Unguja. Mgombea urais wa Zanzibar kwa tiketi ya Chama cha Mapinduzi (CCM), Dk Hussein Mwinyi, amehitimisha safari yake ya siku 43 kusaka kura za kumrejesha madarakani, huku akiwataka wananchi kumchagua chama hicho, akisema ndicho chenye uwezo wa kusimamia amani na kuleta maendeleo.

Mgombea huyo alizindua kampeni za chama hicho Septemba 13, 2025, katika viwanja vya Mnazimmoja, Mkoa wa Mjini Magharibi, na kuzunguka mikoa yote mitano.

Katika mikutano hiyo, Dk Mwinyi amefanya mikutano mikubwa ya hadhara mitano na mingine midogo, ambapo alikutana na makundi mbalimbali.

Akizungumza katika ufungaji wa kampeni hizo leo Oktoba 26, 2025, katika viwanja vya Mnazimmoja, Dk Mwinyi, kama alivyoanza, amemaliza kwa kutaja vipaumbele 10 watakavyotekeleza baada ya kuingia madarakani.

Amesema wataendelea kuwaunganisha Wazanzibari na kudumisha umoja, amani, utulivu, ushirikiano, maridhiano, na uvumilivu.

Pia amesema watajenga uchumi imara unaozingatia usawa na kunufaisha maeneo yote ya Zanzibar.

“Tutaimarisha upatikanaji wa ajira kwa vijana kwa kuzalisha ajira 350,000 katika sekta rasmi na isiyo rasmi ifikapo mwaka 2030,” amesema Dk Mwinyi.

Kipaumbele kingine ni kuhakikisha uhakika wa chakula kupitia Hifadhi ya Taifa ya Chakula na kuongeza uzalishaji wa ndani kupunguza utegemezi wa kuagiza nje ya Zanzibar.

Kwa mujibu wa Dk Mwinyi, wataimarisha uwezeshaji wa wananchi kiuchumi kupitia mikopo, matumizi ya teknolojia, na mafunzo ya umahiri.

“Tutasimamia uanzishaji wa makazi bora na miji ya kisasa kwa kuzingatia teknolojia mpya ya ujenzi, mipango ya miji, na usafi wa mazingira,” amesema Dk Mwinyi.

Kipaumbele kingine ni kuanzisha hifadhi ya kitaifa ya mafuta ili kuhakikisha upatikanaji endelevu na kupunguza athari za mabadiliko ya bei.

Iwapo wakipata ridhaa, wataweka vivutio maalumu vya uwekezaji katika sekta kuu za uchumi kama uchumi wa buluu, viwanda, kilimo, na huduma.

Kingine ni kuendelea kuimarisha upatikanaji wa huduma za jamii, ikiwemo elimu, maji, na umeme, pamoja na kuimarisha hifadhi ya jamii kwa wananchi wote.

Amesema kuna mradi mkubwa wa maji wa Dola milioni 55 za Marekani, ambapo wanatarajia kusaini mkataba wa kuanza ujenzi wake.

Mbali na mradi huo, pia amesema wanatarajia kusaini mkataba wa kujenga hospitali maalumu.

“Kupitia vipaumbele hivi, kinaonesha dhamira ya kujenga Zanzibar yenye maendeleo ya kweli, usawa wa fursa, na ustawi wa kila mwananchi bila kuacha mtu nyuma,” amesema Dk Mwinyi.

Kwa upande wa michezo, amewaahidi vijana wakae mkao wa kula, akisema Serikali ya CCM itajenga mji wa viwanja vya michezo.

“Hivyo ndugu zangu, hasa vijana, kaeni mkao wa kula; mambo mazuri yanakuja. Haya yote yatafanyika mara tu nitakapoingia madarakani kwa kipindi kingine,” amesema mgombea urais huyo.

Amesema wamefanya kampeni za kistaarabu na kuyafikia makundi yote, haoni sababu ya CCM kushindwa kwa kishindo katika uchaguzi huu.

“Ndugu zangu, kama tunavyojitokeza katika mikutano hii, tujitokeze siku ya kupiga kura, mkipigie Chama cha Mapinduzi tushinde kwa kishindo,” amesema.

Naibu Katibu Mkuu wa CCM Zanzibar, Dk Mohamed Said Dimwa, amesema kuchagua CCM na Dk Mwinyi ni sawa na kuchagua maendeleo.

“Dk Mwinyi ni daktari wa binadamu na daktari wa maendeleo, kwa hiyo, mkichagua yeye na CCM mnakuwa mmechagua maendeleo,” amesema Dk Dimwa.

Leave a Reply

Your email address will not be published. Required fields are marked *