijua changamoto zake.

“Oktoba 29, nendeni mkamchague Yeriko Nyerere akawapiganie, aende akawasemee matatizo ya ajira, akatetee mahitaji ya maji, mikopo ya kinamama na kuwaondolea kausha damu,” amesema Devotha.

Awali akiomba kuungwa mkono na makundi mbalimbali, Yeriko ameahidi kuboresha mazingira ya uvuvi na biashara za mama lishe na waendesha bodaboda.

 “Mkinichagua nitajenga bandari tano za uvuvi ndani ya jimbo hili, kuboresha miundombinu ya barabara ili tuvutie utalii wa uvuvi,” amesema.

Akisisitiza hoja hiyo, Devotha amesema serikali ya Chaumma itakopesha boti za uvuvi kwa vijana wa Kigamboni ili wafanye uvuvi wenye tija na kujiongezea kipato.

Kuhusu tatizo la maji, Yeriko ameahidi kushughulikia kero hiyo akitaja mikakati yake.

“Kigamboni tunazalisha sehemu kubwa ya maji yanayohudumia Dar es Salaam, lakini sisi tuna uhaba wa maji, mkinichagua nitamaliza kero hii,” amesema.

“Kuhusu mama lishe, bodaboda na wajasiriamali, mimi mkinichagua nitapigania uhuru na masilahi yao ili waweze kufanya kazi zao kwa urahisi na kupata faida ya jasho lao,” ameongeza.

Kuhusu ardhi, Yeriko amesema Kigamboni ni kati ya maeneo yenye migogoro mingi ya ardhi akianika mkakati wa kushughulikia kero hiyo endapo atachaguliwa.

“Katika kuratibu migogoro ya ardhi, tutahakikisha ardhi yote Kigamboni inapimwa na kurasimishwa kwa wananchi. Ikiwa kuna mradi wa uwekezaji, mwananchi mwenye eneo hilo atanufaika na uwekezaji huo kama mmiliki mwenza wa mradi husika.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *